The Chant of Savant

Wednesday 12 December 2012



TAARIFA za mauaji ya raia wema yanayosababisha na polisi ni nyingi mno. Bahati mbaya hata mauaji yanapotokea hakuna anayewajibishwa.
Kabla ya kuendelea na makala yangu, hebu tutoe takwimu chache tu za mwaka huu kuhusiana na mauaji yaliyotekelezwa na jeshi la polisi.
Januari 14, 2012, Mgoyo Mgoyo wa kijiji cha Wegero, kata ya Buswahili aliuawa na polisi.
Februari 4, 2012 mkazi wa kijiji cha Nyarwana, kata ya Kibasuka, tarafa ya Inchage Nyamongo, Daniel Masimbe aliuawa baada ya polisi kumpiga risasi kwenye koromeo.
Agosti 27, 2012 Jeshi hilo lilimuua Ally Zona kwa kumpiga risasi ya kichwa mkoani Morogoro likizuia maandamano ya CHADEMA.
Agosti 30, 2012 huko Chato mkoani Geita David Gilles Vyamana na Gilbert Ntabonwa, wakazi wa kijiji cha Kakeneno waliuawa na polisi wakiwa kwenye nyumba ya kulala wageni.
Septemba 20, 2012. Daudi Mwangosi aliauwa kwa kupiga risasi akiwa kazini kwenye kijiji cha Nyololo, Mufindi.
Novemba 12, 2012 polisi walimuua Rashid Juma (23) huko Bukombe, Geita kumpiga risasi.
Takwimu hizi si za mwaka wote. Hapa hujausisha takwimu zote za mwaka na zile ambapo wahanga wanaouawa na polisi wanaelezwa kuwa ni majambazi kuficha ushahidi.
Hakika ni vigumu kwa sasa kutofautisha jeshi la polisi na genge la wauaji. Kwa watanzania, kwa sasa, hakuna tofauti baina ya majambazi na polisi hasa wale wanaopenda kutumia silaha zilizotokana na kodi zetu kutumalizia mbali tena bila kosa.
Hebu tusaidiane. Askari anayekuja na bunduki yake akimsaka jambazi ambaye hana hata taarifa zake ni askari kweli ua mbabaishaji anayetafuta rushwa au hata kuiba?
Tukio la aibu na kusikitisha lililojiri hivi karibuni Kunduchi Machimboni jijini Dar es salaam ni ambapo mwandishi wa habari wa gazeti hili Shaban Matutu alipigwa risasi mojawapo ya viashiria kuwa hatuna jeshi la polisi kwa ajili ya kulinda usalama wetu.
Inashangaza watu wanaoitwa polisi tena waliokwenda CPP Moshi ‘kupikwa’ kufanya vitu sawa na majambazi. Ni aibu na pigo kwa taifa kuwa na jeshi kama hili likilipwa mishahara na marupurupu kwa pesa ya walipakodi linaowaua kama wadudu wa kawaida.
Kisa cha kupigwa Matutu ni tone katika mabalaa ambayo yameishasababishwa na polisi wetu ambao baadhi yao wamejigeuza genge la mauaji bila sababu ya msingi. Inatisha pale unapoambiwa eti polisi wameingia kwenye nyumba ya mtu bila kujitambulisha wala kumuonyesha search warrant, kumueleza lengo lao, haki zao na kuamini kuwa amewaamini kufanya kazi yao.
Ni balaa zaidi pale waharifu hawa, wanaoitwa polisi, wanapompiga risasi raia mwema wanayepaswa kumlinda kikatiba. utawala wa sheria ni kuwatendea wananchi kwa usawa kwa mujibu wa sheria bila kujali huyu ni ndugu, rafiki, adui au kivyele wangu.
Polisi ni watumishi umma na si wauaji wake. Ni ajabu hata rais bado anamkingia au kumvumilia Mkuu wa Jeshi lenye sifa mbaya ya uuaji wa raia wasio na hatia tena kwa kutumia pesa yao ya kodi.
Si uzushi wala uchochezi kusema kuwa kwa sasa IGP Said Mwema ataingia kwenye vitabu vya historia kama Mkuu wa Jeshi la Polisi aliyeongoza jeshi lililoua raia wema wengi bila kuchukua hatua.
Je rais ana nini na Mwema? Je nini kinamzuia rais kumfukuza kazi licha ya kumchukulia hatua? Hapa tatizo ni kujuana au rais anaridhika na utendaji wa jeshi la polisi chini ya Mwema?
Kuna haja ya kumbana rais atuonyeshe huu utawala wa sheria anaoimba majukwaani kila siku uko wapi na kama upo ni kwa ajili ya nani? Huwezi kutwambia utawala wa sheria wakati watu wanavunja sheria tena kwa kutenda makosa ambayo ni makubwa kama kumwaga damu na hawachukuliwi sheria ukasema kuna utawala wa sheria. Hii ni kejeli kwa utawala wa sheria.
Hebu jikumbushe kisa cha aibu na ajabu kilichotendwa na Mkuu wa Mkoa wa Kanda ya Kipolisi ya Kinondoni, Charles Kenyela aliyeita waandishi wa habari ili kulidanganya taifa.
Kenyela, kwa sababu ajuazo, alitoa taarifa juu ya kujeruhiwa kwa risasi kwa mwandishi Matutu ya uongo na uzushi akijua wazi kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
Alimkashifu Matutu kwa kumwita jambazi wakati siyo. Jeshi lake lilimuumiza yeye na mkewe na bado likawa na mshipa wa kumkashifu. Kenyela alikaririwa akisema eti mwandishi Matutu aliyejeruhiwa pamoja na mkewe, mama J, ni majambazi ambao walikuwa wakisakwa na polisi kwa tuhuma hewa ambazo hakuzitaja.
Ajabu ya maajabu ni kwamba mama J ni mjamzito na raia mwema sawa na mumewe. Inashangaza kuona mtu wa cheo kama cha Kenyela kufanya uharifu usiovumilika lakini bado Mwema akaendelea kumvumilia.
Kinachojidhihirisha kwenye uongo wa Kenyela ni kwamba ima alitaka kuwalinda askari wenzake huku akijua walichotenda ni kinyume cha sheria na kanuni au hakufanya utafiti.
Inawezekana alidanganywa na watu wa chini yake naye akaamua kujivua nguo hadharani.
Tunaandika kutaka Kenyela na Mwema wachukuliwe hatua za kisheria ili liwe somo kwa wengine.
Je hapa anayevunja amani ni nani?. Maana huwezi kuwa na amani bila haki na uwajibikaji. Polisi wameshindwa kuzuia ujambazi na jinai nyingine kama utoroshaji wa madini, wanyama na kufurika kwa wahamiaji haramu.
Badala yake wamekuwa mabingwa wa kuua raia wasio na hatia. Je hapa serikali inaweza kutueleza nini tukaielewa? Jeshi letu la polisi limekuwa kinara hata katika tafiti zinazohusu upokeaji wa rushwa na hakuna anayeguswa na hili? Je hapa kazi ya rais ni nini iwapo wananchi hawana usalama ilhali aliapa kuwalinda wao nchi na katiba yao kwa mamlaka waliyomkabidhi?
Chanzo: Tanzania Daima Desemba 12, 2012.

No comments: