The Chant of Savant

Wednesday 3 October 2012

Uchaguzi NEC ya CCM ufisadi mtupu

WENZENU juzi tulikuwa na uchaguzi wa kugombea ulaji mbalimbali Kijiweni kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa. Katika uchaguzi wetu, kulikuwa na mnyukano wa kufa mtu.
Vijana wengi ambao hatukuwa tukiwajua, walijitokeza na kutaka kuwanyang’anya ulaji wazee wazima. Pamoja na jeuri ya vijana, ulaji wa mwenyekiti, mke wake na maswahiba wake ulilindwa kwa gharama zozote hadi kufikia kubadili sera ya kijiwe toka upayukaji kwenda ufisadi.
Ngoma kubwa ilianza kunoga pale wakongwe kama Dk. Mbwa Mwitu aka Eddie Ewassa na Mchunguliaji aka Endelea Chenga kutakiwa watemwe kama tulivyomfanyia Ewassa kwenye kashfa ya mkaa tuliyoibatiza Richomond tuliyoasisi lakini tukamtoa kafara Ewassa Mbwa Mwitu ili kuokoa ulaji wangu na wake.
Baada ya kumtosa niliamua kuendelea kumlipa marupurupu kama mzee na kiongozi wa Kijiwe aliyestaafu.
Kitu kimoja ambacho unayesoma hapa lazima ufahamu na kuzingatia ni kwamba wakati tukipitisha ufisadi kama sera mpya ya Kijiwe, tunawaambia wanakijiwe kuwa bado tutawakomboa na kuwapa maisha bora wote tukihakikisha wanakula kashata na kunywa kahawa bila kikwazo na kwa afya yao.
Ukiachia mbali tishio la vijana, kulikuwa na tishio la wake za watu wasio na majina wala vyeo kutaka kuchukua ulaji wa wake na washikaji zetu. Ngoma ilikuwa nzito hadi tukaanzisha mkakati wa kuondoa majina kimya kimya bila kujali lawama.
Hivyo, hata umoja wa wake zetu nao ulikumbwa na misukosuko si kawaida. Nakumbuka nyumba ndogo yangu yaani Bi Sofi Lion alitishiwa na mke wa kigogo mwenzangu aitwaye Joni Malikula. Kama siyo busara kutumika, si ajabu angekufa mtu. Kwa vile tunajua Kijiwe kina wanawake wengi na tusingependa watumie wingi wao kuchagua mwenyekiti mwanamke, tuliingilia haraka na kuzuia akina mama kutustukia kuwa tumekuwa tukiwatumia kwa kuwapa nafasi uchwara za udohoudoho.
Hata Umoja wa Vijana ambao tumeuweka mikononi mwa vitegemezi vyetu tunauangalia kwa makini sana hasa tukijua kuwa vijana na akina mama ni wengi kuliko sisi vizee. Hivyo, wakijitambua na kujua janja yetu, wanaweza kutunyang’anya ulaji wetu kirahisi. Wanaweza kufanya mapinduzi ndani ya mapinduzi tukaishia kunyang’anywa maulaji yetu.
Pamoja na kufanikiwa kurejesha ulaji wetu, wale wahuni wote waliotaka kutukosoakosoa kama Deo Filikumjomba, Nimlord Mkononi na wengine tuliwatupilia mbali.
Hawa jamaa walituudhi sana walipotaka eti waziri mkubwa wa Kijiwe ajiuzulu baada ya kuongopa na kufanya madudu. Kwa kuwashughulikia kama tulivyofanya, wengi wenye mawazo mgando kama hayo watakoma kama siyo kukomaa.
Kosa jingine walilotenda hawa jamaa ni kutaka eti wazee wa Kijiwe walioghushi nao watupwe nje wakati ni washirika wetu. Akina Mare Nyagu, Emmy Nchimvi na Willy Lukuvu walinusurika kutokana na sera mpya ya kulindana na kulinda ufisadi.
Wakati tukiendelea kupongezana kwa kuminyana na kuokoana, wapinzani wetu waliandika ujumbe ufuatao kwenye mtandao wao ambao anwani yake ni siri.
Waliandika: “Kama wapinzani wetu wataamua kufanyia kazi hii sera mpya ya Kijiwe ya ufisadi vilivyo, hawana haja ya kutafuta la kuwaambia walevi wakaelewa. Upinzani uende vijijini na kutoa tafsiri ya hiki kinachoendelea ndani ya Kijiwe. Uwaeleze walevi hasa wanywa kahawa kuwa kile Kijiwe walichoanzisha na Ticha Mchonga kikaleta nafuu kilikufa zamani.
“Wawaeleze ukweli kuwa kile Kijiwe hakikufa kifo cha kawaida bali kiliuawa na nafasi yake kuporwa na wenye maulaji na dili, tena zipatikanazo na kila aina ya jinai na ujambazi kama vile HEPA, Richomond na mazabe mengine.
“Kwa wenye kupenda ukombozi wa Kijiwe chetu, wanapaswa kushangilia na kukiombea kiendelee kufanya makosa kinayorudia kila mara ili kidhoofike na kuondoshwa kama KANU kule Kenya.”
Waliendelea: “Ingawa baadhi ya vigogo waliokuwa wapeleke pigo la mwisho kwa Kijiwe waliomo ndani wamekuwa wanafiki, woga na wababaishaji, njia iliyochukuliwa na Kijiwe kwa sasa ina uhakika wa kuimaliza.
“Hata Usalama wa Kijiwe wafanyeje kulinda huu uchafu wa mchana, mwisho wa Kijiwe kama siyo mwanzo wa mwisho umeishawadia. Ni vizuri kuwa sasa Kijiwe hakina kiongozi hata mmoja mwenye visheni.”
Walinishambulia mimi na kusema: “Ukimwangalia mwenyekiti wake, kila mtu anajua anavyopwaya. Makamu wake naye, hana udhu tena baada ya kashfa za Ngorongororo na kujaza watoto wake kwenye balozi za Kijiwe nje zimemmaliza kabisa. Zaidi ya hawa amebakia nani?”
Baada ya kusoma utumbo wao tuliamua kwanza tunyamaze na kumaliza sherehe za kupongezana ili hapo baadaye tuje tuwashughulikie hata kwa kuwanyotoa roho. Tutaazima vijana wa jamaa yetu Mwemamwema wawamwangosi ili wakome kufuatilia ulaji wetu. Hatuwezi kuacha amani ya Kijiwe ivurugwe na watu wanaotaka kutunyang’anya ulaji wakati ulaji wetu tumepewa na Mungu na walevi wenyewe.
Hata kama walevi wanaliwa, wao inawahusu nini? Tulishasema kama wanataka ulaji waende baharini wakavumbue vijiwe vingine kwenye visiwa ambavyo havijakaliwa na mtu wakatawale na kula kule. Hawa hawana adabu na wana tamaa kama jamaa zetu wa Uangusho wanaodai eti wanataka watawaliwe kisharia wasijue kaya ina wenyewe na wenyewe ni sisi tusio na dini wala nini.
Nasema tena. Haamshwi wala kuangushwa mtu. Nenda Arabuni muone watakavyowanyotoa roho watumwa nyie msio na macho wala akili.
Kwa ufupi tulichofanya ni kile wazungu huita ‘ballyhoos done by yahoos and yo-yos.’ Hatukuwa na jinsi bali kuendelea kutowaamsha waliolala, yaani vijana na akina mama.
Baada ya kuhakikisha kuwa wanamalizana wenyewe kwa wenyewe wakigombea ulaji wa hovyo wa kupewa kwa kutumia jinsia na umri, sasa maulaji yetu ni salama u salimini. Tunaendelea kupeta na kutesa bila noma kama hatuna akili nzuri.
Hatufichi ujanja wetu. Tunasema tena kwa kinywa kipana - walevi wajijue na wataendelea kuliwa na kuliwaga hadi wakome ubishi. Sisi ni kijiwe chenye maarifa na sanaa kila aina vya kuwalewesha na kuwala walevi mchana kweupe.
Naona niishie hapa niwahi home kumpa talaka mshirika wa bedroom kutokana na kunitia hasira kama Wahasira kutokana na vijana wetu kujiunga na CHAKUDEMA. Nitaua mtu leo!
Chanzo:Tanzania Daima Oktoba 3, 2012.

2 comments:

Anonymous said...

Stori refu hata unasahau mwanzo ulianza vipi ujinga mtupu

Jaribu said...

Yeah! Ukiwa na short attention span hii stori inahitaji siku nzima kuielewa. Unahitaji tuition?