The Chant of Savant

Wednesday 20 July 2011

Maisha Magumu, nani aliwaroga Watanzania?

HAKUNA ubishi kuwa hali za maisha nchini Tanzania sawa na majirani zake ni mbaya. Kuna uhaba wa chakula na kupanda kwa gharama za maisha kwa ujumla. Nchini Kenya tumeishashuhudia mshike mshike baina ya serikali na wananchi wanaoshinikiza watawala kukidhi matakwa ya umma kama walivyowaahidi kwenye uchaguzi.

Nchini Uganda bado hakieleweki ingawa imla wa nchi hiyo ameendelea kujifanya hamnazo. Nchini Malawi mapambano yameripotiwa jana ambapo mtu mmoja aliuawa na wengine wengi kujeruhiwa kwenye maandamano ya kupinga utawala wa Bingu wa Mutharika kutokana na kupanda gharama za maisha. Tanzania tuna hali ngumu kuliko wote kutokana na kuendelea kukaa kizani kama mende kwa muongo mzima. Je nani alituroga kiasi cha kuwa mashahidi wa mateso yetu wakati wengine wanaamua kuingia mitaani? Nani alidhani kuwa wamalawi waliozoea kuhenyeshwa na uimla wa Banda wangejitambua na kuleta mageuzi makubwa ya kupigiwa mfano?

Wakati wenzetu wakiionyesha dunia walivyo na akili sawa sawa sisi tunawashinda kwenye ushirikina kama ilivyoripotiwa hivi karibuni na shirika la habari la Uingereza BBC bila serikali yetu hata kupinga. Ni aibu namna gani.
Leo hii watanzania wamegeuka hamnazo kiasi cha kuwavumilia hata mawaziri wanaopitisha bajeti kwa kuhonga wabunge! Tunawavumilia wabunge wala rushwa na wanaojilipa posho kwa kuuchapa usingizi na kuongea umbea! Je nani alituroga? Tuguswe wapi ndiyo tuamke? Je hii haimaanishi kuwa watanzania karibu wote ni mafisadi kila mtu kwa nafasi yake?
Kwa yaliyojiri Malawi BONYEZA HAPA na HAPA.

1 comment:

Anonymous said...

Ni kweli kabisa watanzania tunajua kulalamika pembeni lakini tukikutana na viongozi wenyewe tunanywea. Tunajua wazi kabisa mambo yanayotokea na hali mbaya ya uchumi lakini hakuna anayesema chochote.Bei za vitu zinapanda hakuna viongozi vilaza wapo kimya;kwa kuwa wanamudu maisha kwa kujilipa mishahara minono. Wakati watu wa kawaida hata mlo mmoja unawashinda kumudu. Inabidi tuamke sasa kwa kujifunza mambo ambayo anayotokea. Naamini kuwa watu wanaelewa na kuyaona mabaya ya viongozi wetu; ila wanapuuza. Ni wachache wanaotilia maanani sijui ni uoga ndio unaotusumbua. Au wengine wanauwezo wa kuelimisha jamii kwa kalamu zao instead wanapotosha baada ya kupewa kitu kidogo.