The Chant of Savant

Wednesday 21 November 2012

Rais JK, Mangula wana siri nzito


KWA wanaokumbuka, Makamu Mwenyekiti mpya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Philip Japhet Mangula, Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, watakubaliana nami kuwa aliondolewa kwenye nafasi ya ukatibu kwa aibu ya aina yake.
Pamoja na kukitumikia chama kwenye nafasi ya ukatibu chini ya uenyekiti wa Benjamin Mkapa na kusuka mpango wa kuiwezesha CCM kushinda, Mangula alitupwa nje na Rais Kikwete pindi aliposhika wadhifa huo.
Wachambuzi wengi wa mambo, wakati ule, waliona kama Rais Kikwete alikuwa ameonesha kigeugeu katika kupangua watendaji wa Mkapa na kuweka wake wakati akijua fika kuwa ni Mkapa na Mangula waliomsaidia kushinda na hata wakati mwingine kusaka fedha haramu kama za EPA kama ilivyowahi kudaiwa na mwanasheria aliyesimamia dili hili zima, Michael Bhyndika Sanze.
Mengi yalisemwa juu ya urais wa Kikwete kuanzia shutuma za wizi wa pesa ya umma kutoka kwenye Benki Kuu chini ya kashfa ya EPA ambayo Kikwete aliizima baada ya kukabidhiwa mikoba.
Yalisemwa pia ya Kikwete na kampeni zilizotumia pesa ya EPA kuwahonga wapiga kura baada ya kuwachafua wagombea walioonekana kuwa tishio, hasa Salim Ahmed Salim ambaye uzalendo wake ulitupwa kando na kuitwa Mwana Hizbu, hata Mwarabu wakati ni Mtanzania safi.
Kwa wanaojua mchezo mzima, kilichomponza Mangula hakijulikani wazi na bado kimeacha maswali kwanini Kikwete alimtema haraka, hivyo huku akimkingia kifua Mkapa?
Si Mkapa, Mangula wala Kikwete waliowahi kukanusha shutuma hizi nzito pamoja na Dk. Willibrod Slaa kuwataka wafanye hivyo mara nyingi.
Laiti Mangula angejua kuwa mambo yangebadilika haraka namna ile, angekata pua na kuunga wajihi wakati ule kabla ya kutimuliwa na kuadhirika kiasi cha kurejeshwa chamani kama zana nyingine yoyote.
Kwa wanaofahamu jeuri ya Mangula na alivyotupwa, wameshangaa jinsi alivyokubali kuramba matapishi yake sawa na Kikwete aliyemtupa nje baada ya kupata uenyekiti. Maana aliwahi kusema kuwa wastaafu wasikae Dar na kufungua NGOs, waende vijijini.
Je, nini siri ya Rais Kikwete na Mangula “kurudiana”? Je, Kikwete amegundua kosa lake au Mangula amepunguza hasira zake? Je, hii ni ndoa ya mashaka au mwisho wa uhasama?
Kwa wanaojua maisha ya watumishi, wanaoachia ngazi bila kuiba vya kutosha, bila shaka watakubaliana nami kuwa Mangula amelazimishwa na ukata kukubali kumtumikia Kikwete hasa wakati huu ambapo watu angalau waadilifu, au wenye madhambi yaliyofichika na wenye busara ni wachache ndani ya CCM.
Kwa upande wa Kikwete, naye kama Mangula amelazimishwa na ukata wa uadilifu kiasi cha kuramba matapishi yake. Je, ndoa hii itafana na kufanikisha kile walichodhamiria ambacho ni kuifufua CCM ili iweze kuwa ‘fit’ kuelekea uchaguzi 2015?
Kila mti utaujua kwa matunda yake. Maneno ya Mangula wakati wa kuwashukuru wajumbe kwa kumpitisha nadhani yanaweza kutufungulia kijidirisha cha kuchungulia kilichomo moyoni mwake. Alikariri, “Isifike mahali CCM ikatangaza tenda ya uongozi,” Je, hapa Mangula alikuwa akimpiga kijembe bosi wake ambaye ilidaiwa aliingia madarakani kwa pesa, tena pesa yenyewe chafu au maswahiba wa Kikwete wanaoutafuta urais kwa pesa chafu itokanayo na usaliti na wizi kwa taifa?
Je, Mangula alilenga kupeleka ujumbe gani? Je, Mangula alikuwa akitubia dhambi ya kuiba pesa na kuitumia kama hongo aliyoishiriki wakati wa kuitafutia CCM ushindi wa urais wa Kikwete? Je, alikuwa akiwakumbusha wale wanaotaka urais kuwa kipindi hiki hatashiriki mchezo mchafu kama huu?
Je, Mangula amekubali nafasi husika kwa masharti ambayo ni siri ya wawili kiasi cha kuwa na jeuri ya kutamka maneno yanayoonekana wazi kumgusa bosi wake ambaye ni hasimu wake wa zamani kimsimamo? Hakika ndoa hii ya wawili inaacha maswali mengi kuliko majibu.
Je, Mangula ambaye aliondoka kwenye ukuu kwa aibu ana jipya gani la kuleta katika CCM? Mangula baada ya kutemwa na Kikwete alijaribu kugombea uenyekiti wa Mkoa wa Iringa akabwagwa na Deo Sanga mwaka 2007.
Baada ya hapo alijaribu kugombea ujumbe wa NEC jina lake halikurudishwa. Kwa wafuatiliaji wa mambo kitendo cha Mangula kujishusha hadi kugombea cheo kidogo kama kile kilionekana kama mtego kwa CCM, ingawa wakati ule si Kikwete wala CCM waliojali.
Je, ni kitu gani ameifanyia CCM hadi kumkumbuka? Je, ametubu dhambi zake au waliomtema wamejikuta wamebanwa kiasi cha kukuta kuwa Mangula ndio muarobaini? Hata hivyo Mangula ambaye ameonesha kushindwa tena kwenye nafasi ndogo anaweza kuleta jipya gani zaidi ya kutafuta riziki? Je, atakubali kuacha msimamo wake na kile anachoamini ili kuishi?
Wahenga walisema: mtumikie kafiri upate mradi wako. Je, haya yanajidhihirisha kwa Mangula? Kwa wanaojua tabia ya Kikwete, wanatia shaka kama ndoa hii itadumu hasa ikizingatiwa alivyomtema Yusuf Makamba baada ya kugeuka mzigo na kumteua Wilson Mukama ambaye aliishia kuwa mzigo hata zaidi ya Makamba.
Chanzo: Tanzania Daima Novemba 21, 2012.

1 comment:

Anonymous said...

Yaani huna cha ku comment
na mwenye blog hebu tuondole huo upuzi hapo wa matusi