The Chant of Savant

Wednesday 16 May 2012

Tufute vyeo vya wakuu wa wilaya na mikoa

AADA ya kuwepo malalamiko mengi sana kutoka kwa wanakijiwe kuwa mwenyekiti nawafuga wanyonyaji marafiki na washikaji zangu kwa kuwazawadia ukuu wa kijiwe wa mkoa na wilaya, tumeamua kukata mzizi wa fitina.
Tumefutilia mbali vyeo na ulaji wa wakuu wa kijiwe wa wilaya na mikoa ambao kweli walikuwa wanyonyaji niliowalipa fadhila kwa kuhakikisha kila uchaguzi wa kijiwe napeta.
Nilijua hili ingawa sikutaka kujionyesha kutokana na kuwa fursa nzuri ya kuwahifadhi washikaji na washirika zangu.
Hivyo, taarifa rasmi tunayotoa ni kwamba kuanzia sasa hapatakuwa na vyeo vya mkuu wa wilaya na mkoa wa kijiwe.
Kila kijiwe kwenye ngazi ya wilaya na mkoa kitaendesha mambo yake kijuavyo na kitakavyo mradi kisifanye ufisadi hadi CAGI aje kuwaumbua kama ilivyotokea kwa jamaa fulani hadi wakatimuana huku wengine wakilia kama vichanga kwa kuukosa ulaji.
Meku Sirilo Chaaami upo hapo? Maana huu ulikuwa wizi uliokuwa umehalalishwa. Hivyo walevi wote mikoani na wilayani watakuwa wakijifanyia mambo yao bila kulisha wanyonyaji fulani waliokuwa na connection na mwenyekiti yaani mimi Dk. Mzee mzima Mpayukaji Msemahovyo wa Nkwazi wa Mhango wa Waambie Walioko juu ili wa chini wasikie.
Hivyo, tuelewane na kukubaliana. Kwa maana nyingine ni kwamba walevi wametangaza ukombozi na kukata mikatale ya kunyonywa na kikundi cha watu. Nashukuru sana kunusurika. Maana walevi walikuwa wamepania kuning’oa kwenye ulaji kama nisingewatoa sadaka washikaji zangu husika.
Nilichukia nusu ya kunyotoa mtu roho lakini ningefanyaje iwapo wenye mali walikuwa wameamua baada ya kushtukia uteuzi wangu? Hata hivyo haikuwa kazi rahisi. Maana zali lilipoanza niliamua kujirusha kwa kufanya ziara nchini Brazil kwenda kuona walevi wa kule wanavyokunywa kahawa. Nilishawapa taarifa ya matanuzi yangu na shosti wangu huko kwenye nchi ya soka na samba.
Walevi waligundua kuwa wengi wa wateule wangu walikuwa ama marafiki zangu wa mke wangu au watoto wangu ambao kusema ukweli walikuwa wakinitumia kuwasukia ulaji washikaji na washirika wao.
Pia waligundua kuwa kumbe sisi ndiyo tulikuwa chanzo cha umaskini na mateso yao! Kituko ni kwamba wengi hawakuwa na sifa za kuwa wakuu wa vijiwe ingawa niliwapa ulaji kwa vigezo ambavyo nilivijua mwenyewe bi mkubwa na vitegemezi vyangu.
Pia nilikuwa nikitumia fursa hii kuwapa ulaji walamba viatu wangu hasa makanjanja walevi waliokuwa wakijipendekeza na kufanya kazi zangu chafu ukiachilia mbali nyumba zangu ndogo.
Pia watoto wa wakubwa zangu kama vile Mgosi Machungi, Mipawa, mzee Maneno na Kidevu nao niliwapa ulaji ili waendelee kuneemeka wao na familia na koo zao kwa mgongo wa walevi.
Juzi nilimtangazia bi mkubwa kuwa mashoga zake na ndugu zake niliokuwa nimewajaza kwenye ulaji wa wilaya na mikoa wanapaswa walie tu kwa vile wenye mali wameshtuka sina jinsi ya kuwabeba. Hivyo chini ya mfumo mpya wa Uhujumaa na Kujimegea hawa wamepigwa panga.
Wakitaka kusavaivu basi wakauze bwimbwi au kusafirisha kahawa nje ya kijiwe.
Kweli cha mlevi huliwa na mgema wahenga walisema. Ila walevi wakishtuka humkopa mgema hata kunywa wakakataa kulipa ukiachia mbali kumshtaki kwa ndata iwapo mgema mwenyewe ni mgema gongo.
Mwanzoni wakati mimi na washikaji zangu tukifanya huu usanii hatukujua kuwa walevi wangeshtuka. Hakuna mtu alilia kama rafiki yangu Muongo Rweye aliyepoteza ulaji kwenye kijiwe cha wilaya na Ugosini.
Jamaa pamoja na kujidhalilisha kwa ajili yangu kwa miaka, jamaa wameamua kummwaga manonihino baada ya mimi kumkumbuka mtwana wangu mtiifu zaidi hata ya mbwa.
Hakuna kitu kilinikera kama matamshi ya Msomimkatatamaa aliyedai kuwa washikaji zangu waliokuwa wakinisaidia kuongoza vijiwe wilayani na mikoani ni sawa na kupe. Eti alisema eti walevi ni ng’ombe na wateule wangu walikuwa kupe wanaonyonya damu ya hawa ng’ombe tena waliokondeana!
Wakati wakubwa wenzangu wa kaya wameamua kupanua genge la walaji wao, mie nimevunja langu baada ya wanakijiwe kunijia juu. Nadhani hili litakuwa somo kwa walevi kuwashughulikia wakubwa zao na kuwazuia kuendelea kuwatumia kama punda au the beast of burden kama ilivyo sasa.
Nisionekane nafanya uchochezi, acha niwaachie wahusika wajipime na kuamua wenyewe. Maana waliogeuzwa hayawani na mataahira ni wao na si mimi. Deontologically even teleontologically, they need to do something. They should forget political tradeoffs. Lol! Nimejisahau na kumwaga ung’eng’e! Nisameheni ni hasira tu zinazonichochea kumwaga ung’eng’e huu.
Naona mzee Kidevu alishaanza kuinua kibendera kwa kuona nazidi kupuyanga na utasha asijue ni mihasira ya kukosa pa kuwaficha na kuwahifadhi washirika zetu. Hata hivyo, sikuzidiwa kete zote. Maana bado niliweza kuwateua watoto wa marafiki zangu kushika nafasi nyingine nyeti kijiweni.
Hamjamuona mtoto wa swahiba yangu Mgosi Machungi wa Makambale akitesa kama hana akili nzuri? Hamumuoni daktari Hoseini anavyotesa kama hana akili nzuri? Sisi wasanii ni wajanja siku zote inapokuwa kwenye kuonyesha mazingaombwe yetu wakati tunapopambana na ombwe la ulaji.
Muhula huu nina kazi kweli kweli. Nina kibarua cha kuandika Katiba mpya ya kijiwe. Kazi inayonikabili ni kuhakikisha inaandikwa Katiba ambayo itatulinda mimi, shosti zangu na vitegemezi vyetu kutokana na mazabe tunayoendelea kuyafanya.
Bila kufanya hivyo kuna siku walevi wanaweza kunigadafi kama siyo kunimbaraaka kama jamaa zangu wa kule Maghreb. Ingawa nimelazimika kuwateua kina Msomimkatatamaa kuandika Katiba, sina raha na watu hawa. Maana wanaweza kunibadilishia kibao nikajikuta nanyea debe bila sababu. Hata hivyo, time will tell.
Kwa vile bado nimeshikilia usukani, lazima nipambane kuhakikisha nikistaafu sipewi namba lupango. Naona dege lenye mafua la rafiki yangu Njaa Kaya linakaribia kutua likitokea Aids ya Baba. Acha niwahi kumlaki ili animegee mbinu ya ku-survive.

No comments: