The Chant of Savant

Tuesday 26 July 2011

Mwanzo wa ndoa ya Maalim Seif kuvunjika?

Maneno ya katibu wa Fedha na Uchumi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mwigulu Nchemba alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Tegeta hayawezi kupita bila kudurusiwa. Nchemba alikariria na vyombo vya habari mnamo jumanne, 19 julai 2011 akisema, “…Mnakumbuka kule Zanzibar walikufa watu 27 lakini leo Maalim Seif yuko Ikulu na ndevu zake amenyoa, ananawiri tu; je, waliokufa wamefaidika nini…?”

Wengi wanaojua: harakati binafsi za kisiasa za Seif Sharrif Hamad tangu CCM, kuasi na kufungwa hadi kuanzisha chama chake cha CUF na hatimaye kujirejesha CCM wanaweza kukubaliana na maneno ya Nchemba. Kadhalika, wengine wasiomfahamu Hamad vizuri kwa awamu zote alizokuwa serikalini, gerezani, upinzani na sasa serikalini tena wanaweza kubisha. Kwa wanaojua kuwa CUF ni Sharrif na Sharrif ni CUF, hawana shaka na aliyosema Nchemba.

Wanaokubaliana na Nchemba wanaweza kuwa sahihi kutokana na sababu zifuatazo:
Kwanza, CCM wanamjua Shariff vizuri kwa vile alikuwa mwenzao mwanzo akawakimbia, wakamtia adabu na akarejea ili afaidi ulaji nao.

Pili, aliyosema yana ukweli kwa kiwango kikubwa kutokana na Shariff mwenyewe kutokanusha yaliporipotiwa. Si Shariff, ofisi yake hata chama chake waliokanusha maneno ya Nchemba kiasi cha kuyapa uzito na ukweli.

Je ni nini alichosema Nchemba? Kwa ufupi Nchemba aliongelea unafiki, ulafi na usanii vilivyofanywa na Hamad kwa kuwatumia wazanzibari hadi wakamwaga damu ili yeye ale kama anavyofanya sasa chini ya kisingizio cha serikali ya umoja wa kitaifa na kuleta mshikamano Zanzibar. Pia Nchemba aliweka wazi kuwa chama chake kiliua watu kule Zanzibar tofauti na wenzake waliokuwa wakikanusha au kukwepa kuzungumzia mauaji haya ya kinyama yaliyosababishwa na CCM NA Hamad. Maana ukiangalila anachoongelea Nchemba na kinachoendelea unaona ukweli kwa kiasi kikubwa. Kuna baadhi ya maswali ambayo hadi kesho hayajawahi kupewa majibu yanayoingia akilini. Hivi kweli Shariff ameleta mshikamano wa wazanzibari au mshikamano wake na CCM? Hivi umakamu wa rais wa Shariff unawasaidia nini wale aliowahi kuwashawishi wakaingia mkenge na kuandamana hadi wakauawa au kupoteza viungo? Je hili la kutupiwa umakamu wa rais ndilo walilokuwa wakifia wazanzibari?

Sitaki mtu aniambie kuwa alichofanya Shariff ni sawa na walichofanya akina Morgan Tvangirai waziri mkuu wa Zimbabwe au mwenzake wa Kenya Raila Odinga. Wao walishinikizwa na jumuia ya kimataifa wakaunda serikali kwa kugawana madaraka. Ukiangalia Zanzibar, baada ya seif kupewa umakamu wa rais ndiyo ikawa imetoka ukiachia mbali kupewa nafasi mbili za uwaziri. Odinga na Tvangirai wamo kwenye serikali ya umoja wa kitaifa wakisimama kidete kupigania maslahi ya wananchi na vyama vyao na si kugeuzwa nyumba ndogo kama ilivyo hapa kwetu.

Kimsingi, kwa maneno ya Nchemba, alichofanya Shariff ni usaliti wa kawaida ingawa CUF na Hamad wenyewe hawataki kukubali ukweli huu. Ukiangalia maneno ya Nchemba na nafasi yake katika chama chake, unagundua kuwa CCM wanajua fika Shariff alivyofanya usaliti kwa tamaa ya madaraka. Hili halina mjadala na yaweza kudhaniwa ndiyo maana Shariff hakukanusha.

Wengi wanaweza kuchukulia maneno ya Nchemba kirahisi na kudhani ni mawazo yake binafsi na si msimamo wa chama. Je Nchemba katumwa na wakubwa zake ampe ukweli wake Shariff? Je hizi ni dalili za CCM kuanza kumchoka na hatimaye kumtosa Shariff? Wenya akili wanajiuliza nini kitafuatia baada ya muhula huu kuishi na Zanzibar kwenda kwenye uchaguzi. Shariff atawambia nini wazanzibari baada ya kumalizika muhula huu? Kimsingi, alichofanya na kumaanisha Nchemba ni kwamba kama Hamad na wenye mawazo kama yao wanaokula CCM wataendelea na kidomo domo wajue wanaweza kushughulikiwa bado. Kimsingi Nchemba alikuwa akimkumbusha Hamad usaliti wake na hivyo kuhakikisha anaishi kwenye nyumba ya vioo na hivyo asitupe mawe. Tangu kufungwa kwa kile watani wa Shariff huita ndoa hii ya mkeka, faraja pekee ya Shariff ni kelele za Zanzibar kutaka iwe na mamlaka zaidi kwenye muungano. Hii, kimsingi, ndiyo hoja fichi ya Shariff na wanzanzibari wengi waaminio kuwa muungano unawanyima uhuru. Hata hivyo, nje ya muungano Zanzibar itakuwa kama Comoro na isitoshe hawa waliopo madarakani wanalijua hili na hawako tayari kuona muungano ukiuawa.

Swali la Nchemba ni fupi lakini zito na lenye ujumbe mzito sana. Hebu tulirejee. “…Mnakumbuka kule Zanzibar walikufa watu 27 lakini leo Maalim Seif yuko Ikulu na ndevu zake amenyoa, ananawiri tu; je, waliokufa wamefaidika nini…?” Pamoja na kuonekana kumgusa Hamad binafsi, ni ukweli usiopingika kuwa tangu Hamad agawiwe umakamu rais amenawiri na ndevu zake zimepunguzwa. Je wale waliopoteza maisha wamefaidika nini? Jibu la swali hili si rahisi ingawa Nchemba anajaribu kujenga mazingira ya kulipatia jibu. Hata kwa kukangalia maneno ya Nchemba bado hatuwezi kupata jibu sahihi. Maana hatujui wanavyojisikia wale waliopoteza ndugu zao au mali na hata viungo vyao. Je wataendelea kutekwa nyara kwa lugha tamu za makubaliano huku damu zao ama ndugu zao zikiishia kuneemesha kitumbua cha watu wachache waroho waliowahadaa? Ni suala la muda ukweli kufumka na wahusika kujikuta wakizomewa hata kuadhibiwa na historia.

Nchemba anajua wazi kuwa kilichosilimisha Hamad si kingine bali njaa. Anajua fika Hamad asivyo na tofauti na wanasiasa wengine walioamua kujirejesha CCM kinyume nyume kama vile Augustine Mrema, Masumbuko Lamawai, Warid Kaboro, Thomas Ngawaiya, Tambwe Hiza, Shaib Akwilombe, Dk Masha, Stephen Wassira na wengine wengi ambao wanafanya siasa za matumbo kama Hamad.

Je mwanzo wa ndoa ya mkeka baina ya CCM na maalim Seif ndiyo unaanza? Maana inapotokea wale wanaojiona watu wazima kuanza kurushiwa vijembe na matusi ya wazi na watoto wa jana kiumri na kisiasa huku wakubwa wakijifanya kutohusika jua kuna jambo.

Kama Shariff na CUF walikuwa wakidai waliibiwa ushindi mar azote, kama ni kweli, ilikuwaje wakakubali cheo cha kutupiwa tena kwa baadhi ya wakuu wa chama huku umma ukiendelea kuteseka kama awali?
Chanzo: Dira ya Mtanzania Julai 26, 2011.

No comments: