The Chant of Savant

Wednesday 5 December 2012

Muungano wa EAC ni mkuki kwa taifa

INGAWA kuna baadhi ya wenzetu waliuona msimamo wa kiongozi wa nchi, dhidi ya kuwepo kwa sarafu moja ya Afrika Mashariki kama jambo la maana, lawama zinapaswa kupelekwa kwa Rais Jakaya Kikwete mwenyewe.
Wengi tulipinga hata huu ‘Muungano’ wa kuburuzana na kugeuzana majuha, lakini hakuna aliyesikiliza kilio wala ushauri wetu.
Kwa kumbukumbu, nimekuwa mpinzani nunusi wa Muungano wa Afrika Mashariki, sio kwa sababu napenda kuwa kisiwa bali kutokana na sababu zenye mashiko.
Kwa mfano, Rais Kikwete anapoanza kulalamika na kuonya kuhusu hatari ya kuwa na sarafu moja wakati haoni hatari ya kuunganisha nchi zenye ardhi kubwa na zisizo na ardhi kabisa, anamaanisha nini?
Je, kama rais, anakosa nini kuingilia kati kwa niaba ya nchi yake? Mbona kwenye kuburuzwa alitumia madaraka yake bila kuchelewa wala kulalamika?
Tulisema, na tunazidi kusema, kuwa Muungano wa Afrika Mashariki ni mkuki kwa Tanzania zaidi ya nchi nyingine.
Hebu angalia jinsi nchi karibu zote, ukiondoaTanzania, zilivyo na zigo la idadi kubwa ya watu ikilinganishwa na maneno yao.
Kenya ina idadi ya watu karibu sawa na Tanzania wakati ardhi yake ni chini ya nusu ya ukubwa wa taifa hili, Uganda kadhalika.
Ukitazama Burundi na Rwanda ndiyo unapata kichefuchefu. Fikiria nchi yenye ukubwa wa kilometa za mraba 26,338 na kuwa na watu takriban milioni tisa.
Nchi ambayo ni ndogo hata kuliko Mkoa wa Tabora, ina idadi ya watu kama hiyo halafu eti mnaungana.
Tabora ina ukubwa wa kilometa za mraba 76,151 - mara tatu ya Rwanda na Burundi. Mnaunganisha nini kama siyo umaskini?
Burundi yenye ukubwa wa kilometa za mraba 27,834 nayo ina watu takriban milioni nane.
Uganda ina ukubwa wa kilometa za mraba 93,065 na idadi ya watu takriban milioni 33, huku Kenya ikiwa na kilometa za mraba 224,080 na idadi ya watu milioni 44.
Jumlisha idadi hiyo ambapo ni watu wa nchi zote isipokuwa Tanzania, unapata milioni 80. Tanzania ina ukubwa wa eneo la kilometa za mraba 945,000 na idadi ya watu wapatao milioni 40.
Eneo la Tanzania bado ni kubwa kuliko ukiunganisha nchi zote zinazolilia kuungana nayo kwa mara zaidi ya mbili.
Ukiziunganisha nchi hizo zote, unakuta kuwa zina ardhi yenye ukubwa sawa na takriban moja ya tatu ya Tanzania.
Maana zina ukubwa wa jumla wa kilometa za mraba 371,217. Je, hapa bado kuna uhalisia au kudanganya? Kwanini akina Rais Kikwete na baadhi ya viongozi walishindwa mahesabu rahisi kama haya?
Tuliwahi kuhoji kwanini kama Muungano ni ‘big deal’ tusiungane na Msumbiji na Zambia badala ya nchi hizi nyemelezi zisizo na cha kutuchangia zaidi ya kutunyonya?
Ukija kwenye rasilimali unapata swali lile lile kuwa Tanzania aihitaji kutoa rasilimali zake kwa nchi maskini wakati kuna nchi zenye ufanano kama Kongo (DRC) na Msumbiji linapokuja suala la rasilimali.
Kwanini hatukujifunza toka kwenye muungano wa mashaka na matatizo na Zanzibar jamani? Hapa tunaongelea ukubwa na rasilimali.
Hatujaongelea historia na matatizo ya kijamii nchi husika zinayokabiliwa nayo. Hatujagusia mipango ya wazi na fichi ya nchi husika.
Turejee kwa Rais Kikwete. Je, ameona mwanga au ndiyo kutaka kujiondolea lawama wakati wananchi hawakushirikishwa katika Muungano huo?
Je, Tanzania ilijifunza nini kwenye kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977?
Kuna haja ya kumuuliza Rais Kikwete kwanini yeye na wenzake waliharakisha kuziingiza Burundi na Rwanda kwenye umoja huu bila hata kuwauliza wananchi?
Kumbukumbu zetu ni kwamba, wali-fast track na baadaye wakaja eti kuuliza maoni wakati kila kitu kilikuwa kimeishaamriwa.
Je, namna hii Tanzania haijengi mazingara ya migongano baina ya watu wake na wavamizi watakaozaliwa na Jumuiya?
Rais Kikwete alikaririwa hivi karibuni akisema: “Kwa uzoefu wangu itifaki ya sarafu moja inahitaji umakini kabla ya nchi wanachama kuafikiana.
“Kwa sababu hapo baadaye tutakuja na sera moja ya fedha ambayo itatoa mwanya mdogo kwa nchi mwanachama kukopa fedha nje ya jumuiya...sera hiyo itatoa ukomo wa kiasi cha fedha kinachotakiwa kukopwa na haitakubalika hata kama nchi mwanachama inashida ya kukopa zaidi kufanya hivyo.”
Rais Kikwete alisahau hayo wakati akiridhia kila jambo lililopendekezwa na nchi nyingine bila kuangalia maslahi ya taifa.
Hivi nchi kama Kenya inadai vivutio vyetu viko kwao wakati wakijua ni kinyume na sheria kufanya hivyo, watashindwa nini kukopa kwa kutumia Afrika Mashariki kwa manufaa ya nchi yao huku wakitutupia mzigo?
Nchi zinazotawala kibazazi zitashindwa nini kutumia bandari yetu kuingiza silaha zitakazoishia kuhujumu nchi nyingine?
Je, Rais Kikwete amekumbuka shuka asubuhi? Kama tunahitaji somo juu ya Muungano basi tujifunze toka Marekani, ambao walihofia taifa lao kupoteza kwa nchi maskini kama Mexico, wakaamua kujenga hata ukuta huku wakiacha mpaka wao na nchi tajiri Canada ukiwa wazi.
Lazima tuangalie maslahi yetu. Maana sio busara kuunganisha mbuzi na fisi ukasema umefanya jambo jema. Kama ni muungano basi tuungane na Msumbiji na Zambia na Kongo kabla ya hizi nchi ndogo ambazo hazina cha kuchangia zaidi ya kutunyonya.
Chanzo; Tanzania Daima Desemba 5, 2012.

No comments: