The Chant of Savant

Friday 28 October 2011

Aibu serikali kutolewa vyombo nje


Habari kuwa wizara ya Habari Utamaduni na Vijana na Michezo ilitolewa vyombo vyake hivi karibuni baada ya kutolipa pango la nyumba kwa mwenye nyumba yaani NHC ziligonga vichwa vya habari. Wengi wanajiuliza. Inakuwaje wizara inayopangiwa bajeti kila mwaka kushindwa kulipa pango la nyumba kama hakuna ufisadi? Je pesa inayotengwa kwenye bajeti kwa ajili ya kulipia pango inakwenda wapi na kwa nani? Ajabu utashangaa kusikia kuwa wakubwa wa wizara wanaishi kwenye mahekalu ya serikali ukiachia mbali kuporomosha mahekalu yao binafsi? Je pesa ya pango inaishia kwenye mifuko na miradi ya wakubwa wa wizara?

Tumejuzwa deni la pango. Vipi madeni ya maji, simu umeme na mambo mengine? Maana kwa hali ilivyo, ni kwamba kila mtu anajifanyia atakavyo ilmradi ni wakati wa madili uliopindua maadili. Anayebishia hili ajiulize ni matajiri wangapi anawaowajua tena watu walioanza kazi jana kwa vyeo vya chini lakini wana mimali ya kutisha. Nenda ukachunguze wafanyakazi wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere au KIA utajua ninachomaanisha. Usiishie hapo. Nenda bandari, uhamiaji, mita za mafuta, TRA hata mbuga za wanyama utajua nimaanishacho. Ukitoka hapo malizia benki kuu na wizara ya biashara utaona ninachomaanisha. Tunaipeleka wapi nchi? Ajabu hakuna anayejali. Hata wakubwa wanaotuaminisha kuwa wako makini hawastuki wala kushangaa!

Turejee kwenye kashfa hii ya wizara kushindwa kulipa pango la nyumba. Kwa ufupi ni kwamba NHC, Kama Tanesco haipaswi kuwa maskini kama ilivyo. Nani hajui kuwa wapangaji wengi ni watu wa mbari fulani tena wenye uwezo lakini wakilipa kiduchu ukilinganisha na wapangaji wa Kiswahili wanaopanga uswahilini? Ingawa NHC inaitwa Msajili wa Majumba, kimsingi si msajili wa majumba bali msajili wa Wahin… malizia tusijeambiwa tunahubiri ubaguzi. Ajabu ubaguzi kwenye upangaji wa nyumba na umilki wa biashara tena zitokanazo na ufisadi si ubaguzi! Nani hajui kuwa wezi kama akina Chavda na wengine wengi wanaendelea kutanua huku vibaka wakimalizwa kwa moto?

Hii maana yake nini? Serikali inaona uchungu kwa wizara yenye kutumia pesa ya walipa kodi, kutimuliwa kwenye nyumba wakati serikali hiyo haioni uchungu pale makapuku wanaponyanyaswa na kunyonywa na wenye nyumba wanaoweza kujipangia kiasi cha kodi bila kubughudhiwa. Hivi nani hajui kuwa wapangaji wengi mijini wamegeuka watumwa wa wenye nyumba wenye tamaa wanaodai kiremba hadi kodi ya mwaka kwa mtu anayelipwa kwa mwezi? Hii ndiyo maana hatuna uchungu na wizara kutupwa nje ya nyumba. Tungeshauri na Tanesco na DAWASA wawakatie huduma hadi walipe. Maana kwa kuendelea kuwavumilia tunaumiza watu wetu. Kwanini kuwavumilia wakati ni hao hao wakwepa kodi ya pango wanaoingia mikataba ya kipumbavu na wezi kama Dowans na kuishia kugawana mabilioni ya kodi zetu huku tukilazwa kwenye kiza kama mende?

Wenye uchugu na taifa letu wana hasira na kisasi na watendaji wanaotumia mamlaka yao kuzidi kuwaibia maskini kodi zao. Kwanini wizara inapata pesa ya kulipa posho za vigogo wake, pesa ya kupitisha bajeti, kujipongeza hata ya kukirimu wageni lakini wizara hiyo hiyo ikakosa pesa ya kulipa pango la nyumba? kunani hapa? Ingawa Afrika inasifika kwa umaskini na uomba omba wake, ukweli ni kwamba hivi havijaumbwa na Mungu bali ombwe la uongozi na vipaumbele uchwara. Inashangaza nchi inayoweza kutumia mabilioni kwenye jimbo moja la uchaguzi kushindwa kulipa pango la wizara yake na hakuna anayewajibishwa.

Nani hajui kuwa tatizo letu ni kuvipa umuhimu vitu vya hovyo na kuvipuuzia vitu vya muhimu? Hebu angalia tunavyowekeza kwenye siasa badala ya huduma za jamii. Jiulize ni helkopta ngapi zilitumika Igunga lakini kura zikasafirishwa kwa mikokoteni na punda? Je hapa tatizo ni raslimali au busara akili na utashi katika kuweka vipaumbele? Kwanini, kwa mfano, serikali inapata pesa ya kununua mashangingi mawizarani, mikoani na wilayani lakini ikashindwa kulipia pango, umeme, simu, maji na huduma nyingine?

Ajabu nchi isiyo na pesa ya kutosha kulipia pango, inaruhusu majambazi wachache kutorosha madini na wanyama na hakuna anayestuka? Nani hajui kuwa pesa nyingi ya kodi inaishia kwenye mifuko ya watendaji wachache wa umma kama tulivyobainisha kuhusu TRA, viwanja vya ndege, mipakani na kwingineko? Kwani hili halijulikani au kwa vile waajiriwa kwenye maeneo haya ni watoto wa wateule au vibaraka wao wanaokula nao? Nani hajui kuwa wengi wa matajiri kwa mfano wa viwanja vya ndege ni waajiriwa wa serikali na wauza unga? Kwani siri? Ajabu utasikia TAKUKURU ikitoa kila maigizo na kushindwa kuwachunguza watu ambao utajiri wao haulingani na vipato vyao. Lakini TAKUKURU itafanyeje hivyo wakati watendaji wake wengi nao wana mali nyingi zilizopatikana kifisadi sawa na wenzao wanaopaswa kuwachunguza.

Leo askari wa usalama barabarani wamegeuka askari wa balaa barabarani kutokana na kula na wahalifu wanaoendesha magari kinyume cha sheria huku polisi wakila na majambazi, wanasiasa na wafanyabiashara haramu na majambazi wakubwa na wananchi wakiendelea kuwa mashuhuda.

Tumalizie kwa sakata la wizara kufungashiwa virago. Ajabu ni kwamba wakubwa watang’aka na NHC itanywea na wizara kuendelea kufanya vitu vyake. Nani anajali kwenye taifa ambalo halina mwenyewe na kila mtu anatesa kwa zamu. Hivi kweli haya nayo yanahitaji rais kuingilia au wananchi wenyewe wanaweza kufanya hivyo kwa kushinikiza serikali iwajibike vinginevyo waitimue? Hata kama wananchi kwa ujinga, ukondoo na kuishi kwao kwa matumaini ni waathirika, wasipopaza sauti nani atawasaidia badala ya wao kujisaidia wenyewe? Tieni akilini.
Chanzo: Dira Oktoba 2011.

1 comment:

Jaribu said...

Rais mwenyewe anahongwa suti na kila siku kulalamika utafikiri hana madaraka. Utakuwa disappointed ukitegemea top down solution.