The Chant of Savant

Wednesday 26 October 2011

Sitta anataka kumdanganya nani?


Hakuna ubishi kuwa Waziri wa Jumuia ya Afrika Mashariki na Mbunge wa Urambo, Samuel Sitta, ni mmojawapo wa wanasiasa wakubwa nchini tena wenye historia ndefu na pana ya taifa letu.

Sitta, ni kati ya wazee walioonekana kama wenye msimamo wa kuleta maendeleo kwa taifa hasa kwa jinsi alivyoendesha Bunge alipochaguliwa kuwa spika wake.

Hakuna kitu kilimpatia sifa na heshima kubwa kama kuridhia kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye ni Naibu Waziri wa Ujenzi.

Maana ni kupitia maamuzi ya Kamati ya Mwakyembe, kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa, waziri mkuu aliweza kulazimishwa kuachia madaraka yake baada ya kubainika kuwa nyuma ya kashfa ya Richmond. Leo hatutaongelea maana ya Richmond maana wengi wanaijua kutokana na kuwa sehemu ya kongwa shingoni mwao.

Tunachoweza kusema ni kwamba tutaongelea kampuni mtoto wa Richmond yaani Dowans ambayo imeshinda tuzo la shilingi 111,0000,0000,0000 ambazo zinapaswa kulipwa na Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO) kwa kuvunja mkataba na kampuni hii.

Tuzo hili lililotolewa na mahakama hivi karibuni limeigawa nchi baina ya watu wachache wenye madaraka na wanaodhaniwa kuwa nyuma ya hujuma hii na wengi wasiopenda kusikia neno kulipwa Dowans.

Mmojawapo wa watu wanaotaka Dowans isilipwe ni Sitta. Kupinga pesa ya umma kulipwa kwa mafisadi si jambo baya. Ila kwa mtu wa aina ya Sitta kusema Dowans isilipwe pekee hakutoshi.

Wapo wanaouliza: Yeye kama mwanasheria kitaaluma na waziri kwenye serikali yenye kuonyesha kasi ya ajabu kuilipa Dowans anachukua hatua gani binafsi? Hivi kujiuzulu nako kunahitaji ushauri zaidi ya uzalendo na utayari kuwa serikali husika haifai?

Je, mtu anayekaa ndani ya serikali hiyo hiyo na kuwaaminisha umma kuwa anaichukia si mbaya kuliko hata wale wanaokaa kimya?

Wapo wanaokwenda mbele na kuhoji: kwanini Sitta asijiuzulu toka kwenye serikali inayoonyesha wazi kulalia ufisadi badala ya kukaa humo humo na kupiga mdomo na kulalamika?

Wengi wanashangaa kwanini Sitta hataki kujua kuwa kikwazo cha kila kitu ni bosi na rafiki yake Rais Jakaya Kikwete. Je, Sitta anadhani watanzania wamesahau yeye na Dk. Mwakyembe walipowasaliti kwa kutotoboa ukweli wote kuhusiana na walioko nyuma ya Richmond?

Leo anakuja na maneno kuwa waziri mkuu akijiuzulu serikali yote inaanguka. Kama ni kweli mbona kamati yake na Bunge lake hawakushinikiza serikali ijiuzulu na badala yake walidandia kupewa vyeo vidogo kwenye serikali hiyo hiyo?

Namheshimu sana mzee Sita. Heri ajinyamazie na kuendelea kusutwa na nafsi yake kama ana udhu kiasi hicho au aendelee kutetea mkate kwa kutetea serikali legelege iliyoshikwa na mafisadi.

Katika hali hii you must either be pregnant or not pregnant but not both.

Ajabu Sitta hivi karibuni alikaririwa akisema kuwa hakutegemea Lowassa aachie ngazi na kama angefanya hivyo basi alijua serikali nzima ingeporomoka. Hii maana yake ni kwamba sifa inazopewa Kamati Teule ya Bunge haizistahili ikichukuliwa kuwa haikuwa imedhamiria kumtimua waziri mkuu na kama ingekuwa imedhamiria, alipojiuzulu kwanini kamati haikushinikiza serikali nzima iachie madaraka.

Hili ni swali ambalo Sitta na wenzake litawaandama daima huku nafsi zikiwasuta kuwa walisaliti umma kwa ajili ya vyeo tena vidogo vya muda.

Wanaokumbuka kashfa ya Watergate iliyomuondoa madarakani rais wa Marekani Richard Nixon watakumbuka jinsi mambo yalivyokwisha tofauti na ilivyotegemewa kama ilivyotokea kwa Lowassa.

Je, Lowassa alijiachia madaraka kwa hiari yake kama sehemu ya uwajibikaji? Kama ni hivyo mbona alilalamika baadaye? Kama ni hivyo kwanini aliendelea kutoelezea alichojua kuhusiana na Richmond? Kama ni hivyo kwanini Lowassa hakutaka kuongelea tuhuma mbali mbali za ufisadi hata kabla ya Richmond zinazoendelea kumwandama?

Je, Lowassa alilazimishwa na bosi wake yaani rais Kikwete kuepuka siri zote kumwagwa hadharani? Je, aliachia ngazi kuokoa serikali akitegemea angerudishwa kwa mlango wa nyuma? Je, Lowassa alifanya uamuzi kutokana na hasira au kuogopa hatari ya kuletewa ushahidi zaidi na kuishia kifungoni?

Ingawa Lowassa ana zigo lake la tuhuma, spika aliyeunda tume iliyommaliza Lowassa, Sitta hawezi kuendelea kujionyesha kama mtu mwema wakati anatumikia serikali hiyo hiyo inayonuka.

Hawezi kueleweka kuiambia serikali isiilipe Dowans wakati anaendelea kubaki kwenye serikali ile ile.

Laiti Sitta angekuwa mkweli pamoja na mwenzake Dk. Mwakyembe wangeeleza yaliyofichwa na kamati teule ya Bunge na kuomba msamaha yakaisha. Bila kufanya hivyo nao wataendelea kuwa wanafiki na mfisadi wa kawaida waliohongwa vyeo uchwara kwa kuisaliti nchi.

Tatizo kubwa la wanasiasa wetu wengi ni kudhani kuwa umma hauna akili wala kumbukumbu kujua nani ni nani katika nini.

Mwakyembe na Sitta wamekuwa wakiisakama serikali lakini ajabu hawataki kutoka kwenye serikali hiyo hiyo! Wamekuwa wakitaka waonekane kama wapiganaji dhidi ya ufisadi kwa kuendelea kutumikia serikali wanayoituhumu kuwa fisadi!

Huwezi kusema kuwa serikali ya Kikwete ni ya kifisadi lakini bado ukasema eti Kikwete si fisadi. Ni ajabu hata Kikwete anawavumilia au ni kwa vile wote wanatumiana? Yale yale ya Magomeni! Aliyeuza dhahabu feki kapewa noti feki. Mchezo kwisha!

Je, Sitta anataka kumdanganya nani wakati kila kitu kiko wazi? Heri mzee Sitta angejinyamazia na kuendelea na cheo chake kitokanacho na kazi pevu aliyofanya kuinusuru serikali anayoishambulia kila siku.
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 26, 2011.

No comments: