The Chant of Savant

Tuesday 8 May 2012

Tuanzishe sera ya hujumaa na kujimegea


ZAMA za Mwalimu Juliyasi Mchonga hasa kuanzia mwaka 1947 kauli mbiu ya kikaya ilikuwa ni Ujamaa na Kujitegemea. Kijiweni tumebadilisha kwa vile sisi na mabonge ya wajanja.
Tunasema kila mtu lazima afanye hujuma chini ya dhana ya Uhujumaa na ajimegee ofisini mwake. Naona yule msomaji kapuku anasonya ilhali yule msomaji kibopa anachekelea.
Yes, kijiwe kimegundua sayansi ya kutengeneza mabilionea kama Heze Maige, Lazarus Nyalandio, Bill Ngereza na wengine wengi. Sasa Heze mwenyewe kamwagwa manonihino, tutaona jeuri yake. Angekuwa Mchanaga angeambiwa hivyo Yethu!
Wakati kayani wanahangaishana na kufungana kamba kwa kupitia taasisi kama Takokula sisi kijiweni hatuna haja ya kudanganyana. Tumebariki jinai yetu na tumeipa jina na sera.
Sera yetu, nasisitiza, inaitwa Uhujumaa na Kujimegea. Hatufichi wala kufanya sanaa. Tunahujumu na kujimegea kama hatuna akili nzuri kiasi cha kukigeuza kijiwe kuwa shamba la bibi tena la nyanya. Upo hapo mshirika?
Lolol! Nshasahau mara hii! Naona kama nimedokoa stori badala ya kutoa uhondo kwa wasomaji. Nisameheni jamani. Wakati mwingine Mwenembago akipanda huwa napagawa.
Ngoja jamani niwape lau intorodakisheni ya sera yangu mpya. Definition, Uhujumaa na Kujimegea ni mfumo wa maisha ambapo kila mtu anaishi peponi kwa imani siyo matendo. Pia Uhujumaa ni mfumo wa kupambana na Ujamaa.
Katika mfumo wa Uhujumaa, wakubwa hujimegea vya wadogo na kuvifanya vyao na wadogo humegwa. Kwa maana nyingine ni kwamba wakubwa huwamega wadogo hasa wadogo wenyewe wanapokuwa woga na walalamishi wasichukue hatua.
Anayetaka kujua nimaanishacho arejea jinsi Denjaman Makapu alivyojimegea Kiwila na kuwaacha walevi wakipiga kelele. Angalia hata nkewe alivyojimegea flats na kuzipiga bei huku akiwaacha walevi wakihaha na pa kuishi.
Huo ndiyo Uhujumaa na Kujimegea ambapo wakubwa huwategemea waliwa ili kujineemesha wao na familia na marafiki zao.
Chini ya mfumo wa Uhujumaa na Kujimegea, familia, marafiki washirika hata waramba viatu huunda genge moja la kujimegea na kuhujumu. Hamkuona wakati wa kuunda upya baraza kuu kuu la maualaji ambapo makapi yalikuwa re-cycled na kuonekana mapya.
Chini ya mfumo wa Uhujumaa na Kujimegea wachovu kama Stivi Wahasira, Daudi Matthias Daudi, Bill Lukuwi, Makorongo Muhanga, Adumu Milima, Matiya Chikwawa, Melina Nugu, Joji Mkunjika na mengine wanaweza kurejeshwa.
Hayo tuyaache ni ya wadanganyika wanaojitoa waliwe tofauti na huko nyuma. Chini ya sera ya Uhujumaa na Kujimegea, tunaendelea kumega bila wasi wasi wala wisi wisi.
Zamani sikujua kuwa utapeli unafanywa na watu wa juu. Kwa imani yangu nilidhani utapeli na usanii ni kazi ya wachovu bila kujua kuwa kumbe hata wakubwa wanaweza kuwa matapeli.
Kutokana na mfumo huu sadifu na adhimu nilioubuni kama mzee Mchonga, nahakikisha kuwa ulaji wangu hauguswi hata wakija akina Mzito Kabwela na yule ras wa zamani Deo Filiponjombe kuutishia. Najifanya nina usongo na ufisidunia ilhali nami ni fisi aliyejificha kwenye makandokando ya ukuu.
Hamkumsikia kinara wa mafisidi akiwaunga mkono wadharauliwa kwa kushupalia dili zake wasijue lilikuwa changa la macho? Hakuna kitu kilinichekesha kama kufichuka kwa unafiki wa jamaa yangu Jimmy Mbatiya alivyoteuliwa kuula kama shukrani ya kujitoa.
Tamaa bwana, mwenye tamaa hana tofauti na fisi ambaye hata ukimuungia nyama ya fisi mwenzie, tena mtoto wake atafakamia kama Mbatiya alivyopwakia uchafu wa ukuu uchwara akakiweka rehani chama chake cha Enimasihara Mabadiliko.
Zamani nilijua mafisi ni Gusi Mlemavu na Joni Cheo bila kujua kuwa kumbe na Mbatiyaa ni bonge ya pandikiza ambaye naye ameunda sera yake ya utumiwaji na uliwaji.
Kama Chama Cha Magamba walivyoanzisha siasa za magamba ambapo magamba huwaita wanayoyakimbia magamba, nasi siku hizi tunaitana wahujumaa-siyo wahujumu kama wao.
Juzi nilishangaa nusu kukata roho niliposikia Nepi Mapepe akimuita Jimmy Millya gamba eti kwa vile amejitoa kwenye chama cha magamba. Kuongeza uhondo eti aliandaa maandamano ya kujiunga mkono kwa kisingizio cha wasomi wa vyuo vya juu.
Kuna bango lilikuwa likisema eti magamba yanajiondoa kwenye chama cha magamba. Anayeondoka ndiye gamba au gamba ni lile linalong’ang’ania kwenye mti ambao unaitwa chama? Wasomi hawawezi kuongeza ujinga kwa kwenda shule. Hivi kweli hawa walikuwa wasomi au wasoni?
Msomi hawezi kujipeleka utumwani au kukubali kwa hiari yake kugeuzwa kondoo au kuku. Msomi ni adui wa ukuku, ukondoo na unepi ulioonyeshwa na hawa matapeli wanaoitwa wasomi. Kama ni wasomi basi si wa vyuo vikuu bali vyoo vikubwa tu.
Msomi hafikirii kwa masaburi wala tumbo kama jamaa wa magamba ambao hawaamini kuwa kuna kesho ambapo watapigwa chini na kujikuta pakanga. Wangejua hivyo wasingeruhusu madudu wanayotenda.
Turejee kwenye mfumo wa Uhujumaa na Kujimegea. Chini ya mfumo huu mkuu huwa juu ya sheria kiasi cha kufanya atakavyo kama mfalme. Hata mfalme ana nafuu maana ni muwazi kuwa hapendi demokrasia tofauti na wahujumaa wanaojifanya wademokrasia wakati ni maimla wa kunuka.
Ni wangapi wanajifanya vipenzi vya watu wakati ni maadui wakubwa wa watu hao? Ni kipenzi gani cha watu anaweza kuwageuza watu hao punda wa kubeba kila upuuzi wake? Ni kipenzi gani cha watu anaweza kuwanyonya kwa kuwaweka rehani mikononi ni mifukoni mwa mafisadi wenzake?
Ni kipenzi gani cha watu anaweza kutumia pesa na raslimali za watu hao hao kwa kuzifuja yeye marafiki zake waramba viatu wake na familia yake? Huyu hakika si kipenzi cha watu. Heri sisi wahujumaa na wajimegeaji wanaofanya mambo yetu wazi wazi.
Naona mawaziri wapya wananikodolea macho hasa huyo wa manjagu na maafande, Emma Nchimbia, asije akanitia pingu. Ngoja nisepe zangu.
Chanzo: Tanzania Mei 9, 2012.

No comments: