The Chant of Savant

Tuesday 2 August 2011

Nani aliokoe bunge letu?



Hali ya afya na udhu wa bunge letu la sasa ni vya kutia shaka. Lazima wajitokeze watu jasiri na wenye mapenzi na taifa lao walikemee hili bila woga wala kuchelea lolote.

Rais wa zamani wa Zambia Dk Kenneth Kaunda aliwaambia wazambia kuwa watamkumbuka na wasimpate tena. Hii ni baada ya kushindwa kwenye uchaguzi uliomtupa nje ya madaraka baada ya kutumikia nchi hiyo kwa zaidi ya miongo miwili. Kaunda aliyesema haya kwa kujua ambacho kingetokea baada ya wazambia kumchagua rais wa zamani wa nchi hiyo marehemu Fredrick Chiluba.

Ingawa spika wa zamani wa bunge la Tanzania Samuel Sitta al maarufu mzee wa viwango hakusema aliyosema Kaunda, alipaswa kusema hivyo. Hata hivyo historia ni shahidi. Sitta alipatilizwa kutokana na kutenda haki kwa wananchi kwa kufichua na kuushughulikia vilivyo ufisadi wa Richmond ambao ulimjengea chuki na wakubwa wenye kuhusika na uchafu huu.

Hakuna ubishi kuwa bunge letu sasa limeingiliwa na siasa za kizamani, kuburuzana, ubabe hata kutenda yasiyopaswa kutendwa na watu wazima wenye hadhi husika.Waingereza wana msemo; show me your friends I will tell you who you are yaani nionyeshe marafiki zako nitwambia wewe ni nani. Je Spika wetu ni nani? Historia yake ina utata au tuseme haieleweki wengi hawajui yeye ni nani, mke wa nani na ana taaluma gani. Ukienda kwenye wavuti wake wa Wikipedia unakuta maelezo kiduchu kama yafuatavyo:

Anna Semamba Makinda (amezaliwa tar. 15 Julai 1949) ni mbunge wa jimbo la Njombe Kusini katika bunge la kitaifa nchini Tanzania. Pia alikuwa Naibu Spika wa Bunge tangu 2006 hadi 2010. Kwa sasa ndiye Spika wa Bunge la Tanzania. Mwaka wa 1990 na 1995 alikuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto. Pia miaka ya nyuma alishawahi kushika nyandhifa kadha wa kadha.

Kwanini anaficha historia yake kama haina dosari? Yeye ni kiongozi wa umma anayepaswa kuweka kila kitu wazi ili umma umjue kumkosoa hata kumpongeza inapobidi. Japo mambo ya familia yanaweza kupuuzwa, ukweli ni mambo muhimu. Maana kwa kujua hadhi ya kifamilia ya mhusika inakuwa rahisi kumtathimini.

Wengi wanaweza kusema eti anasakamwa kwa vile ni mwanamke. Hasha. Tuna nchi mbili kwenye jumuia ya Afrika Mashariki ambazo maspika wa mabunge yao ni wanawake lakini wenye kufanya vizuri kutokana na kuwa wanasheria kitaaluma. Hawa ni Nyakuhabwa Mukantabama Rose (Rwanda)

Na Rebecca Kadaga (Uganda). Ingawa spika wa bunge la Kenya ni mwanamme bado ni mwanasheria Kenneth Marende. Kwanini wenzetu wameona busara ya taaluma kwenye nafasi hii nyeti ya kutunga sheria wakati sisi tukiendekeza maslahi uchwara ya makundi? Je wahusika walitumia udhaifu wa mteule wao ili iwe rahisi kumtumia kupitisha mambo yao au iwe rahisi kwake kuvunja sheria na kuzuia wabaya wao? Maswali ni mengi kuliko majibu.

Kwa wanaokumbuka mizengwe na patilizi vilivyotumika kumzuia Sitta na kumsimika Makinda spika wa sasa, watakuwa wanajua tunachomaanisha. Sitta hakutendewa haki ingawa aliutendea umma na bunge haki. Hili halitafutika katika historia ya bunge la Tanzania. Hakika, ukiona tabia za mtoto waweza kujua tabia za wazazi wake. Pia ni ukweli kuwa sifa na vigezo vilivyotumika kumpata Makinda ni vya hovyo. Maana kigezo kikubwa kilichotumika ni hali ya kuwa mwanamke. Huu, licha ya kuwa udhalilishaji wa kuonyesha wanawake wanabebwa, ni ubaguzi wa kijinsia hata kama utapambwa vipi. Kwa vigezo duni kama hivi ni rahisi kuamini kuwa Makinda alipachikwa pale alipo kulinda maslahi ya kundi fulani lenye kutia shaka.

Kwa kuzingatia hilo hapo juu, hata kilichowapata wabunge Godbless Lema (CHADEMA-Arusha Mjini), Mchungaji Peter Msingwa (CHADEMA-Iringa Mjini) na Tundu Lissu (CHADEMA-Singida Mashariki) kinaweza kusema zaidi ya tunavyoweza kueleza. Kwanini wabunge wote ni wa CHADEMA? Jibu ni rahisi. Ndicho chama tishio kwa serikali ya sasa. Ndicho chama ambacho kinasifika kufichua kashfa na uoza mwingine kuliko vyama vingine. Ndicho chama kilichojitofautisha na CCM kisera na kimkakati.

Turejee kwaMakinda, ingawa alichaguliwa kwa taratibu za bunge baada ya kupatikana kwa kupindisha taratibu na mazoea ya chama, bado hawezi kukimbia lawama kuwa alipatikana kutokana na rafu aliyochezewa Sitta baada ya kulijengea bunge heshima kubwa kwa kipindi kimoja alichotumikia kama spika.

Chama Cha Mapinduzi wana utaratibu ambao umegeuka kuwa kama sheria wa kuruhusu mwenye kushika wadhifa fulani kutumikia vipindi viwili. Tuliona hili kule Zanzibar wakati makamu wa rais wa sasa Dk Gharib Bilal alipotaka kupambana na rais wa zamani wa Zanzibar Amani Abeid Karume alipokuwa akigombea kipindi cha pili cha urais wake. Hata rais mstaafu Benjamin Mkapa aliwahi kuzuia watu kuchukua fomu kumpinga kutokana na utaratibu huu wa kumaliza ngwe mbili. Nani mara hii amemsahau wapinzani wa Mkapa waliioshushwa kwenye treni Tabora? Hata rais Kikwete alipokuwa akigombea ngwe ya pili alipata mpinzania John Shibuda ambaye alilaaniwa na wana CCM wengi kutokana na kutaka kuvunja utaratibu huu.

Mifano ya kuachiana ngwe ni mingi. Kwa hiyo michache hapo juu tunaweza kuendelea na hoja yetu kuwa alivyopatikana Makinda ni ushahidi tosha wa yale anayotenda akiwa alitumwa rasmi kuyatenda.

Kimsingi, spika anapaswa kuwa mtumishi wa wabunge na si kuwafanya wabunge watumishi wake. Hivi spika anamwakilisha nani zaidi ya wananchi? Ila kwa spika wa sasa inatia shaka kama kweli anawakilisha wananchi zaidi ya wale waliomchomoa huko walikomchomoa na kumsimika hapo alipo.

Wabungwe ni wawakilishi wa wananchi na ndiyo maana wanalipwa mishahara na marupurupu makubwa kwa kazi hii. Spika asiyetumbua na kutekeleza hili hatufai katika karne hii ya mapambano ya kupanua haki na uhuru wa wananchi. Spika ambaye anaonekana kuwa kikwazo anatufanya tukumbuke hata bunge la chama kimoja ambalo kwa kiasi fulani lilikuwa likifuata sheria kuliko la sasa kutokana na kuendeshwa na mtu asiye na chembe ya taaluma ya sheria. Chifu Adam Sapi angefufuka leo angetaka arejee uspika ili kulinusuru bunge. Maana hata wakati wa chama kimoja bunge lilikuwa na maana kuliko sasa ambapo kikundi cha watu wenye ajenda zao za siri kimetubambikizia spika ili kulinda maslahi yake. Nani mara hii amesahau wabunge Machachari kama Tumtemeke Sanga, Stephen Nandonde na wengine wengi waliolitingisha bunge kwa hoja moto moto zilizolenga kuikosoa serikali?

Tuhitimishe kwa kutoa wito kuwa wakati wa kumkagua na kumwajibisha spika wa bunge na naibu wake umefika. Vinginevyo watu hawa watalipeleka taifa pabaya kutokana na maamuzi yao ya kutia shaka. Bunge letu liko msambweni. Nani aliokoe zaidi ya wananchi wakishikamana na wabunge wao?

Chanzo: Dira ya Mtanzania Agosti 1, 2011.

No comments: