The Chant of Savant

Thursday 10 October 2013

CCM : Sitta anapompigia mbuzi gitaa

MWANASIASA machachari,  Samuel Sitta ambaye ni spika wa zamani wa bunge na Waziri wa  Jumuia  ya  Afrika  Mashariki  alikaririwa hivi  karibuni akikirushia Chama chake Kimondo.  
“Tumepoteza hadhi ya nchi yetu, ni aibu kusikia kuna vijana wa Kitanzania zaidi ya 600 waliopo katika magereza mbalimbali duniani kwa sababu ya suala la dawa za kulevya.” Asemacho Sitta kina ukweli usiopingika ingawa anampigia gitaa mbuzi.
Chama Cha Mapinduzi (CCM), tangu kilipotekwa na mafisadi, kama alivyowahi  kudai  mwanzilishi  wake  Marehemu  Baba wa Taifa Mwl Julius Nyerere, imepoteza si uwezo wa kuona bali kusikia, kuelewa, kubadilika hata  kusoma  alama  za  nyakati.  Sitta  anaijua  CCM vizuri. Imemlea na kumkuza hadi kufikia utu uzima kiumri na kisiasa. Hivyo, anachosema kina mashiko.
Hata hivyo ni vizuri kumpa ushauri nasaha wa bure Sitta.  Kwanza, afahamu kuwa CCM imefikia mahali ambapo wahenga husema:
 Kamba hukatikia pabovu. Huwezi kutegemea CCM inayoishi kwa kutegemea michango na ufadhili wa wanufaika wa jinai kama vile ufisadi, ujambazi, madawa ya kulevya, magendo na jinai nyingine kuukata mkono unaoilisha. Rejea kukwama kwa zoezi la kukamata majambazi lililowahi kuanzishwa na serikali ya rais Jakaya Kikwete. 
Zoezi hili lilisitishwa baada ya kugundua kuwa kumbe baadhi ya watu waliohusika na ujambazi walikuwa wafadhili wakubwa wa CCM. Sitta anajua fika kuwa watu kama Alex Massawe anayeshikiliwa nchini Dubai kwa kujihusisha na jinai alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kukamatwa kiasi cha kuushangaza umma. Baada ya wakubwa kugundua kuwa wanawakamata wasitiri wao, waliamua kuliua zoezi hili kimya kimya.
Pili, Sitta afahamu kuwa CCM ya sasa imeshachoka kiasi cha kutoweza kurejeshewa nguvu. Hakuna ubishi. CCM kwa sasa iko ICU au chumba cha wagonjwa mahututi huku wakuu wake wakijaribu kila mbinu bila mafanikio. 
Hebu tuangalie kauli nyingine ya Sitta, aliyekaririwa akisema, “Inaumiza tunapoelekea mwaka 2015 kwenye uchaguzi mkuu tunawashabikia viongozi walioliingiza Taifa letu katika mikataba mibovu, zabuni za upendeleo na wengine bado wamewatumia vijana kama punda kubeba dawa za kulevya.” Huu nao ni ukweli usiopingika na hakuna anayeweza kusema madai haya yanamlenga  mtu fulani kutokana na chuki na mashindano ya kisiasa. 
Mfano, nani asiyejua kuwa wanasiasa kama Edward Lowassa, Andrew Chenge na makundi yao waliliingiza taifa kwenye mikataba ya kijambazi,   kubwa lao ukiwa ufisadi wa Richmond iliyokwapua mamilioni ya shilingi huku ikisababisha mgao wa umeme na kupanda gharama za umeme? 
Sitta anajua fika kuwa watu hawa walipatikana na hatia chini ya Kamati aliyounda kuwachunguza. Lakini kutokana na ushirika na ukaribu wao na wakubwa, bado wanaendelea kupeta wakipewa hata nyadhifa za juu chamani. 
Huu ni ushahidi tosha kuwa CCM haiwezi kuvunja ndoa yake na mafisadi kwa vile inanufaika na jinai waliyotenda. Nani hajui, kwa mfano tenda ya ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara ilitolewa kimagendo na kinyemela kwa manufaa ya CCM? Nani anahoji hili ndani ya chama?
Sitta haongei bila ushahidi hata kama ni wa jumla na kimazingira. Kwa mfano anasema, Siku hizi baadhi ya viongozi wa siasa wanajisifia kumiliki magari ya kifahari na nyumba za kisasa wakati enzi za Mwalimu viongozi walikuwa wanaogopa hata kutaja kama wanamiliki nyumba au gari.” Nani hajui kuwa hawa wanaotukoga kwa majumba na magari ya kifahari wameiba vitu hivi toka kwetu? 
Rejea jinai ya wabunge na mawaziri kujiuzia nyumba za serikali kwa bei ya kutupwa.
 Rejea baadhi ya wakuu wa wizara kujiuzia magari ya umma kwa bei ya kutupa. 
Na ni mara hii kasahau kwa mfano hujuma iliyotendwa na Hilda Gondwe akiwa Ofisa Tawala wa mkoa wa Kilimanjaro ambaye hivi karibuni ameteuliwa kuwa mjumbe wa kamati ya maadili ya viongozi wa umma. 
Gondwe alijiuzia gari  aina ya Toyota Land Cruiser VX iliyokuwa imenunuliwa miaka mitatu kabla kwa shilingi 155,000,000 za Kitanzania  akalinunua kwa shilingi milioni moja akiwa amelitia taifa hasara ya shilingi 149,000,000 hapo Mei 2010. 
Ni ajabu kiasi gani kwa mtu kama huyu eti kuteuliwa na rais ambaye ni Mwenyekiti wa CCM kushika wadhifa unaohusiana na maadili wakati hana maadili yoyote zaidi ya madili? Je aliyemteua Gondwe hakujua tuhuma zake au aliamua kwa sababu anazojua kufunika kombe na mwanaharamu akapita na kupeta kama wasemavyo watoto wa mjini? 
Hivyo, ifahamike kuwa Sitta anapodai viongozi wanashinda kutukoga kwa majumba na magari walivyotuibia anajua anachosema. Ushahidi wa hili ni kwamba hakuna atakayemjibu ili kuogopa kuchokoza mengine mengi. Hivyo, wahusika watajifanya hayawahusu ili kashfa zao ziendelee kusahaulika.
Sitta aliongelea jambo jingine muhimu ambalo ni ile tabia ya wanasiasa walioibia umma kutumia chumo la wizi kuwanunua wapiga kura. 
Kuna mbinu nyingi chafu zinazotumika kwa sasa mfano, kufadhili vikundi vya akina  mama na vijana, kufadhili miradi ya madhehebu ya dini. Kwa juu ya hili linaweza kuonekana kama mapenzi ya maendeleo kwa umma. 
Kisichowekwa wazi ni jinsi wahusika walivyopata hiyo pesa na kwa nini wawe na uchungu na watanzania wakati wa kuelekea uchaguzi. Sitta anajua fika jinsi wengi wa wanasisasa wanaomwaga pesa hovyo hovyo walivyo wezi na mafisadi wakubwa wanaopewa pesa na mafisadi wengine wasiotaka kujulikana ambao wako kwenye mitandao yao. 
Tunampongeza Sitta kwa kuwa mwiba kwa wezi hawa hata kama naye ana mapungufu yake kama vile kuendelea kukaa kwenye chama anachojua fika kimeishafilisika kulhali. Hivyo basi kuna haja ya kumuunga mkono Sitta hasa anapopendekeza jibu mujarabu kwa matatizo yetu ambalo ni kuandikwa katiba mpya isiyochakachuliwa kama muswada uliopelekwa kwa rais kusaniwa pamoja na kupitishwa kinyume cha sheria.
Tumalizie kwa kusema kuwa Sitta japo anampigia mbuzi CCM gitaa, watanzania wanaweza kutumia nasaha zake kuiadhibu CCM kwa kutotaka kubadilika.
Chanzo:Dira ya Mtanzania Oktoba 2013.

No comments: