Ya kule mwisho wa reli tuliyasikia ndata wawili walipomdedisha mlevi mmoja. Kisa? Alikuwa anawadai uchache. Badala ya kumlipa vijisenti walimlipa kipigo kilichomnyotoa roho. Kumbe akina Kamuhaanda wako wengi siyo?
Kwanza, ngoja nimlilie kidogo Daud Mwangosi aliyenyotolewa roho na akina Kamuhaaanda. Ee mwenyezi Mungu nilipizie kisasi kwa mabazazi wanaonyotoa roho za waja wako wasio na makosa.
Tuendelee. Juzi nilinyaka habari kuwa walevi wameanza kuwachoma moto ndata baada ya kugeuka vibaka, majambazi na majangili. Rafiki yangu aliyeko kule Ngala alinitumia mikanda miwili jinsi ya ndata walivyonyotolewa roho baada ya kumnyotoa rho mlevi mmoja huku wengine wakiuawa kule Nk’aagwe baada ya kutaka kudhulumu vipusa.
Ni ajabu kusikia kuwa kumbe hata ndata wanafanya biashara ya pembe za ndovu! Kama hili ni hivi jamani nani anatawanusuru hawa wajomba zetu—tembo? Walevi tulizoea kuwaona ndata wakiwatoa kitu kidogo na kitu kikubwa wauza gongo. Baada ya kuanza biashara ya mibwimbwi hasa ilipoanza kuwahusisha wanono, wanene na wazito, tulishuhudia ndata nao wakipata chao kwa kuwatoza ushuru wauza bwimbwi. Anayebisha aende mitaa ya Mnazi Mmoja aone jinsi wale wamama wanaouza mibwimbwi wanavyokata ka-laki kila afendi akibisha hodi mlangoni. Asiyejua chesi zima ni kwamba baada ya ndata kugundua kuwa wadingi wao wanahusika na mibwimbwi nao wakaona wajiweke karibu na wauzaji huku wakiachia miteja iteketee.
Kama ndata na wadingi wao wasingekuwa washirika wa biashara hii, unadhani ungeona teja hata moja mitaani likitanua na kutanuka? Unajua siri ya Mkulu kusema kuwa ana orodha ya vigogo wa mibwimbwi? Kwa taarifa yenu Njaa Kaya alichosema kuwa anawajua wauza bwimbwi na ana orodha yao si uongo wala usanii. Kwa taarifa yenu mimi ndiye nilimpa ile orodha. Nilimpa lini na wapi? Msiniulize kwani sitaki umbea na isitoshe hii ni kile ambacho wataalamu huita top secret ya confindential. Are you there dudes? Mdingi knows everything and he monitors almost every move to see to it that he is not suffering any loss.
Samahani. Nimenogewa na kikameruni nikasahau kuwa siyo lugha ya kaya ya taifa. Anyways, ninachotaka kusema ni kwamba hata huu ujangili na ujambazi wa ndata msidhani ni jambo la kuzuka tu. Umekuwapo muda mrefu. Jamaa yangu anayefanya kazi kwenye mbuga za wanyama tangu enzi za Ruksa na Ndongara Muhunidini anasema kuwa kama walevi wangejua kinachoendelea kule huenda wangejinyotoa roho kwenye kile ambacho kingeitwa mass suicide au kujinyotoa roho kwa halaiki. Kwa wale ambao walikuwa bado makinda ni kwamba genge la Ruksa na Muhunidini ndilo lililomnyotoa roho mwandishi Stan Katabaro aliposhupalia ujambazi na ujangili wao. Nani mara hii kasahau majina kama Brigedia Ali na Ortello Business Coop yaliyovuma wakati wa utawala wa Ruxa? Nani hajui kuwa usafirishaji wa wanyama na nyara za kaya unafanywa chini ya ushirikiano wa ndata na idara za mipakani na forodha? Shauri yenu nyie endeleeni kudanganywa huku mkiliwa.
Tangu wakati ule wanyama wameendelea kuuawa huku baadhi ya majambazi na majangili wenye madaraka wakizidi kuneemeka. Waulize akina Pio Msekua, Khatiiib, Menghjii, Lazaro Nyalando, Eze Maige na wengine wenye ulaji wao kule maporini. Wanyama wanauawa ukiachia mbali kusafirishwa nje. Najua wengi watasema nachonga nikimaanisha wale wanyama waliouzwa na yule habith wa kihindi Umangani kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mkia. Hao ni cha mtoto. Kuna wanyama ambao kwa kitaalamu tunawaita exotic ambao wanauzwa kimya kimya bila walevi kujua. Hivi mnajua kuwa kenge, nyoka, kobe, mijusi hata nguchiro ni big deal kwenye baadhi ya nchi? Shauri yenu. Mkiona watu wanaukata na kuula mnadhani ni ngekewa msijue kumbe wanawaibieni. Hebu angalia viwanja vilivyoota mbawa. Ukigusa kijiwanja tena uchochoroni uswazi uaambiwa milioni hamsini! Bado hujajenga. Wenzenu wanaangusha mije ngo ya kutisha nyinyi mnapanga mbavu za dog.
Ukiona akina Eze Maige na Lazaro Nyalando wanaangusha mihekalu unadhani njuluku wamepata wapi kama siyo kwenye ujangili na ujambazi huu? Hata hao ndata unaoona wanavaa buti zilinazotembea soli upande usidhani ni walalahoi kama wewe. Ni matajiri wa kutupwa. Wanafanya usanii kujificha nyuma ya uchovu lakini ukweli ni kwamba si wachovu kama wanavyoonekana. Hii Danganyika na Danganyana bwana. Unaweza kuona njemba ikifanya kazi ya kichovu yenye mshahara kiduchu lakini ikaangusha hekalu la mabilioni na kumilki migari ya bei mbaya ubaki kushangaa. Wapo wengi sana kiasi cha kugeuza kaya kuwa kaya ya majambazi na majangili. Nani aulize wakati ujanja kupata hata kama kwa kushikishwa ukuta?
Kaya yetu imegeuka ya majangili kuanzia juu kwenda chini. Kila mtu anajitahidi kuwa jangili iwe ni kwa kuuza wanyama, watu hata kujiuza yeye mwenyewe hasa wale wa kiwango cha chini kama watoto wa shule. Unashangaa kuona kibinti cha shule kinamilki simu ya bei mbaya huku kikiwa na credit muda wote. Je kinafanya kazi gani ya kukipatia kipato kama siyo kufanya ujambazi na ujangili wa kujiuza? Hayo tuyaache.
Nani mara hii kasahau nyara zilizowahi kukamatwa sehemu mbalimbali za kaya tena zikiwa ima zimepakiwa kwenye magari ya sirikali au ndata? Nani mara hii kasahau sakata la kukamatwa kwa maafisa wawili ndata huko Mugumu waliokuwa wakitokea Biharamulo mnamo tarehe 5 Januari 2013? Mbona hata majina yao yanajulikana kuwa ni Kulwa na Nyarata?
Funga kazi ni ujambazii uliotokea hivi karibuni kwenye jiji la walevi la Dar –alaa-si-Salama maeneo ya Msimbazii. Wajue nini kilitokea? Si majambazi yalikuja kwenye kituo cha kuuzia wese baada ya kupewa inshu na wahudumu wa ndani kuwa kutakuwa na mshiko ukisafirishwa benki. Wazee wa kazi walipoingizana na kuishia na madafu kama vimilioni 150, si kikanuka hadi ndata kuingilia. Wacha shaba zitembezwe mbichi mbichi. Walevi walidhani jamaa walikuwa wamekuja kuokoa zile njuluku wasijue kuwa ndata nao walikuwa na lao. Si baada ya kuwazidi nguvu majambazii wenzao ndata wakaishia na zile njuluku. Hadi leo naambiwa eti ndata watano wako lupango kwa kushukiwa kuiba njuluku zile. Je hawa ni ndata au majambazi tu?
Acha mie niende kujililia. Maana ndata wanapogeuka majambazi na majangili waweza hata kuuza vichwa vya watu hasa zeruzeru.
Eti gongo ni pombe? Kwaheri!
Chanzo: Tanzania Daima Januari 16, 2013.