The Chant of Savant

Friday 2 September 2011

Jambazi anapojilinganisha na Yesu!

Ni muda mrefu tangu kijiwe kikutane kujadili mambo mbali mbali. Hii ni kutokana na wajumbe wetu kusambaa sehemu mbali mbali duniani kusaidia ukombozi wa nchi mbali mbali. Hivi karibuni mwenyekiti nilikuwa kwa mama kuwahamasisha vijana wampindue maana anakula bure na kulala bure yeye na ukoo wake.

Msomi Mkatatamaa alikuwa Masri ambako tulikwenda pamoja na kumpindua Huseni Kibaraka. Kwenye msafara huu nami nilikuwapo kabla ya kuondoka mwezi Mei kwenda zangu AbortAbad kwenda kumkamata Msama bin Burden ambaye tulimnyotoa roho. Kumbuka mimi ni SEAL ingawa hii ni top secret. Hivyo, unaposoma usome kwa sauti ya chini ili watu wasikusikie hasa mafisadi wakakimbia kwa kujua ninawatafuta.

Pamoja na kwamba baadhi ya wajumbe wetu wako kule Libya ambapo Mlamali Kashafi tumeishamwangusha, kijiwe kitaendelea bila wao kuwepo. Kwa taarifa nilizo nazo ni kwamba Msomi mkatatamaa yumo mjini Cairo kusaidia utawala mpya wa Libya kuunda serikali mpya. Yeye ndiye mshauri mkuu anayeniwakilisha mwenyekiti.

Kikao cha leo cha kijiwe ni kujadili na kumlaani Devil Jaa Hilo aliyenakiriwa hivi karibuni akijilinganisha na Yesu mtoto wa Maria. Hivyo mjadala wa leo pamoja na kuegemea kwenye ufisadi na usanii wa Njaa Kaya, kitaangalia mambo mbali mbali hasa wakati huu ambapo kaya iko kizani huku mapanya yakiendelea kuiguguna kama alivyonaswa Jaa Hilo akitaka kufanya kwa kisingizio eti cha kuwahonga waishiwa. Huyu naye anafikiri kwa masaburi au makali kwa wale wasiojua msamiati mpya wa masaburi. Ikumbukwe. Hapa hatumaanishi yule jambazi Masampuri aliyewatukana waishiwa kuwa wanafikiri kwa makario.

Baada ya kukutana baada ya muda mrefu, tunapata kahawa haraka haraka kukazia swaumu zetu na kuanza shughuli.

Mbwamwitu analianzisha aningia akiimba wimbo wake aupendao sana.

Anaimba,

Watu wa dunia hii mie wamenishinda,
Wakiingia kanisani wanahubiri na kuimba sana,
Wakitoka nje wanakwenda uza miunga.
Wakiingia ofisini wanajisifu na kuiba sana,
Wakitolewa wanaanza kusema eti wao ni Yesu,
Mambo mambo mambo
Mambooo mambo mambo, mambo yamenishinda.

Baada ya kumaliza kuimba wimbo wake alioanza kuuimba alipomaliza kusoma habari inayomhusu Jaa Hilo na Ruhani Njoo, anampasia gazeti Mchunguliaji, Mbwamwitu anakwanyua mic na kuzoza.

“Waheshimiwa wajumbe, leo nina hasira sana. Hasira zangu zimesababishwa na kuona jambazi mmoja mwenye maulaji eti akijilinganisha na Yesu baada ya nduguye na fisadi mwenzie aitwaye Phil Ruhani Njoo kusaliti ofisi yake na yule aliyempa ulaji bila kufikiri asijue ni jizi.”

Kabla ya Mbwamwitu kuendelea kunema, mzee Maneno anaingilia, “We unaongelea Ruhani Njoo na Jaa Hilo badala ya wale mahabithi wawili yaani Bill Ngelanija na mtoto wa Adimu Milima ya Kigoma ambao Njaa Kaya anajitahidi kuwaokoa!”

Mzee Maneno anamkabidhi kipisi cha sigara kali mzee Ndevu na kuendelea, “Hapa bila walevi kushinikiza mahabithi wote wanne wasulubiwe utakuwa ni usanii na usaliti kama kawaida. Wanakaya tutaendelea kuliwa.”

Mara miguno inasikika huku mzee Ndevu akisema, “Astaghafullahi eti tunaliwa! Matusi hayo mzee Maneno pia chunga maneno yako.”

Mzee Maneno haombi msamaha anaendelea, “Ndiyo tunaliwa. Sasa tunaliwa vipi msiniulize. Kama tusingekuwa tunaliwa si tungekwenda huko maofisini na kuwachoma hawa majambazi lau kwa kahawa.”

Kila mmoja ananyamaza kidogo kusukuti aliyesema mzee Maneno. Ni kijembe babu kubwa.

Tukiwa wote tunafikiri jinsi ya kumjibu, Mbwamwitu ambaye ana unywanywa wa kuongea hasa ikizingatiwa kuwa aliingiliwa na mzee Maneno anakula mic. “Waheshimiwa sana. Mzee Maneno kasema ukweli. Tena amefikiri kwa ubongo na si masaburi. Ametonesha donda ili waathirika tuumie na kuamka na kujihami. “

Anakunywa kahawa yake na kukatua kashata na kuendelea, “Mie narudia, mnaliwa.”

Kabla ya kumaliza, Mchunguliaji hajivungi, anamnyang’anya mic na kujibu, “Kama kuliwa unaliwa wewe na hao akina Njaa Kaya, Ruhani Njoo, Jaa Hilo, Milima ya Kigoma na Ngelanija na wenzake. Kwani hatujui kuwa wanatumiwa na mabwana zao watokao ughaibuni kuja kuchukua kwa kujifanya wanawekeza?”

Akiwa anatweta Mchunguliaji anaendelea. “Mie siliwi na kama kuna anayetaka kuliwa aliwe mwenyewe siyo mimi.”

Mpemba kaguswa pabaya. Anaingilia kwa ulaini kabisa kutokana na Mchunguliaji kunyamaza ili kuona ujumbe wake umefikaje. Mpemba anasema, “Yakhe kwani kuliwa tusiii? Mbona kama kuliwa wote twaliwa! Wala kodi zetu, wachangishana pesa yetu kupitisha upuuzi na wizi wao. Je huku si kuliwa jamani?”

Kabla ya swali lake kujibiwa, Mgosi Machungi anachip in, “Mgoshi kama kujigh’wa ni kuibiwa basi nao wanajigh’wa. Mie aiposema kujigh’wa niizani yale mambo ya kwenu ya popobawa.”

Kabla ya Mgosi kuendelea Mpemba anaingilia, “Yakhe hayo mambo ya popobawa yalikuwa ya Chama Cha Makafiri na Salimuni Amri yule kidhabu aliyetaka kututesa kwa vile eti tu wapemba.”

Mpemba anaendelea, “Mie naona hata hao akina Ruhani Njoo, Jaa Hilo, Ngeleza na Milima ya sijui Kigoma sijui Ujiji sijui Maneromango ndiyo mapopobawa wenyewe wanaokula pesa yetu. Mie nanchukia huyu ruhani haswa nkizingatia maruhani walivotuibia kura kule Zanzibar. Sasa waiba pesa nchi nzima ati. Hawa ni majambazi yatumiayo kalamu kuwaibia wanakaaaya wallahi.”

‘Wanakaya siyo wanakaaya. Hujui wanakaaya ni wavuta bangi Ami?” Anatania Mbwamwitu.

Mwenyekiti nami sitaki kuonekana kihiyo au mwoga kama Njaa Kaya. Nakula mic. “ Jaa Hilo ambaye ni jaa kweli hivi karibuni alitoa mpya alipofanya makufuru ya makufuru kwa kujilinganisha na Yesu pale jambazi mwenzie alipomwokoa kutokana na kashfa yake ya ujambazi na kuwasingizia waishiwa wabuge. Mie nasema, Jaa Hilo si Yesu bali Yuda atake asitake. Kusum ibn al muthnaka.”

Nabwia kahawa kidogo na kuangalia huku na kule na kuendelea. “Sasa nasema. Nenda kawambie wote kuwa nitawapindua kama nilivyowapindua akina Kibaraka, Kashafi, Bin Ali au kuwajeruhi kama tulivyomfanyia yule habithi wa Yamani Salehe.”

Wajumbe hawana mbavu kutokana na ninavyoongea kwa mamlaka na kujijazia ujiko.

Naendelea, “Njaa kaya na hao nyani wake hana jipya hata kama amejifanya kufuta uamuzi wa habithi Ruhani Njoo. Msitu ni ule ule na nyani ni wale wale. Hivyo hata huo uchunguzi tuliokuwa tumeambiwa ni usanii na utoto wa kawaida uliokuwa ukifanywa na watu wazima kimwili lakini watoto kiakili.”

Naona ndata wanakaribia, hivyo kila mtu atimke kivyake tukikutana tena tuwatokee hao majambazi na kuwaangukia kipopo.

Jaa-hilo na Ruhani-njoo mnanipata? Kumbaff sana.

Chanzo: Tanzania Daima Agosti 31, 2001.


No comments: