The Chant of Savant

Monday 5 March 2012

Mlevi apata PhD katika Utawala


Ambuye muwapatse moyo

Ambuye muwadalitsa

Cholinga Ambuye lololo

Yehova Yire

EL Shaddai

Yehova Tsidkenu

Yehova Shalom

Yehova Shammah

Yehova Nissi

Ndugu zangu toka kule utawasikia wakisema: nyimbo yopembedzera iyi ndipo ndimayikonda

Kwanini nisiimbe kumsifu Mungu kunijali kupata PhD yangu ya Utawala toka kwenye chuo kikuu cha Topchekreti nchini Nohihino. Mie huwa sipendi kutangaza mambo yangu kama wale malimbukeni. nilikuwa nikisoma kisirisiri ili kuepuka wasiniroge au matapeli kuja kunishawishi niachane na kuharibu ubongo wanipe shahada feki kama zile za akina Imma Nchimvi, Makorongo Muhanga, Meli Nyagu, Bill Lukuwi, Dolorous Kamalashomile, Mustaafu Mkulu, Didas Makalio na wengine wengi wanaojiita wasomi na madaktari wakati ni vihiyo. Huwa nachukua shahada mbili yaani za kughushi na kupewa dezodezo. Huu ni ufisadi wa kitaalamu hata kama umebarikiwa na kuhalalishwa na wakubwa wenye maslahi nao.

Mada yangu au thesis ya shahada yangu ilikuwa “Mfumo wa Walevi unahitaji kurekebishwa nan a kutengenezwa mfumo mpya,” kwa kimombo ni “Structural and Sytemic Overhaul of the current corrupt system governing Walevi and the way it must be replaced.”

Pamoja na kwamba ukurasa mmoja hautoshi kueleza nilichokiandika hadi kupewa shahada ya udaktari, nitatongoa machache niliyodurusu hadi maprofesa wa kizungu wakapata kizungumkuti na kunipa shahada yangu hata kabla ya muda wake. Kitu kingine ni kwamba nimeiingi akwenye vitabu vya historia na maajabu kwa kuwa mwanafunzi wa kwanza kufanya shahada ya udaktari katika kipindi kifupi na kupata alama zote. GPA au kiwango changu cha alama kilikuwa 7.0. hii imewahi kufikiwa na Albert Einstein na Newton peke yao. Mie ni binadamu pekee aliye hai kuwahi kufikia kiwango hiki. Hii maana yake ni kwamba maswali yote niliyoulizwa tangu kuanza kujiandaa na mada yangu na mada yenyewe niliyajibu kwa kiwango cha juu kuliko hata walimu wangu.

Kutokana na mafanikio, nimepata mialiko mingi kwenda kufundisha vyuo vikuu hasa jinsi kanywaji kanavyofanya mtu kuwa kipanga.

kwa ufupi ni kwamba mada yangu kama nilivyoieleza ilikuwa ikihusika na mifumo mbali mbali ya kijamii na kisiasa chini ya utawala unakumbwa na ugonjwa uitwao ammaglobulinemia ambao mara nyingi ni mparaganyiko wa muundo wa viasilia. Pia kuna ugonjwa mwingine uitwao bulimia ukiandamana na mwingine uitwao megalomania kama nilivyoueleza hapo juu.

Kwa mfano, nilipofanya analysis-uchambuzi wa kina, juu ya kaya ya Bongolalaland, niligundua kuwa magonjwa haya yalianza kuiandama mwaka 1992 ilipochanganya viasili vya vyama vingi na chama kimoja kiasi cha kuzaa kiumbe wa ajabu aitwaye usanii au coniostosis carcinoma ambayo ni kansa ya hatari sana kisiasa. Kitaalamu hii niliita mitostic anomaly. Kiini hiki cha ugonjwa huu kilionekana katika nchi nyingi kuanzia Maghreb hadi kusini. Ndiyo maana Nato walivujisha fomula ya kukitibu kiasi cha kuzitibu nchi nilizotaja hapo juu.

pia niliweza kujenga dhana au theory ya kupambana na ugonjwa uitwao Kleptocracy au kitaalamu zaidi “kleptogonia” and “criminogonia” nilsema “ we need purebred of Jasmine like mindis that will thwart all alleles resulting from this abnormality in meiosis and mitosis of the cell of the country suffering from kleptocracy so as to become kleptogonia and criminogonia.”

Kusema ukweli sina tafsiri ya nondo hizi nzito ambazo ziliacha wazungu wakikuna vichwa na kugugumia kwa kujua kuwa kumbe kifaa kipo ila kilichelewa kujitokeza. Kanuni hii niliita Jasmin na ndiyo maana hata mapinduzi yote yaliyotokana nayo yanaitwa Jasmin Revolution.

kwa taarifa yenu Jasmine formulae kumbe ndiyo iliyotumiwa na waandamaji kule Libya Masri na Tunisia walikopi kwangu kutokana na fomula yangu kuvujishwa na NATO. Usimwambie mtu kwa sababu waliniomba msamaha yakaisha.

Kitu kingine ambacho kiliwachanganya maprofesa ni ile hali ya kutoka na minor thesis isemayo kwa nchi Matonya zikatiwe misaada ili watu wake wawe kama Jasmin na kufanya kweli. Nilisema wazi kuwa misaada wanayotoa wafadhili haisadii bali kuongeza alleles za ugonjwa kiasi cha Carsinoma kubadilika na kuwa Kaposi’s Sarcoma ambayo mara nyingi waganga huiita kansa ya ngozi in vivo. Lakini katika sayansi ya utawala hii Kaposi’s sarcoma tunaiita ufisi kutokana na kutandaa kwenye mwili wa nchi kwa kushambulia huku na kule kama fisi wafanyavyo. Hivyo jinaufisi au ufisadi kwa lugha nyepesi.

Hivyo misaada ikikatwa, kondoo watageuka fisi na kuanza kushambuliana na viini vya Kaposi’s sarcoma. Katika elimu ya chembe chembe za uhai Cellular anology and morphology hii huwa tunaiita killing the formation of malignant neoplasmic Golgi apparatus. haya madudu ni magumu kwa Kiswahili. Hivyo nitaomba niachie hapa nisije nikapasua vichwa vya wasomaji wangu ambao najua hawasomei PhD kama mimi ambaye nililazimika kuyasoma haya madudu ili kuipata na kuwakoga walioghushi na kupewa dezo.

Kwa ufupi ni kwamba mimi ni mtaalamu wa chembechembe za mfumo ndiyo maana ilinibidi kusoma chembe chembe za viumbe hai ili kuweza kulinganisha na mifumo ya dola. Uzuri wa PhD yangu ni kwamba naweza kwenda hospitalini na kutibu au hata kufundisha kwenye vyuo vikuu hasa wanafunzi wanaotaka kubobea kwenye utafiti wa chembe chembe za uhai. Ndiyo maana niligundua kuwa kanywaji kana chembe chembe zinazoamsha ubongo na kufanya kazi kama kompyuta.

Sitaki niseme mengi ili nisionekane najidai na PhD yangu. kwa ufupi ni kwamba ninaposema naitwa Dk. Mlevi Mdanganyika si kwamba naigiza au kutumia ya udaktari wa kughushi au kupewa. la! Nimesotea sana kwa madolari mengi ambayo yalitolewa na rafiki yangu na ndugu yangu Bill Gates na shemeji Mellinda. Ila usimwambie mtu ili Matonya wenu wenye masuti wasijeenda kumghasi kutaka asomeshe vitegemezi vyao visivyo na akili. Hamkuviona vingi vikiondoka na divisheni zero? Angekuwa kitegemezi changu siku hiyo ningemnyonga kama siyo kumkatakata vipande na kuwapa mbwa. Hata hivyo angepata wapi utaahira wakati wazazi wake wote tu vipanga? Hata bi mkubwa wangu anamalizia PhD yake kwenye uwekezaji. Uzuri anasoma majuu ambako hakuna shahada za chupi kama nonihino. Hata hivyo miwaya itawamaliza. Mwakaribishwa wote kwenye mnuso wa kusherehekea kutunukiwa PhD kwa mlevi isipokuwa wale walioghushi.

Chanzo: Dira Machi, 2012.





No comments: