The Chant of Savant

Wednesday 3 August 2011

Watawala wezi wafuatilie kinachoendelea Misri


Leo ni siku iliyongojewa sana na wamisri. Wamisri wana hamu sana ya kumuona mwizi na imla wao wa zamani Hosni Mubarak, mkewe na wanae wakisimamishwa kizimbani kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa hili. Hata kama ataachiwa kutokana na ukweli kuwa serikali inayomfikisha mahakamani imeundwa na vibaraka wake, ni pigo kwa mtu aliyejiona muungu mtu kufikishwa kizimbani na kunyea debe. Ni aibu kiasi gani kwa mtu aliyeitawala nchi kwa zaidi ya miongo mitatu kuletwa mahakani akiwa kwenye nguo za kulalia amelala kitandani? Hii ni mara ya kwanza kwa wamisri kumuona aliyekuwa kijogoo wao akiwa amelala kitandani kizimbani.

Nachukua fursa hii kumtaka rais wangu Jakaya Kikwete kufuatilia zoezi hili ili ajipime yeye na familia yake wako salama au hatarini kiasi gani.

Je watawala wetu wezi wanapata somo gani kuhusiana na hali hii? Watawala wezi wanaotumia wake na watoto wao kuibia umma wanapaswa kutia akilini kuwa mambo yanabadilika. Bado zamu yao ambalo ni suala la muda tu. Nani alijua kuwa Mubarak imla aliyetisha kwa kuwa na mashushu karibu kila eneo na nyanja ya maisha ya wamisri angeporomoka kama dongo? Hayawi hayawi huwa. Tunashuhudia maimla kule Malawi, Senagal, Uganda,Congo Brazza na kwingineko wakitaka kuwarithisha ima watoto au ndugu zao urais kana kwamba ni mali ya ukoo. Tunashuhudia vyama vya kijambazi vikipandikiza vilaza wao wawe marais ili waibe na kuwalinda waliowatengeneza. Je wakati wa Afrika kuchukua hatua umefika? Ngoja tuone kitakachotokea baada ya Mubarak kusimama kizimbani. Mungu ibariki Afrika.Kwa habari zaidi juu ya yaliyojiri mahakamani BONYEZA HAPA

1 comment:

malkiory matiya said...

Za mwizi ni arobaini tu,sijui mali walizojilimbikizia wataenda kuzificha wapi. Tufanya uchunguzi wa hali na mali hadi zile walizoficha nje ya nchi lazima tujue.