The Chant of Savant

Wednesday 20 March 2013

Chanzo cha umaskini wetu ni utawala wetu

HiVI karibuni kuliripotiwa habari kuwa msafara wa Naibu Waziri wa Maji, Binilith Mahenge ulipata ajali baada ya gari mojawapo katika msafara ule kumgonga mtoto Adam Ramadhani huko Muheza. Waziri alikuwa wilayani humo kukagua miradi ya maendeleo.
Japo ni kazi ya waziri kukagua miradi ya maendeleo, ukiangalia kwa undani, mazoezi kama haya yanalitia taifa hasara. Si uzushi. Siku hizi karibu kila mwenye kacheo kake ni mkubwa kiasi cha kuhitaji msafara wa magari.
Kwa kiasi fulani tumegeuka nchi ya wapenda sifa na misafara vitu ambavyo vinasababisha matumizi mabaya ya pesa za walipa kodi wetu maskini.
Inashangaza kuona nchi maskini kama zetu zinakuwa na matumizi ya ajabu na kijinga wakati nchi tajiri hazifanyi hivyo.
Nitoe mfano. Katika nchi tajiri, waziri au mbunge hapewi dereva wala mlinzi au wabeba mikoba (wasaidizi).
Anaendesha gari lake mwenyewe na sifa mojawapo katika kugombea ubunge lazima ajue kuendesha.
Hii inalenga kuokoa pesa za walipa kodi.
Inakuwaje tunafuja pesa ya umma, mfano, kwa kutoa walinzi ofisini na nyumbani, madereva, makatibu muhtasi na vikorombwezo vinginevyo vingi wakati bajeti yetu inategemea kuomba?
Hata wabunge na mawaziri wa nchi tajiri, licha ya kuendesha magari yao wenyewe, hawatumii magari ya bei mbaya kama ya wabunge wa nchi maskini kama yetu.
Ukiangalia Tanzania, unashangaa mantiki na busara ya kufuja mali ya umma namna hii.
Mkuu wa wilaya, mkoa, idara, wizara, mbunge na waziri wote wana misafara kila waendeko. Na watembeleapo eneo fulani basi wakubwa wa eneo husika wataacha kazi zao na kushiriki misafara hii ya hasara na ya kizamani.
Wanatumia magari mengi bila sababu huku wakifuja mafuta na kuchafua mazingira na kusababisha umaskini kwa walipa kodi bila sababu.
Kimsingi, nchi yetu inaendeshwa kisiasa badala ya kiuchumi. Wanasiasa wana sauti kuliko wachumi na mambo ya kisiasa yanapewa kipaumbele zaidi yale ya kiuchumi. Namna hii hatuwezi kuendelea.
Ukiachia ugonjwa wa kupenda misafara na sifa, kuna tatizo jingine la wanasiasa kuwatumia wananchi katika mambo yasiyo na tija kwa taifa hata kusababisha kusimamisha uzalishaji.
Mfano, unapowatoa watu maofisini na watoto mashuleni kwenda kumpokea mkubwa unategemea nini kama siyo kusimamisha uzalishaji na kuathiri uchumi?
Unapopoteza muda mwingi kwa kufunga barabara kwa vile wakubwa watapita wakitoka au kwenda uwanja wa ndege unategemea nini?
Ni ajabu kuwa bado tuna utapiamlo na hang over ya kikoloni ambapo akija kutembea kiongozi wa taifa jingine tunapoteza muda mwingi kwenda kumlaki kwa ngoma na makando kando mengine yasiyo na umuhimu. Zama za kuchezeana ngoma na ngojera zilishapita.
Kwa wenzetu, tena wenye nguvu ya kiuchumi, hata akija kiongozi wa nchi nyingine anamalizana na mwenyeji wake bila kupoteza muda na kusababisha hasara kwa uzalishaji na uchumi wa nchi. Ili nieleweke, jirejeshe kwenye mapokezi mengi yanayofanywa na rais wa Marekani kwa viongozi wa mataifa makubwa.
Huwa wanafika uwanja wa ndege na kupokelewa na kikundi kidogo cha watu huku wakikagua gwaride la kikosi kidogo kimoja na mambo yanaishia pale.
Huwezi kuona maelfu ya watu wa Washington eti wakijipanga kando ya barabara kumpokea kiongozi wa taifa jingine.
Hata rais anapokuwa akisafiri au kurejea nyumbani, huwezi kuona baraza lote la mawaziri uwanja wa ndege likienda kumpokea. Kwa lipi iwapo anachofanya ni kazi aliyoomba?
Inashangaza kuona viongozi wetu wanaosifika kusafiri sana hawajifunzi vitu kama hivi.
Badala yake wanaendelea na tabia za kikoloni kama zile zilizokuwa zikionyeshwa na gavana wa kikoloni.
Kwa taarifa yenu, gavana alikuwa akifanya aliyofanya ili kutudhalilisha na kutupotezea muda ili atunyonye vizuri.
Ni bahati mbaya kuwa watawala wetu wanaabudia mambo haya ya kihasara kuliko kubadilika.
Hebu jiulize, mfano, misafara, makongamano na hafla za kujipongeza zinakula kiasi gani kwa mwaka katika bajeti ya taifa?
Je ni fedha kiasi gani inatumika kununulia mafuta ya magari yanayotumika kwenye misafara isiyo na ulazima kama vile kumsindikiza na kumpokea mkubwa uwanja wa ndege?
Kuna haja ya kuiga na kufanya mambo ya maana badala ya kuendelea kuwa maskini tena kwa kujitakia huku tukidhalilika kwa kuombaomba na kukopakopa.
Ajabu, wakati tukifanya hii israfu, tunawashauri watu wetu wafunge mikanda na kuwaaminisha kuwa hali ya uchumi ni mbaya.
Hakuna hali mbaya zaidi ya ubaya wa akili na matumizi yetu kimfumo.
Kuna haja ya kufumua huu mfumo tuliourithi toka kwa wakoloni na kufanya mambo kama taifa na watu walio huru kiakili na kisiasa. Vinginevyo tutaendelea kutawaliwa kwa ujinga wetu.
Huwezi kutumia zaidi ya unavyopata ukawa huru. Huwezi kutumia kama mfalme wakati wewe ni kapuku ukaheshimika hata ukijiridhisha kuwa unaheshimika.
Heshima ya mtu ipo katika uhuru wake si wa kisiasa tu hata wa kiuchumi.
Hili unaweza kuliona wakati marais wa nchi maskini wanapotembelea mataifa makubwa.
Hawapokelewi uwanja wa ndege na wenyeji wao kama wao wanavyowapokea na hata wakiwapokea huwa tofauti na wanavyowapokea. Maisha mazuri ni nipe nikupe. Unakwenda kutembelea nchi tajiri unaingizwa ikulu kupitia mlango wa nyuma. Kwanini mhusika akija kukutembelea ukamtendea hivyo badala ya kujidhalilisha?
Wenzetu wanavyowapokea watawala wetu wanawaonyesha kiwango cha hadhi yao kwao.
Obama akimpokea rais wa Urusi au Ufaransa inakuwa issue kwenye vyombo vya habari nchi nzima. Lazima hafla ya kitaifa ifanyike na kuonyeshwa. Lakini kwa ombaomba wa kiafrika hilo sahau.
Kuna haja ya kuanza kuwaainisha maadui wa maendeleo yetu
Ingawa tumekuwa tukiwalaumu wakoloni na nchi mabeberu, kimsingi chanzo cha umaskini wetu ni mabeberu wetu wenyewe yaani watawala wanaopenda ukubwa, sifa na matanuzi.
Chanzo: Dira Machi, 2013.

1 comment:

Anonymous said...

MSEMA KWELI HUTUNZWA