The Chant of Savant

Wednesday 1 August 2012

Mwagawana ardhi wanyonge tujenge mbinguni?


MWAKA jana wakati nikisherehekea kutimiza miaka 14 ya ndoa yetu na mama Kidume Al maarufu Nesaa Msemakweli wa Mpayukaji, niliwaahidi kuwa kuna siku nitashuka na mistari na kuwa supastaa wa kweli na siyo hawa uchwara wa rapu niwaonao kwenye mitaa ya kwetu maeneo ya Ilala Shingofeni. Kabla ya kufanya hivyo, acha niwamegee mistari kidogo.

Dzuwa li lapita mdima usaka
Iwe mwana wanga chonde tabwerela
Ona mulungu wako alikuyita’ nawe
Iwe mwana wanga tabwerela
Iwe mlevi wanga mdima usaka
Ona ardhi yako wezi wanagawana
Iwe mlevi wanga chonde tabwerelaaa
Mmegawana ardhi yetu
Mmegawana ofisi zenu
Tena wengine kwa kuhongana
TANESCO mmegawana
Bandari mmegawana
Benki kuu mmegawana
Uhamiaji mmegawana
Kila palipo na mshiko mmegawana
Mwe!
Hamtosheki!
Mmegawana hata makaburi ya wazee wetu
Wezi wakubwa mnagawana mali walevi, umaskini
Hamjasikia mikwanja na promosheni za uongo na ukweli
Kuwewaka kizani walevi wetu?
Wajinga ndiyo waliwao.
Mmegawana hata madhambi
Hata biashara ya mihadarati na ujambazi
Mmegawana tu!
Hata mazimwi kama Richmond
Dowans, IPTL na mabalaa mengine mmegawana!
Kila mheshimiwa ana fisadi wake awe mwekezaji au mchukuaji
Kila rais ana mfadhili wake
Kila mtoto au mke wa rais ana mfadhili wake
Wana hata miradi yao iitwayo NGO
Je walevi tule wapi?
Hivi kweli nyie mna kesho?
Kama ipo si salama jamani
Akili tieni kabla ya kuingia msambweni
Mnapeana ulaji kwenye kila kijiwe chetu
Wilayani mikoani hadi taifa ni nyinyi tu
Mmetugawanya katika dini
Hata kwenye chama mmetugawanya kwenye mitandao
Mitandao ya kujikomba
Mitandao ya kuiba na kukomba
Mitandao ya sanaa
Mitandao ya magamba na magwanda
Hata walevi mmetugawa
Hawa wanakunywa waini
Sisi tunakunywa gongo
Hawa wanakunywa madaraka
Sisi tunakunywa utumwa!
Kila kitu mmegawana
Sasa baki mgawane roho na miili yetu
Mie kuna siku nitakojolea kaburi la mtu hivi hivi kupinga huu ufisi na ufisadi tunaofanyiwa eti kwa vile sisi ni walevi.
Siku zote nimekuwa nikihanikiza na kusema kuwa nchi hii imebakwa tena mchana ila watu huwa hawanielewi zaidi ya kuniona chizi wakati machizi wao. Watu wanatumia matumbo kufikiri badala ya vichwa hadi wengine kutumia masaburi unategemea nini?
Mijitu inakwenda mjengoni kupiga usingizi na umbea huku ikilipwa mabilioni kwa upuuzi huu na hakuna anayestuka! Juzi mheshimiwa sana Bwana Yosefu 30 alinakiriwa akisema, “Mheshimiwa mwenyekiti baadhi ya makampuni ya mafuta yalikuwa hapa Mjengoni na kutoa chochote kwa waheshimiwa na hili si kwa upande wa serikali ya Chama Cha Mafisadi bali wabunge wa pande zote tukiwemo wapingaji. Msione watu wanazungumza kwa nguvu hapa kutetea, hawa wamepewa chochote,” Je, hawa kweli wanawakilisha walevi au uroho na ufisi wao? Je, majimbo yao si matumbo yao?
Ajabu hawa na wakubwa wao ndiyo wanaogawiana ardhi na kila kitu wasijali sisi na vitegemezi vyetu tutaishi wapi! Mlaaniwe na kulegea. Mungu awalaani ulaji wenu uwatokee puani kama siyo kuwatoboa hiyo mitumbo yenu isiyoshiba.
Tangu aondoke mzee Mchonga urahisi umekuwa sawa na ujambazi tena wa ukoo. Kila jambazi linalokuja linakuja na genge lake kutuibia walevi. Tangu nabii Musa bin Mchonga mwenyewe alaani ikuu akisema kunanuka rushwa, rushwa imesambaa hadi bedroom. Anayebishia hili ajiulize huu uheshimiwa wa dezo (Msomi Mkatatamaa hupenda kuuita wa chupi astaghafillullahi Mwenyezi Mungu nisitiri Ramadhani hii) umetokea wapi kama siyo huko?
Watu mnahongana hata uheshimwa kwa kuangalia chupi zenu sorry underwear? Hivi hawa waheshimiwa wa underwear wanaweza kuwa na mawazo gani ya maana zaidi ya kufikiri chini chini? Ukienda kwa mama Microphone binti Speaker ndiyo usiseme. Ndo hana, hata uwezo wa kuendesha vikao vya kijwe hana. Amepataje?
Sasa ngoja nitoe ushahidi wa kesi yangu ya kugawana kila kitu. Kumbuka mimi ni mwanasharia aliyebobea. Leo nitatoa mfano wa ardhi tu. Haya mengine siku nyingine. Nani hajui kuwa hivi karibuni tulifichua kijiweni na magazeti yakaandika kuhusu kugawana ardhi kwa vigogo na mibuyu?
Kwa taarifa yenu hizi habari mlizosoma magazetini kuwa wezi wakubwa wamegawana ardhi kule wilayani Temekeee zilitoka kijiweni kwetu. Ila sitawambia nani tulimwambia na siku hiyo tulikuwa kijiwe gani.
Ukweli ni kwamba sisi wanywa kahawa ndiyo tulifichua uchafu huu. Waulize kina Martin na Abasalom wanajua fika kuwa sisi ndiyo tuliwachoma hawa wezi wenye kujiita wakubwa na waheshimiwa wakati ni wezi wakubwa wasio na heshima yoyote.
Orodha tuliyotoa ilikuwa na majina ya akina Willy Mukama, Jobiso Ndugai, Maukame Kinyaa Mbarapi, Pereira Ami Shilima, Florence Turukeruke, kaka Rama Kijasti, Ommy Chambo na Iddiliisha Rashid.
Wengine ni Diddie ‘Buttocks’ Masaburi, Jerryfish Silaha, Paulo Chagonjwa na mtaalamu wa kuzusha Seleman Kovu.
wengine ni Haruna Masebusebu, Ludovick Uto, Marina Njeka, Augustine Lyato’ Mlemavu, rasta Dio Filikumjomba, Sylvester Kokakola, Idd Azzana, Cyril Chama, Mohamed Visanga na David Kafulia.
Wengine ni Petero Kafumua, Sele Zedi, We Maulida Koma!, Suzy Limao, Meli Mwanjeka na Zakhia Mengjii.
Nisiwachose na orodha ya vibaka. Ila niruhusu nimalizie na majina maalumu ambayo yanatoka kwenye familia za wenyewe wala nchi na wenye nchi.
Ukiangalia orodha hiyo hapo juu unagundua kuwa sisi hatuna kaya zaidi ya kaya ya majambazi na mafisi yanayojihudumia bila hata kuangalia yaliyowatokea mafisi wengine kama kaka Mwamali Kashafi, Sir Doom Hosseini na wengine. Hata hivyo tusiwalaumu mafisi ni mafisi hufikiri kwa matumbo na masaburi kama haya yetu.
Hivi yule si Uhasama wa Taifa? Walivyonuna, acha niishie wasije wakaniulimboka.
Chanzo: Tanzania Daima Julai 1, 2012

No comments: