The Chant of Savant

Tuesday 4 October 2011

Hongera Lowassa kuivisha gamba CCM


Mpendwa Edward Lowassa, salaamu,

Naomba tena nitumie fursa hii adimu na adhimu kuwasiliana nawe tena. Nafanya hivyo kutokana na baadhi ya mambo kunichanganya kiasi cha kusikia umbea mwingi. Nakuandikia angalau kutaka kujua ukweli na uongo ni upi.

Kwa mara nyingine nimepata fursa ya kutimiza ahadi yangu ya kukuandikia tena kuhusiana na mvutano uliokuwapo baina yako na Chama Cha Mapinduzi (CCM) pale kilipokutuhumu kuwa gamba (fisadi papa kwa kuazima usemi wa Reginald Mengi).

Hata wauiteje, kitendo cha kuendelea kushikilia nafasi ulizoamriwa kuachia ni ushindi mkubwa kwako na kuivisha gamba CCM iliyotaka kukuvua gamba. CCM walishazoea kujigamba kwa kufunga magoli ya kisigino wasijue wewe umewafunga na mkono!

Juzi nilisikia wambea wakisema eti wewe ni fisadi wa kunuka ndiyo maana hukuhangaika kujibu wala kujitetea bali kunyamaza na kupanga mipango ya kuwashikisha adabu CCM kabla hawajakushikisha adabu.

Kuna washenzi wanasema eti ulinyamaza kwa kuogopa CCM wasikunyime marupurupu na makandokando ya uwaziri mkuu mstaafu kwa sababu wewe hukustaafu bali kulazimiswa kuutema ulaji. Katika wambea hao kulikuwa na wanasheria waliosema kuwa kwa muda uliokaa kwenye uwaziri mkuu huna sifa ya kuitwa mstaafu wala kulipwa marupurupu ya ustaafu. Wambea walikuwa wanasema kuwa pesa unazopewa kama si fadhila basi ni aina nyingine ya ufisadi wa kimfumo. Mie napingana na hawa kwa vile cha mlevi huliwa na mgema kama wewe. Na pia hawa hawakujui vizuri. Ulipewa miezi mitatu, ukapangua. Uliongezewa mwezi na ushei, nao umepangua. Sasa wanataka uonyeshe umwamba gani zaidi ya huu?

Bwana Mkubwa,
Wengi wanakumbuka tambo na kujipiga kifua za CCM huku baadhi ya vinara wake wakikukamia wasijue wewe ni gari kubwa. Yako wapi sasa? Si wamefyata mkia. Walisema eti wanakupa mwezi mmoja ujivue gamba wasijue watanywea kama konokono aliyenuswa na simba.Hivi hawa hawakujua kuwa wewe ni morani? Hata yule Bwana mdogo aitwaye Nape siku hizi simsikii akikoroma na kuapa kuwa lazima uvuliwe gamba. Je ulimuita na kumpa vipande vyake au una maswahiba chamani waliomtonya na kumwabia aache kuharibiana ulaji?

Mpendwa,

Katika waraka wangu niliokuandikia mwezi jana, ingawa hukuujibu moja kwa moja, nilifurahi kukumbuka vipande vyako ulivyotoa kwenye kata ya Moita hapo mwezi Julai alipojivua gamba Rostam Aziz mshirika wako wa zamani kwenye maulaji ya Richmond. Nakumbuka ulisema kuwa kama wangekutimua kwenye chama basi ungeondoka na wabunge 11 na mawaziri wanne ambao hukuwataja. Mwanzoni mie nilidhani ulikuwa mkwara nisijue ni ukweli.

Naona nimeongea mengi kiasi cha kusahau hata kukupongeza kwa ushindi wako wa kishindo dhidi ya CCM ambayo ilitaka kukatiza mbio zako za kugombea urais mwaka 2015.Nakumbuka pale Moita ulisema lazima ugombee urais mwaka 2015 hata kama ni kusimama kama mgombea binafsi.

Leo sitauliza maswali mengi isipokuwa machache. Je bado unaamini kuwa hata ukigombea nje ya chama chochote unaweza kushinda? Je kama wapiga kura watakuuliza kilichokutoa CCM utawajibu nini? Na je kama utaendelea kuwa kwenye CCM kama ambavyo hali inaonyesha, kama waliotaka kukuvua gamba watakataa kukupendekeza kugombea utafanya nini? Ina maana utawapiga mkwara kama uliowapiga kwenye kujivua gamba wanywee? Je ombi langu la kutaka utangaze mimali yako na kupangua shutuma za kashfa ya Richmond, Dowans, kujilimbikizia mimali na nyingi umelifikiria vipi?

Juzi nilizinyaka kuwa CCM inakuvutia pumzi. Wambea wanasema kuwa baada ya kumaliza kibarua kigumu cha Igunga ambapo mambo si mazuri kwa CCM, kuna uwezekano wa kukuita na kukupa talaka yako. Je kama watafanya hivyo una mpango gani wa kupangua? Je ukweli ni upi, umewagomea na kuwabwatukia wakanywea au wanakuvutia pumzi ili wamalizane cha Igunga?

Je ule mtandao wako bado una bao? Kuna kitu nilikuwa nimesahau. Vipi zile shutuma kuwa mwanao Fred alihojiwa na mamlaka za Uingereza kwa kuingiza mabilioni ya shilingi bila maelezo? Je ni kweli Fred ni mfanyabiashara maarufu? Je anafanya biashara yake au ya familia?

Je kwanini hukwenda Igunga kumpigia kampeni mgombea wa CCM wakati swahiba na mwenzio Rostam alifanya hivyo? Je uligoma, kuzuiliwa au? Pia kabla ya kusahau, bado ule mradi wa kujenga ofisi ya bei mbaya kwa ajili yako mjini Monduli bado unaendelea?

Kabla ya kusahau, vipi ule ushauri wako kwa CCM, hasa viongozi wake, kufanya maamuzi magumu mojawapo likiwa kukutimua, je walikujibu au wanaendelea kukuvutia pumzi ili wakufanyia maamuzi magumu yaani kukutosa bila kujali kuwa ulikuwa mwenzao? Je kama mojawapo ya maamuzi magumu itakuwa kukushikilia hadi ujivue gamba, utaendelea kuwashauri wafanya maamuzi magumu tena? Hivi kati yako na wale wanaosema uvuliwe gamba nini adui wa CCM anayeiangusha mbele ya jamii? Je ni wewe unayekataa kuachia ngazi au wale wanaozungushazungusha mambo wakati kila kitu kiko wazi? Je mwoga ni yupi, wewe unayeogopa kutoka au wao wanaoogopa kukutoa?

Nauliza maswali hapo juu si kwa kejeli. Ni kwa sababu nimechanganyikiwa kwa hiki kinachoendelea ambapo mnapimana ujogoo huku wapiga kura wakiendelea kusota na kuhisi kama wamesalitiwa.

Nimalize kwa kukupongeza tena kwa kuishinda CCM. Swali ni je, hizi zitakuwa mbio za sakafuni au wataendelea kukugwaya huku wewe ukitesa na kujiandalia kuutwaa urais mwaka 2015 come shine come rain?

Chanzo : Dira Oktoba 2011.

No comments: