The Chant of Savant

Tuesday 8 May 2012

Rais Kikwete aangalie asigeuke janga la kitaifa


Uteuzi wa Ladislaus Komba ambaye anatuhumiwa wazi wazi kujihusisha na uhujumu na ufisadi katika wizara ya Maliasili na utalii hasa kusafirishwa kwa wanyama 130 kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro ni aibu kwa taifa na aliyemteua.
Kashfa hii ilivuma sana huku ikiwahusisha watendaji wakuu wa wizara ya Maliasili na Utalii hasa waziri Ezekiel Maige na katibu wake mkuu Komba. Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ilizidi kupigilia msumari kwenye tuhuma hizo kwa kushauri wahusika wawajibishwe. Taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa kamati James Lembeli ilisema kuwa usafirishaji wanyama nje bila kufuata taratibu uliifanya kamati kupendekeza Bunge liiagize serikali kuwachukulia hatua kali za kinidhamu, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Ladislaus Komba, na wale wote waliohusika na utoaji wa vibali vya kusafirisha wanyama.
Inashangaza kuona kuwa pamoja na shutuma zote hizo, rais Jakaya Kikwete alipuuzia hata kamati ya bunge na kumteua mtuhumiwa kuwa balozi wa Tanzania nchini Uganda. Mtuhumiwa kama huyu anaweza kuiwakilisha nchi kwa maslahi kweli? Je kwanini rais aliamua kumteua haraka bila hata kungoja tume ya Bunge imalize kazi yake? Je kuna namna rais au hata watu wake walihusika na utoroshaji wa wanyama pamoja na ufisadi mwingine unaodaiwa kutendwa na wahusika? Hakuna kitu kinakatisha tamaa kama maneno yaliyosemwa na mchungaji Peter Msigwa hivi karibuni bungeni aliyekaririwa akisema, “Kule KIA (Kilimanjaro International Airport) vijana wanalalamika kuwa kuna baadhi ya watu wanaokuja kugongewa passport zao huku wenyewe wakiwa kwenye ndege.” Je hawa ni akina nani kama siyo wauza unga hata magaidi? Je rais ana nini na waharifu kama hawa? Si afadhali achague moja kati ya wananchi na hao wafanya biashara za utajiri wa haraka. Kwa nchi yenye uongozi wenye kujua unachofanya maneno ya Mbunge yangefanyiwa kazi siku hiyo hiyo. Maana ni ushahidi wa kuwapo tishio kwa usalama wa taifa. Je kama hao wanaogengeshewa mihuri wakiwa kwenye ndege kinyume cha sheria wanaachwa tumueleweje rais? Nini kazi ya genge la usalama wa taifa? Kama ni hivyo hakuna haja ya kuwa na watu kwenye viwanja vya ndege wala mipakani ili ijulikane kuwa hii ni No Man’s Land. Au hao nao wamebinafsishiwa uhuru wa Tanzania? Hivi rais anategemea wajukuu zake wataishije kwa uchafu huu anaoendelea kuuvumilia asitumie mamlaka aliyopewa?
Kuhusu yanayoendelea kwenye utoroshaji wa wanyama Lembeli alikaririwa akisema, “Kamati ya Bunge inapendekeza kwamba Bunge liitake serikali kumwajibisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, kwa kutengeneza mazingira ya rushwa ikiwa ni pamoja na kuyanyang’anya makampuni 16 vitalu vilivyogawiwa,”
Ajabu wakati kamati ya Bunge ikipendekeza waziri husika awajibishwe, rais ameendelea kukaa kimya. Ili iweje na kwanini kama hana maslahi na uoza huu?
Hapa tunaongelea watu wawili. Bado kuna wengine wengi ambao bunge limetaka wawajibishwe lakini rais ameendelea kulidharau bunge. Je kwanini wabunge wasiachane na siasa chafu za kulindana na kumshughulikia rais kama nao hawaridhiki au kushiriki uchafu huu? Kama kamati ya bunge inatoa mapendekezo yasitekelezwe maana yake ni kwamba bunge halina maana hata sababu ya kuwepo huku wabunge wanaowakilisha wananchi wakizidi kuonekana kama vikaragosi mbele ya mawaziri na makatibu wa wizara kama ilivyotokea kwa Komba.
Watu wenye mapenzi na taifa letu wanashangaa jinsi ambavyo Kikwete ameendelea kuwa mlinzi na muhimili wa watu wanaojulikana wazi kutokuwa na udhu wa kukaa kwenye ofisi za umma.
Hivi kwa mfano waziri wa nishati na madini na naibu wake wanangoja nini wakati wameishavuruga kwa viwango vyote? Rais ana faida gani na watu hawa?
Hivi mawaziri wanaojulikana kwa mfano kughushi vyeti vya taaluma wanangoja nini kwenye ofisi za umma wakati ni waharifu wa kawaida kwa vile hawakutaka kukanusha madai yaliyotolewa dhidi yao? Ingawa Kikwete amekuwa akijigamba kuwa serikali yake si ya ubia, ukitazama vizuri madudu anayoendelea kuyakingia kifua, unagundua kuwa kuna watu wana hisa kubwa kwenye serikali ya Kikwete.
Ukisoma ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa fedha za serikali (CAG) unapata kichefuchefu na kujiuliza nini kazi ya serikali hasa rais. Kwa mfano kwenye ripoti ya hivi karibuni iliitaja tena familia ya rais mstaafu Benjamin Mkapa kuwa mkewe aliuza majumba ya Msimbazi kinyume cha sheria. Ukiuliza kwanini Mkapa hachukuliwi hatua kutokana na ufisadi wa wazi aliotenda unaambiwa ana kinga. Unazidi kushangaa ni kwanini kinga ya Mkapa inakuwa yake, mkewe, wanae, wakweze hata marafiki zake?
Kwa hali ilivyo, nchi yetu inaanza kuonekana kama nchi ya vibaka ambapo mtu akiiba anazawadiwa kama ilivyotokea kwa Komba aliyeteuliwa balozi au Edward Lowassa aliyevurunda akazawadiwa marupurupu ya ustaafu wakati hakustaafu. Je namna hii rais wetu hajawa chanzo cha mauti yetu? Ajabu ni rais huyu huyu anayewanyamazia washirika wake anayelalamika kuwa serikali haina pesa. Anataka pesa ipi iwapo watendaji wake mawizarani, serikali za mitaa na kila taasisi wanaguguna kila kitu huku naye akichekelea na kuwalinda? Hakuna maneno mabovu aliyowahi kutoa Kikwete kama aliyotoa alipoulizwa swali juu ya kumshughulikia Mkapa akiwa nchini Sweden na kusema eti wamuache mzee Mkapa ajipumzikie. Wengi walishindwa kuelewa Ni kwanini rais wao ni mgumu kushughulikia ufisadi kiasi hiki kama hana faida na huo ufisadi. Kwa tabia yake ya kuwalinda wanaotuhumiwa kwa uharifu Kikwete na wenzake wametukamata mateka kiasi cha kutufanya tuendelee kuwa maskini wakati watu wachache wakitajirika kwa kutuubia. Kunogesha ngoma, Kikwete kaendelea kuwateua hata mawaziri uozo wanaojulikana kwa kashfa mbali kuanzia kughushi vyeti vya taaluma na upuuzi mwingine. Je nani atamkabili Kikwete na kumwambia imetosha?
Chanzo: Tanzania Daima Mei 9, 2012.

No comments: