The Chant of Savant

Wednesday 8 August 2012

Makinda anataka kumdanganya nani?





TAARIFA kuwa Bunge limeunda kamati ya kuchunguza wabunge wake wanaotuhumiwa kwa rushwa iliyofichuliwa na wabunge wenzao, zilionekana kuwa habari njema.
Lakini, baada ya kuangalia jinsi mizengwe inavyoanza kuchukua nafasi yake na aina ya watu wanaounda kamati hiyo, waweza kusema hiki ni kiini macho kutokana na sababu zifuatazo:
Kwanza, wengi wa wajumbe wa kamati hii licha ya kutoka chama kimoja na watuhumiwa, hawana udhu wala historia ya kuridhisha kufanya kazi hii.
Pili, tuhuma zinazowakabili wahusika ni za jinai. Hivyo, jambo bora lililostahiki kufanyika si kuwachunguza, bali kuwafikisha mbele ya vyombo husika vya sheria.
Kama hili haliwezekani au linaonekana kuwa hatari kwa waheshimiwa kuogopa kuumbuliwa mbele ya mahakama, kwanini mahakama isifanye hivyo kwa njia ya usiri?
Kinachofanyika ni ubaguzi wa wazi wazi wakati wa kushughulika na watu wanaotuhumiwa kwa makosa ya jinai.
Kanuni ya adhabu iko wazi kuwa kila mtu anayetenda kosa la jinai, lazima afikishwe mahakamani na si kwenye kamati.
Kama watawala wetu wameamua kuvunja sheria na kubagua wananchi ili kuwalinda wenzao, kwanini isiundwe tume inayohusisha watu wenye udhu kama vile majaji au Watanzania wanaoaminika na kujulikana kwa udhu na uzalendo wao badala ya hii danganya toto?
Hakuna haja ya kufikiria juu ya heshima ya wabunge ingawa wakishajihusisha na rushwa heshima yao inapotea.
Kama siyo Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) kutekwa na ofisi ya rais hadi ikapoteza maana kwa kuwa chombo cha kulinda na kusafisha mafisadi, ingeweza kufanya kazi ya kuwachunguza hata kuwashitaki watuhumiwa kama wangepatikana na mashtaka.
Lakini, kwa vile TAKUKURU haina heshima wala udhu tena, ingeundwa tume yenye kuwa huru na kuwachunguza hawa watuhumiwa.
Hebu fikiria. Watu wanatuhumiwa kwa rushwa na wanaendelea kukaa bungeni wakati walipaswa kuwajibishwa kungoja taarifa za uchunguzi. Hii pekee inatosha kuonesha kuwa haki haitatendeka.
Wabunge wanapotuhumiwa kula rushwa, kwa maana nyingine ni kwamba Bunge limetuhumiwa chini ya dhana ya uwajibikaji wa pamoja.
Hivyo, kuruhusu Bunge kuchunguza wabunge wake wanaotuhumiwa kula rushwa, ni sawa na kulifanya kuwa mtuhumiwa, mwendesha mashitaka, polisi mkamataji na hakimu katika kesi inayolikabili.
Hapa, haki haitatendeka zaidi ya kuvuruga mfumo mzima wa utawala wa sheria kama upo. Bunge linachukuliwa kama mtuhumiwa si kwa maana kuwa wabunge wote ni wala rushwa. Hasha. Linatuhumiwa kutokana na ubovu wa mfumo na muundo wake. Kama Watanzania na serikali pamoja na taasisi nyingine kama Bunge wanachukia rushwa, basi waache sheria ichukue mkondo wake katika kushughulikia wabunge wanaotuhumiwa kula rushwa.
Bila kufanya hivyo, umma utaona ni kama sanaa na viini macho kama kawaida. Itajenga picha kuwa wanaojidai wanapambana na rushwa ndio wala rushwa wenyewe.
Ni pigo kwa haki hasa pale watunga sheria wanapokuwa wala rushwa wenyewe. Hawa hawawezi kutunga sheria za kupambana na rushwa wala ufisadi kwa vile wananufaika na jinai hizi.
Inakuwaje watendaji wengine wakituhumiwa wanakamatwa na kuwekwa ndani huku wakipelekwa mahakamani moja kwa moja, lakini si kwa wabunge wanaopaswa kuwa mfano?
Je, wabunge wa namna hii wanaweza kutunga sheria za kupambana na kile wanachonufaika nacho?
Je, wabunge wa namna hii wakishirikiana na serikali inayotuhumiwa kupatikana kwa njia ya kuiba pesa ya umma na kutoa rushwa wanaweza kuivusha nchi yetu?
Rejea madai ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willbrod Slaa, kuwa Rais Jakaya Kikwete aliingia madarakani kwa kutumia pesa ya wizi toka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu. Bahati mbaya, pamoja na kuchagizwa akanushe hata kutoa maelezo kuhusiana na tuhuma hizi, Kikwete siku zote amegwaya kufanya hivyo kwa kuchelea anaweza kuumbuliwa zaidi.
Tatu, kinachofanyika licha ya kuwa kiini macho na juhudi za kulindana, ni sawa na kupeleka kesi ya wizi wa mahindi inayomkabili ngedere kwa ngedere mwenzie au nyani. Hukumu yake inajulikana kuwa ngedere watashinda tu. Kwa vile mchezo wa mahakimu wao ni ule ule.
Kama upogo huu hautarekebishwa, kuna uwezekano wa wabunge wasiokula rushwa nao kuanza rushwa. Maana wanajua wakifichuliwa kesi yao itahukumiwa na wenzao tena wenye kukubuhu kwenye jinai hii.
Nne, wengi wa wajumbe ni wakereketwa na makada wa chama tawala ambacho kinajulikana kwa tabia yake ya kulindana.
Rejea maneno ya Mbunge Anne Kilango aliyekaririwa akisema kuwa wabunge wanapaswa kulinda maslahi ya chama badala ya maslahi ya nchi.
Alikaririwa akisema: “Tulimtosa Lowassa, baadaye ukweli umejulikana, na sasa makosa yetu yanaigharimu serikali na CCM. Tusirudie makosa yale yale, tuwaache hawa kwa maslahi ya CCM.”
Maneno haya ya kifisadi ya Kilango yanaonesha CCM ilivyodhamiria kulinda maslahi yake hata kwa kuhujumu taifa.
Hii ikichangiwa na baadhi ya wanakamati kupata ubunge wao baada ya kushindwa, lazima watalipa fadhila kwa chama kilichowawezesha.
Nani mara hii kasahau jinsi mjumbe mmojawapo, Gosbert Blandes alivyotuhumiwa kupewa ushindi wa ubunge mezani kutokana na mchezo mchafu wa kuchakachua matokeo?
Blandes pia alituhumiwa kutoa hongo kwenye uchaguzi ukiachia mbali kutokuwa na udhu wa kutosha zaidi ya kupaswa kuchunguzwa yeye mwenyewe. Wajumbe kama Brigedia mstaafu Hassan Ngwilizi hawawezi kutenda haki ikizingatiwa kuwa ni wakereketwa wa CCM.
Wajumbe kama John Chiligati wanajulikana walivyo na mamlaka chamani ukiachia mbali mjumbe kama Riziki Omar Juma kutoka kwenye chama chenye ushirikiano na CCM.
Tumalizie kwa kuwasihi Watanzania wakatae huu usanii na ushirika katika ufisadi unaofanywa na taasisi zinazojiita zao wakati si zao, bali za kikundi kidogo cha watu kilichojihalalishia ulaji kwa gharama zao. Kundi lililowageuza wanachi punda wa kubeba mizigo yake.
Swali kuu la kujiuliza hapa ni je, Spika wa Bunge, Anna Makinda, Bunge na wabunge wanataka kumdanganya nani kuwa wanaweza kutuhumiwa, wakajichunguza au kuchunguzana na kuhukumiani kwa haki?
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 8, 2012.

No comments: