The Chant of Savant

Sunday 1 January 2012

Jaji Bomani: Wageni wanaimaliza nchi

MWENYEKITI wa Tume ya Kufuatilia Kampuni za Madini Serikalini (TEITI), Jaji Mark Bomani alikaririwa hivi karibuni akiishauri serikali kubadilisha sheria za madini ili kuepusha utoroshaji wa fedha na madini unaofanywa na wageni waitwao wawekezaji. Ingawa asemayo jaji Bomani ni kweli, wa kulaumiwa si wageni bali watawala wetu vibaka waliotanguliza matumbo badala ya uzalendo na uwajibikaji bila kuwasahau wananchi wanaovumilia au kufumbia macho upuuzi huu.
Tujiulize maswali rahisi: kama wahusika ndiyo hao hao walioasisi na kutekeleza ujambazi kama Richmond, IPTL, Dowans, EPA, CIC, TICT na mwingine mwingi ambapo pesa iliyokwisha kutengenezwa tena ikiwa kwenye benki kuu iliibiwa na hakuna aliyewajibishwa, watahangaika na madini ambayo yanawaletea ten percent bila kutoa jasho? Huwezi kutawaliwa na watu ombaomba tena wakijisifu kwa uhodari wa kuomba ukategemea haya yasitokee. Tatizo siyo sheria mbaya bali wanaozisimamia na kuzitunga kupitia chama chako ambapo hoja hupitishwa kwa kuunga mkono chama badala ya sheria na hoja.
“Hakuna mfanyabiashara anayeweza kusema ukweli juu ya faida gani anayoipata kutokana na kuchimba madini, haiwezekani Tanzania tuendelee kuwa masikini wakati madini yetu yanayotoka yangeweza kusukuma mbele maendeleo yetu,” alisema Bomani. Hii pia ni kweli na ahitaji kuwa jaji au profesa wa uchumi au sheria kujua kuwa huu ni wizi uliohalalishwa. Je wahusika wanafanya hivyo kutokana na ujinga au wanajua sema matumbo yao hayawaruhusu kuona ukweli huu. Hawa si wajinga: wengi ni wasomi tena wenye PhD lakini ni wa hovyo na waroho.
Je wageni wanaoimaliza nchi yetu ni wawekezaji tu hata wengine? Je mchezo huu mchafu ulianza jana au umekuwapo kwa miongo mingi hasa bada ya awamu ya kwanza iliyojitahidi kuziba kila miayanya ya udokozi na ujambazi wa wazi wazi? Baada ya kuondoka kwa awamu ya kwanza, wizi ulibarikiwa wazi wazi. Wakati huu tulikuwa na wahindi wakifanya udukawallah ulioficha madhambi mengi kama uhujumu wa uchumi, ulanguzi wa bidhaa, ukwepaji kodi na utoroshaji wa fedha za kigeni. Nani wamekuwa wanawasaidia kukwepa kodi, kupata vibali feki na kuingia na kuishi kinyemela ukiachia mbali kutorosha pesa yetu?
Nani hajui kuwa mabohari mengi ya wahindi siku hizi yameficha wageni haramu toka India ukiachia mbali ubaguzi katika ajira ambapo wahindi huletwa kufanya kazi za hovyo wakijidai ni wataalamu. Kwani hili halijulikani? Rejea kashfa maarufu kama vile Chavda, Somaia, vithlani na wengine wengi waliohujumu nchi hii kupitia ujuambazi mbali mbali wakishirikiana na wakubwa wetu lakini hawakufikishwa mahakamani. Je tatizo ni wao au walikuwa makuwadi tu? Idd Simba waziri wa zamani wa biashara aliwahi kudai kuwa uchumi wa Tanzania umo mikononi mwa wahindi wapatao 10. Nani alihoji au kustuka? Nani angestuka wakati wahusika wanajua ukweli kuwa wao ndiyo wanufaika wa zahama hii kwa taifa na watu wake?
Nani hajui kuwa kuna wageni wanaokuja Tanzania wakijidai wataalamu toka nchi jirani wakati si wataalamu kitu? Je wanaingizwa na kuajiriwa na nani kama si watanzania wenyewe ambao wamejigeuza shamba la bibi kutokana na ufisi na ubinafsi?
Wageni wanaopata uraia wetu kinyemela hadi wanakuwa hata viongozi waandamizi kama ilivyogundulika miaka michache iliyopita huko Kagera ambapo mwenyekiti wa CCM wa mkoa aligundulika kutokuwa mtanzania. Mpaka leo, CCM haitaki kueleza ni kwanini mtu ambaye si raia alikubaliwa chamani na kufikia kuwa kiongozi mkubwa bila mamlaka kustuka. Hapa hakuna cha kuficha wala kuzungusha. Wageni hawa haramu walitumia uroho na upogo wa CCM kujipatia uraia hata uongozi tena wa juu.
Sababu nyingine itakayoimaliza Tanzania ni kuwa na mipaka iliyo wazi ikisimamiwa na watu waroho wanaoitumia kama duka lao la kutengenezea pesa kwa kuwatoza rushwa wageni na kuwaruhusu waingie nchini na kufanya watakavyo. Kwani hili halijulikani? Anayetilia shaka hili aende mipakani aone maafisa uhamiaji wanavyokusanya pesa kama makondakta wa daladala na kutokea kuwa matajiri wasijue wanachezea maisha ya vizazi vijavyo. Kwa ufupi ni kwamba mipaka yetu haina ulinzi wala udhibiti wa kutosha. Tarehe 22 Desemba 2011, nchini Kenya kwenye bandari ya Mombasa mamlaka ya bandari ilikamata pembe za ndovu zaidi ya mia moja na zote zilitokea Tanzania kutokana na viroba vilivyokuwa vimehifadhi pembe hizo kuwa na nembo ya Kilombero Sugar. Na hii haikuwa shehena ya kwanza. Ukiachia hilo, nani hajui kuwa soko la madini ya Tanzanite ambayo yanapatikana Tanzania pekee duniani liko Kenya na Afrika ya Kusini? Lakini ajabu nchi bado inajisifia kwa uombaomba ikielezwa kuwa nchi ya tatu baada ya Irak kupokea misaada mingi duniani lakini pia ikiwa mkiani kiuchumi!
Kitu kingine kitakachoimaliza Tanzania ni ile hali ya watanzania kutokuwa na vitambulisho vya uraia. Ajabu ni miaka sasa tangu serikali itoe pesa ya kutengeneza hivyo vitambulisho. Wahusika wametia pesa mfukoni na vitambulisho havionekani zaidi ya kupiga kalenda kila uchao. Nani anahoji au kujali iwapo kila mtu ameshika lake? Viongozi wanafukuzia ten percent wakati wananchi wanafukuzia pesa ya kula. Njaa ya ubongo na tumbo vimechanganyikana kiasi cha kuiacha nchi iibiwe kana kwamba wakazi wake ima ni mataahira au wanyama na hayawani wasio na akili.
Pia kuna tatizo la kuajiriana na kuteuana kwa kuangalia uanachama, urafiki, kujuana na mambo mengine kama hayo ambapo wahusika hujifanyia madudu bila kuchukuliwa hatua kutokana na wanaopaswa kuwashughulikia kuwa jamaa zao.
Tumalizie kwa kusema kuwa tatizo la Tanzania kwa sasa si wageni bali watanzania wenyewe hasa viongozi makuwadi wa wageni wanaowatumia kama mawakala wao. Haiwezekani nchi yenye kila idara na nyenzo za kiserikali isijue kinachoendelea. Wahusika wanajua kila kitu lakini kwa vile wao ndiyo wanufaika, hata hizo sheria tunazosema wabadili wanazitunga wao na hawatazibadili. Maana kufanya hivyo ni kuharibu ulaji wao haramu.
Chanzo: Dira Desemba, 2011.

No comments: