The Chant of Savant

Wednesday 12 December 2012

Tuliposherehekea miaka 51 ya udhuru!


TANGU tupate udhuru sorry uhuru miaka zaidi ya 50 iliyopita, walevi walidhani kungekuwa na angalau kitu cha kusherehekea. Kwa hali si hiyo. Tuna uhuru kweli?
Hata hivyo uhuru huo unao wenyewe wanaoweza kuhomola na kuiba bila kuguswa. Wanaoweza kuua bila kuguswa ukiachia mbali kujifanyia madudu ambayo hata wadudu hawajayafikia pamoja na ududu wao. Tunazidiwa hata na wadudu wana uhuru. Hata hivyo na wadudu watu wana uhuru wa kubungua mali zetu kuanzia madini, wanyama, fedha hata afya zetu.
Waliosherehekea uhuru wakati sisi tukisherehekea udhuru wanajulikana. Walialiakana wakala na kunywa damu na pombe zetu huku sisi tukijichana maji ya madimbwi na visima vitoavyo maji vyooni. Hamjaona wanaotiririsha vinyesi mitaani hasa huko uswekeni? Je huko walevi wanakunywa maji au mavi yaliyochanganyikana na maji. No ni maji yalichanganyikana na mavi you name it.
Mjadala wenyewe ulianzishwa na Dk. Mpemba pale alipokuja na kuanza kutushangaa. Alisema, “Nyie hamwendi uwanja wa Uhuru kushereheekeaa Uhuru?”
Hata kabla ya kuendelea Dk. Kapende alidakia, “Uhuru ulikuwa ule wakati wa mzee Nchonga. Huu uhuru au udhuru?”
Dk. Mgosi Machungi hangoji. Anakatua mic, “Ami umesema kwei kabisa. siku ile ya uhuu niikuwa pale Mnazi Mmoja. Tilikula na kunywa hadi tikapuu. Lakini tangu mzee Mchonga ang’atuke na kuwaachia vibaka uhuu uligeuka uzuu,”
‘Sema Udhuru siyo uzuu hatuko Sauzi hapa,” Alitania Dk. Mbwamwitu huku akimpatia kipisi cha sigara kali Mgosi Machungi. Dk. Mipawa na Dk. Kapende hawana mbavu.
Nao inaonekana walikuwa wakimsengenya Mgosi anavyoua “L” na “R” kwa kusema Uhuu badara ya Uhuru.
“Jamani acheni utani. Siku ile mie niikuwa Tanu Youth ligi ambao tiliiongoza kumzomea mume wa malkia iliposhushwa bendea ya Union Jack ya Mwiingiiishi,”
Baada ya kuona hoja inaanza kuyeyushwa na utani na masimango, Profesa Dk Msomi Mkatatamaa anaamua kuokoa jahazi. Anakatua mic na kusema, “Tuache utani. Dk. Mpemba ana hoja tena nzito yenye maana na maanawia.” Anainua kombe lake na kunywa kidogo na kukatua kashata huku akifukuza moshi wa sigara kali na kuendelea, “Hiki kinachoitwa Uhuru kina maana tofauti kwa watu tofauti.
Kwa mfano, kwa wale wanaokula, kuiba, kufuja na kufanya madudu watakavyo bila kushughulikia huu ni Uhuru kweli. Ndiyo uhuru wanaoutaka. Kwa ndata wanaoweza kumiminia watu risasi na kuwamwangosi huu ni uhuru kweli,”
Kinokia chake kinaita hivyo anaamua kukizima ili kuendelea kumwaga pwenti. Anaendelea, “Samahani shemegi yenu naona alikuwa akinipeep. Wabongolalalanders kwa kubeep! We acha tu.”
Dk.Mchunguliaji anachomekea, “Tatizo si wabongo kupenda kudeep. Tatizo ni watawala wetu kuwa wafanya biashara wenye maslahi kwenye makampuni kupe ya simu yanayotoa huduma mbovu kwa bei mbaya,”
“Yakhe usinambie mie kuhusu haya mashirika jambazi. Yanaiba pesa yetu na hatuna pakwenda wenda Tecra wasema wao hawahusiki. sijue wataka twende wapi hawa wezi na wezi wao?”
Profesa anaona mambo yanazidi kuharibika. hangoji Dk Mpemba amalizie malalamiko yake. Anakwanyua mic na kumwaga pwenti, “Malalamiko yenu yanaweza kuelezea ni upande gani wa uhuru mpo. Wanaowaibia pesa kwa kuwapa huduma mbovu wana haja ya kusherehekea uhuru unaowapa haki ya kuwanyonyeni na kuwaibieni.” Anachukua simu yake mfukoni na kuizima baada ya mshirika wake wa Bedroom kumbeep tena. Kabla ya kuendelea Dk Mchunguliaji anashangaa tena na kusema, “Amekudeep tena?”
Dk. Mgosi Machungi naye kampata kibonde wake, anakwanyua mic na kusema, “Mchunguiaji siyo kudeep bai kubeep. Wewe unadhani kudeep ni kuzuri au unataka udeepiwe wewe?”
Profesa Msomi keshagundua kuwa asipoingilia kati mambo yataharibika maana utani wa wanywa kahawa anaujua sana. Anamua kuzima simu na kuendelea, “Tuangalie dhana nzima ya uhuru ambao kwetu ni udhuru.
Wakati tukidanganywa kuwa tunasherehekea uhuru si udhuru, wao bila aibu wala chembe wanatutangazia kuwa kesi ya Dowani imeishakula bilioni 40!
Hapa uhuru uko wapi iwapo juzi juzi walituaminisha kuwa wangewashughulikia majambazi wa njuluku za umma wakati nao wanawatumia hao hao kutumaliza?
Kabla ya kuendelea Dk. Mpemba anachomekea, “Yakhe wasema ukweli. Je wajua kuwa hata magazeti mengi ya dunia sasa yanajua Tanzia inao mabilionea tano mmojawapo akiwamo yule Kagoda na yule mwingine ambaye alilazimisha mwanae achaguliwe nbunge ili aendelee tetea biashara zao?
Je, wajua kuwa bendera yetu sasa yatumiwa na nchi magaidi kufanyia biashara zao? Je wajua kuwa kaya yetu sasa yachimba urani ili itengeze silaha za kutuua sisi wanyonge?”
“Umenena vyema Ami,” Anamuamrisha muuza kahawa amuwekee kahawa anywe hadi alewe maana katoa pwenti si kawaida. anasemea, “We Dk. Shem (huyu ndiye muuza kahawa wetu) mwekee kahawa anywe hadi alewe,” anasemea huku akitabasamu na Mpemba naye anatikisa kichwa kuonyesha amemwaga pwenti kiasi cha kupewa ujiko.
“We Shem, mmwagie kahawa Mpemba hadi azimie,” Anabwatuka Dk. Mbwa Mwitu. Mpemba hajivungi, “Mbwamwitu twaheshiana ati. Kama watakamwagiwa wewe si useme mie nlipe?
Basi mie nsema, Sheem, mmwagie Mbwamwitu tangawizi hadi azimie maana naona ataka sana hiyo huyo,”
Kijiwe hakina mbavu jinsi watu wanavyofungiana nyama hapa.
Profesa anaendelea, “Mheshimiwa Dk Mpemba amesema maneno makubwa. Amevinjari karibu mfumo wote wa maisha unaotuchezea. Amewavua nguo wanafiki na mawakala wao wanaotuibia wakijifanya wanatujengea maisha bora kwa wote wakati wote ni wote wao,”
Anakamata kashata na kupiga tama kahawa na kuendelea, “Hivi mke wa Mwangosi au Shabaan Mitutu wanaujua uhuru? Wanaouawa na kusingiziwa ni majambazi wanaujua uhuru? Watoto wanaonyima pesa ya kwenda kusoma chuo kikuu cha Manzese na vyuo vingine wanaujua uhuru? Wazee wa Jumuia mfu ya Afrika ya Mashirika wanaujua uhuru? Wasichana wa mashuleni wanaojazwa mimba na kuambiwa wana kiherehere wanaujua uhuru? Watoto wanaokalia mawe na kufundishwa na walimu wa UPE wanajua uhuru? Wagonjwa mahospitalini wanaotozwa pesa kumtazama daktari wanaujua uhuru? Ombaomba wasio na suti wanaujua uhuru? Wamachinga pale wanaujua uhuru au wenye maduka ambao wengi ni wageni tena wakimbizi wa kiuchumi? Hivi wale,”
Anakatishwa na vigeregere na makofi toka kwa wanywa kahawa. Akiwa anajiandaa kuendelea kumwaga pwenti ndata wanatokea upande wa Kurasini wakiwa na mibunduki yao. Kila mtu anaamua kujikata kabla hawaja mMatutu au kumMwangosi halafu wakasema sisi ni majambazi kama wao.
Acha niwahi nyumbani kusherehea udhuru toka kwa mshirika wa bedroom!
Chanzo: Tanzania Daima Desembe 12, 2012.

No comments: