The Chant of Savant

Wednesday 11 May 2011

Hawa si wachungaji bali ni fisi na mbwa mwitu

KUMEZUKA mtindo mchafu na wa rejareja wa baadhi ya wachumia tumbo na matapeli kumtania hata kumtumia Mwenyezi Mungu kufanya utapeli na ujambazi wao. Viumbe hawa wachafu kama uchafu wao hawana hata aibu.

Kwa wanaosoma magazeti vizuri wanawajua kwa majina wachumia tumbo waliovaa majoho ya kiroho wenye uroho. Hapa lazima tuelewane. Ninaposema magazeti namaanisha magazetisi yale ya kifisadi ambayo yamejaza mikanjanja inayotumika kama nepi.

Pia simaanisha magazeti yaliyonunuliwa kwa pesa ya HEPA. Na yale ya kiama yanayounga mkono kila upuuzi kama yale ya utumwa (kinyume), mamluki (kinyume), fumba macho (kinyume), Mbongo na mengine mengi ya mifukoni.

Hata ninaposema runinga simaanishi zile za kifisadi na kibubusa kama vile BCT, VTV, NTC na nyingine nyingi ambazo ni zana za ufisadi.

Matapeli hawa wa kiroho wamejaa roho mtakakitu na mchafu chini ya kisingizio cha roho mtakatifu. Hawa si wachungaji bali fisi na mbwa mwitu wawararuao watu wa Mungu.

Hawa walafu hawana tofauti na wale mbwa mwitu aliotahadharisha Bwana Yesu. Hawa jamaa hawana Mungu zaidi ya matumbo yao na mafisadi. Hawana dini zaidi ya ufisadi na utapeli.

Matapeli hawa waliojivisha vyeo vikubwa na vitukufu kama uaskofu, uchungaji hata uijilisti, wameanza kuwa tishio na kero. Ni wa kuogopwa kuliko hata ukimwi na ukoma. Wamekuwa wakiwaibia watu maskini, wajinga na wenye matatizo kwa njia ya kudai sadaka na kula wao na kutajirika.

Wengine walipoona biashara zao za wizi wa sadaka hazitoshi, sasa wameamua kutafuta mbinu nyingine chafu zaidi ya kuongeza wafuasi ili sadaka iongezeke. Wanahubiri tumtolee Bwana wakati hakuna cha bwana wala bibi bali matumbo yao. Walibuni utapeli na sanaa ya kuomba na kufanya miujiza.

Kwani hamuowani kwenye runinga na kwenye hata magazeti na radio wakitangaza uchangudoa wao wauitao kuomba na kufanya miujiza. Kama wanaweza kutenda muujiza lau mmoja si mwingine bali kuwaibia walevi maskini wa Bongolalaland.

Kwa kula na kuiba sadaka hawajatosheka. Sasa wameanza kujipendekeza kwa mafisadi. Wamekuwa wakisikika wakiomba eti amani bila kukemea ufisi na ufisadi. Wamekuwa wakishambulia watu wanaofikiri sawa sawa wanaosema mfalme yuko uchi. Je, hawa ni nini zaidi ya kuwa chui kwenye gamba la kondoo?

Hawa nao wanapaswa kujivua magwanda au tuseme gamba. Niwajuavyo viumbe hawa laanifu hawawezi kujivua gamba. Ni jukumu la farasi wanaowabeba yaani walevi kuwavua gamba.

Ndiyo, wanafaa wavuliwe majoho na hatimaye magamba. Tusiwaruhusu watuombee na kutuomba bali tuwaombee na kuwaumbua. Maana nijuavyo, hivi karibuni mtawasikia wengi kama chiriku wakiimba nyimbo kwenye kambi mbili.

Wapo watakaomuunga mkono Mkuu wa Kijiwe kwenye kila upuuzi atakaoufanya. Pia wapo watakaomuunga mkono Ewassa ili kumsafisha. Katika makundi yote haya mawili hakuna mwenye nia ya kuunga mkono bali kuwatumia mafisadi hawa wakuu kujineemesha.

Niwape kisa kimoja ili mkumbuke na kujua viumbe hawa laanifu walivyo. Mnakumbuka mmoja wa waganga njaa hawa watumiao jina la Mungu aitwaye Zakkie Ka-tortoise alivyomsifia Mkuu wa Kaya kuwa ni mpole sana wakati akitetea genge lake la biashara lisipitiwe na mitambo ya unishati?

Kutokana na elimu na busara haba, jamaa alidhani akijipendekeza na kumsifu, angemtetea asijue naye ni kama yeye kwenye suala zima la usanii. Baada ya Mkuu kutoingia mkenge nadhani mnakumbuka jamaa alivyomgeuka na kumshambulia si kawaida.

Jamaa huyu aligufu na kudhani kuwa Mkuu wa Kaya ni kama Lyatongolwa ambaye akihadaiwa kidogo huchemka na kutoboa kila siri. Japo naye ni tapeli lakini hamfikii mkuu wetu kijiweni. Hakujua kuwa Lyatongolwa ni tapeli na kihiyo kama yeye. Angejua kuwa mkuu ni zaidi kwenye sanaa hii asingepoteza muda kwa kujipa matumaini yaliyoishia kuwa kilio na aibu.

Juzi nilimsikia fisidini Godfala Muhogo-lolo akihanikiza kujikomba na kujiuza kama changu kwa Njaa. Pia hata Mozes Kuloa naye nilimsikia akijinadi gulioni kwa mafisadi. Mzee huyu anatia huruma. Alianza kuwatapeli watu kuwa anatenda miujiza. Baada ya kumshtukia aliwamba ile mbaya na sasa ameibuka na uchangudoa wa kiroho na kisiasa. Hata Chris Mtikisa msimwamini. Murongo huyo hana lolote bali njaa na kujikomba. Anarusha makombora ili aandikiwe cheki na azame na kutuguna na akiishiwa arejee.

Inashangaza sana. “Askofu” mzima unajikomba kwa wezi tena wanaosababisha mauaji ya halaiki. Sorry sina haja ya kukulaumu. Maana wewe si askofu bali askopo au tuseme muasipofu. Ajabu maaskofu hawa wa kujipachika hata hawaoni aibu tunavyowavumilia kwa uaskofu wao wa kujipachika!

Kuna vijiaskofu uchwara vingi vilivyojipachika uaskofu vinavyoibuka kila uchao vikijifanya vinamtetea mkuu ili avitupie mabaki. Viogopeni na vizodoe na kuvifichua vijue mambo vinayofanya ni kinyaa kwenu.

Siku hizi hawa maaskufuru wa kujipachika wamekuwa kama waganga wa kienyeji. Hamkuwasikia wengi wakipambana na babu wa Loliyondo baada ya kuwafunika kwa ujiko na mihela? Wote lao moja. Wangetaka nao wawapate kama babu alivyowapata hadi wazito kiasi cha kugeuka serikali ndani ya serikali.

Wanajikomba kwa kila mtawala bila kujali miiko ya nafasi walizodandia. Hata hivyo huwezi kuwashangaa sana kutokana na ukweli kuwa wao si watumishi wa Mungu bali muungu-mali na madaraka.

Zamani dini zilikuwa zinaheshimika kabla ya kuibuka kwa maaskufuru na mashehena kiasi cha kuzifanya ziwe biashara na ugaidi wa kawaida.

Bad news ni kwamba mzee mzima nilinusurika kurejesha namba mnamo tarehe sita mwezi huu kutokana na mtambo wangu kupinduka nilipokuwa nakwenda kumpa hongera Obama kwa kumnyotoa Osami bin Burden. Nitaongea kwa kirefu wiki ijayo.

Yule changu namkumbuka. Niliwahi kufaidi ulodi wake na kugoma kulipa fadhila. Ngoja nijikate asijenitoa jasho bure watu wakajua kuwa nasi wakubwa ni waasharati.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 11, 2011.

No comments: