The Chant of Savant

Thursday 29 September 2011

Mbunge Lusinde anavuta bangi?

mbunge wa Mtera livingstone Lusinde akimtambulisha mgombea ubunge wa CCM Igunga Dk Dalaly Kafumu huku Lugubu Itumba Igunga Tabora

UHUNI ni kutenda tofauti na ulivyotegemewa kutenda. Kwa mfano, mtu mzima akifanya mambo ya kitoto huitwa mhuni. Je, mbunge anapotenda kama mvuta bangi wa kawaida tumuiteje? Inachanganya hasa kwa msikilizaji au msomaji anaposhindwa kutofautisha maneno ya mheshimiwa mbunge na mpiga debe wa daladala pale Mwenge.

Kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga, mkoani Tabora zimezua mambo. Ukiachia mbali Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuja na mpya ya kuhonga wapiga kura ubwabwa, huku kukiwa na fumanizi la mwaka linalodaiwa kumhusisha kigogo wake wa fedha, Mwigulu Mchemba, vituko vingi vimejitokeza. Hii ni aibu kwa chama kinachojiita mhimili wa usawa, haki na maendeleo ya taifa.

Kituko kitakachojadiliwa hapa ni maneno ya Mbunge wa Mtela, Livingstone Lusinde. Wahenga wanasema mchezo mbaya ni kazi mbi. Na mzoea vya kunyonga, vya kuchinja haviwezi.

Lusinde anasifika kwa kumng’oa madarakani kigogo wa siku nyingi wa CCM, John Malecela, ambaye amewahi kushika nyadhifa nyingi kuliko mwana-CCM yeyote aliye hai.

Hata hivyo ushindi wa Lusinde haukuja kirahisi na kistaarabu ukiachia mbali mizengwe na vita ya kimakundi. Lusinde anakumbukwa jinsi alivyokuwa akitumia maneno ya kihuni dhidi ya mkongwe Malecela, jambo ambalo linaonekana kuwa kasumba kiasi cha kumtukana Dk. Willibrod Slaa.

Kinachoshangaza ni ile hali ya Lusinde kuendeleza matusi hata baada ya CCM kuushutumu upinzani kufanya hivyo. Kinachoshangaza zaidi ni ukweli kwamba Lusinde huyuhuyu alithaminiwa na CCM baada ya kuisaliti CHADEMA chama kilichomfikisha hapo alipo.

Ajabu ya maajabu ni pale CCM ilipodai wapinzani wanaendesha kampeni chafu wakati kiongozi wa kampeni chafu ni CCM yenyewe.

Hivi kuwahonga wananchi ubwabwa ni matusi ya nguoni kiasi gani?

Twende kwa Lusinde anayeitwa mheshimiwa mbunge, ingawa hana hiyo heshima wala kuistahili kama atasikilizwa na kuchunguzwa vilivyo. Hebu soma nukuu hii: “Hapa nimewaona waandishi wa gazeti la Mbowe (Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA); nataka mkaandike kwa namna ambavyo tumezunguka, CCM tukishindwa nakunywa sumu,” alisema.

Je, huyu anayeitwa mheshimiwa hajui kuwa kujiua ni kosa la jinai? Je, anatoa funzo na picha gani kwa Watanzania? Je, asipotimiza hili afanywe nini? Je, ana vigezo gani kuwa CCM itashinda? Je, kuna mbinu ya kuchakachua ambayo Lusinde anaijua kiasi cha kujipa uhakika wa mia kwa mia kuwa watashinda pamoja na kuvuruga kampeni kwa kufumaniwa na kushindwa kutangaza sera zao? Je, CHADEMA hili wamelichukuliaje? Je, wananchi hasa wapiga kura wanalichukuliaje hili? Ajabu CCM imeshindwa hata kumkemea!

Lusinde hakuishia pale kuonyesha uhuni wake. Alikaririwa akisema, “Nataka tuwaambie, tutawapiga bao la mbali kabisa na huyo Dk. Slaa sisi tunammudu ndiyo maana tukamwambia mzee Kikwete, endelea kuongoza nchi atuache vijana tumkabe koo maana yule mzee ni mnafiki mkubwa.”

Hivi huyu Lusinde hajui kuwa kumuita mtu mnafiki ni kumkashifu waziwazi? Sijui kiwango cha elimu cha kiumbe huyu. Ila kwa aliyokaririwa akibwabwaja, kuna uwezekano hana elimu ya kutosha na kama amefika hata chuo basi ni wale wanaobebwa au kuingia kwa namna kama siyo kughushi kama mawaziri waliotamalaki kwenye baraza la sasa la mawaziri waliotuhumiwa na Keinerugaba Msemakweli.

Hebu tuendelee kumchambua Lusinde. Ukiachia nukuu mbili hapo juu, Lusinde alikaririwa akikazia kinachoweza kuonekana kama uhuni kwa kusema: “Kale kazee kagonjwa kale, ndiyo maana nimekuja kuwaambia inawezekana viongozi wa CHADEMA wanavuta bangi, zile bangi zile, haiwezekani unatembea nchi nzima unahamasisha vurugu, unatangaza vita.”

Ajabu Lusinde, mjumbe wa NEC wa CCM, Je, Lusinde anaweza kuthibitisha madai kuwa viongozi wa CHADEMA wanavuta bangi na amejuaje wanavuta bangi kama yeye havuti? Je, ni viongozi wangapi wa CCM wavuta bangi? Tunauliza swali hili kutokana na Lusinde kuonyesha kipaji cha kuwajua wanasiasa wavuta bangi.

Je ikibainika kuwa viongozi wa CHADEMA si wavuta bangi, Lusinde ataweka wapi uso wake ukiachia mbali kuchukuliwa hatua za kisheria? Je, hizi ndizo sera za vijana wa CCM ambao kutokana na maneno ya Lusinde wanaonesha uhuni na umalaya kutokana na fumanizi la Mchemba?

Leo hatutaandika mengi zaidi ya kuhitimisha kwa kusema kuwa: kwa maneno yake Lusinde, Mbunge wa Mtera, amethibitisha yametuchanganya kushindwa kumuweka kwenye kundi la wahuni na washamba wa siasa wanaopaswa kupelekwa jando au unyago wa kisiasa haraka sana ili kuona mwanga.
Chanzo: Tanzania Daima Septemba 28, 2011.

No comments: