The Chant of Savant

Thursday 24 November 2011

Siku Lowassa alipomvisha gamba mwenyewe (Kikwete)




Hakuna ubishi kuwa rais Jakaya Kikwete alipokuja na dhana ya kujivua gamba, alilenga kutua mizigo ambayo imemwia mizito tangu alipoingia madarakani. Mojawapo ya mizigo hiyo ni Edward Lowassa na Andrew Chenge ambaye alimrithi toka kwa mtangulizi wake. Lakini kwa kadri Kikwete alivyoutege mtego wake, umemnasa hata kabla wanyama aliwalenga hawajatia guu mtegoni.

Wakati Kikwete akiandaa mtego alisahau kitu kimoja. Alisahau kuwa aliutega kwenye njia moja hiyo hiyo ambayo alitaka kupitia kurejea salama nyumbani . je angereaje nyumbani kupitia njia hiyo hiyo asiutegeu mtego au asinaswe nao? Sasa siyo siri. Lowassa amemvisha gamba Kikwete kiasi cha kushindwa kuelewa gamba ni nani na nani si gamba. Ingawa Lowassa amejitetea kuhusiana na Richmond, bado hawezi kukwepa kunaswa na mtego wa marehemu baba wa taifa.

Kwa wanaofuatilia hali ya mambo na jeuri ya akina Richmond hadi walipojibadili jina na kuitwa Dowans, wamepata siri ya jeuri yao. Kwa maneno ya Lowassa, hakuna shaka yoyote Richmond-Dowans ni Kikwete. Hebu tunukuu baadhi ya maneno yake. “Mwenyekiti utakumbuka kwamba mimi nilishaamua kuvunja mkataba wa Richmond mapema, lakini baada ya kukupigia simu ukiwa katika safari nje ya nchi ulisema tusubiri kwani ulikuwa umepata ushauri wa makatibu wakuu wa wizara, sasa leo hii ninahukumiwa nakuitwa fisadi kwanini?” Je Kikwete aliingilia mchakato mzima bila faida binafsi? Je rais anayevunja kanuni na kuvuruga utawala wa sheria anafaa kuendelea kuongoza nchi ambayo kimsingi anaikwamishwa kwa tamaa zake?



Hapa hakuna shaka kuwa kitendo cha Kikwete kumzuia Lowassa kuvunja mkataba kililenga kulinda maslahi fulani ya rais ambayo hata hivyo hayatajwi kwenye utetezi huu jadidi wa Lowassa. Je tujiulize swali moja, kwanini utetezi huu haukutolewa mapema? Jibu analitoa Lowassa kuonyesha kuwa la Kikwete na Lowassa ni moja. Anasema, “Nilijiuzulu kuwajibika kwa ajili ya kuilinda Serikali yangu na kwa heshima ya chama changu, sasa kwanini leo nahukumiwa kwa jambo hili, tena natukanwa na wana CCM wenzangu na siyo wapinzani nchi nzima kwamba mimi eti fisadi?,”

Kwa jinsi Lowassa alivyoyapanga maneno yake, kwanza anataka aonewe huruma kama mbuzi wa shughuli tuseme kafara. Pili anataka kumkumbusha Kikwete kuwa asingejitoa kuubeba msalaba wake Kikwete wote wangekuwa msambweni. Pia ni taarifa kwa Kikwete kuwa wakati wake naye kubeba msalaba wa Lowassa ni huu. Na kweli, Lowassa amefanikiwa kuzima harakati na shinikizo la kuvuliwa nyadhifa zake na kuadhirika. Laiti Rostam Aziz asingefanya papara, naye angegoma. Maana mgomo na ushawishi na siri vya Lowassa havikumwokoa peke yake bali hata mwenzake Chenge.

Kimsingi, hoja ya Lowassa ina mashiko kuwa magamba ndani ya CCM si mawili wala matatu bali wote. Hali inakuwa mbaya zaidi gamba kuu linapokuwa rais na mwenyekiti wa CCM ambaye kwa kiasi fulani anaweza kuonekana mnafiki kuanzisha harakati hii bila kujua kuwa naye ni sehemu ya gamba tena nenen kuliko yote.

Kimsingi, Lowassa amefanikiwa kuvua gamba lake na kumvisha mwenye gamba. Tumesema. Lakini hatukusikilizwa.

Kitu kingine ambacho Lowassa amefanya ni kuthibitisha ukweli wa madai ya Dk Wilibrod Slaa katibu mkuu wa CHADEMA aliyetoa orodha ya mafisadi kule Mwembe Yanga ikiongozwa na Kikwete mwenyewe. Kikwete alijitahidi kutojibu tuhuma za Slaa akidhani zitajifia na kuwang’ang’ania wenzake asijue ikifika siku ya kifo kila mtu hpambana kuokoa nafsi yake kama alivyofanya Lowassa.

Hivyo tuhitimishe kwa kusema kuwa mchawi aliyekuwa akitafutwa na CCM kumbe ni mwenyekiti wao! Je ni kudhalilika kiasi gani kwa Mwenyekiti wa chama tawala na rais wa nchi kuwahadaa watu wake kuwa anaweza kupambana na ufisadi wakati yeye ndiye fisadi nambari wani?

Tumalizie kwa maneno mengine ya Lowassa. Anasema, “Mwenyekiti nikukumbushe mwaka 1997 kule Zanzibar, kina Mzee Daudi Mwakawago walikuja na mafaili yakiwa na tuhuma dhidi ya mtizamo hasi wa jamii dhidi yako, kwa hiyo wakati ule kama si busara za kina Mzee Mkapa (Benjamin) leo usingekuwa hapo ulipo”.

Kauli hii ina ujumbe mahususi kuwa Kikwete asijisahau. Pili ni kumkumbusha kuwa, licha ya kuchafuka kiasi cha kutotamanika, bado ana rungu la urais ambalo anaweza kutumia kumwokoa Lowassa ili aweze kuendelea na mbio zake za kuusaka urais hapo 2015. Ukweli huu umo kwenye maneno haya ya Lowassa, “ Mwenyekiti nikukumbushe jambo jingine, kule Zanzibar mwaka 1997 walipoleta tuhuma za mtizamo wa umma dhidi yako, ulisema kwamba kuwa Rais ni mipango ya Mungu,”

Wengi wanangojea kuona ni usanii gani mwingine atafanya Kikwete kuepuka aibu hii. Pia hapa ndipo siri ya kuenguliwa kwa spika wa zamani Samuel Sitta inapojulikana. Maana, kimsingi, Bunge ilipaswa likae na kuangalia kashfa ya Richmond upya pamoja na ukweli kuwa rais na Lowassa (waziri) mkuu licha ya kulidanganya bunge na taifa, walificha ukweli kwa faida zao binafsi. Hakika, huu ni mtihani mwingine kwa spika wa sasa Anna Makinda na tuhuma kuwa alipachikwa pale kufua nguo chafu za serikali. Ajabu ya maajabu, bado magamba haya yanawafuatafuata akina Sitta kutaka kuwaadhibu pale ambapo wanapaswa kuadhibiwa wao. Je wabunge wetu nao watakubali kugeuzwa nepi za rais na watu wake? Pia kuna haja ya kuangalia upya hata haya malipo ya Dowans bin Richmond. Maana kutokana na shutuma hizi mpya ni kwamba anayelipwa ni Kikwete na watu wake na ndiyo maana hataki kutetea wananchi dhidi ya ujambazi huu wa mchana.

Hakika Kikwete naye ni bomu au tuseme gamba. Anapaswa kujiwajibisha au kuwajibishwa mara moja kutokana na mateso taifa linayopata kutokana na tamaa zake. Hapa ndipo upinzani unapopaswa kuachana na majadiliano na kuingia mitaani ili haki itendeke-kieleweke. Kazi kwetu.

No comments: