The Chant of Savant

Tuesday 19 April 2011

CCM imejivua gamba lipi? sehemu ya pili

Hakuna ubishi. Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaendelea kulewa sifa kwa kusema chama chao kimeamua kubadilika. Utasikia viongozi wao wakizidi kuuhadaa umma kuwa wamejivua gamba wakati siyo.

Siku za hivi karibuni kama si salamu za pongezi kwa mwenyekiti utaona maandamano ya kumuunga mkono kwa kukivua chama gamba! Je, kweli CCM imejivua gamba?

Kwa wanaokumbuka kituko kilichoteka hivi karibuni kwenye vikao vya CCM vilivyokwisha mjini Dodoma, watakumbuka mzengwe mmoja. Zengwe hili si jingine bali kudai eti katibu mkuu wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba, amejiuzulu wakati alipaswa kufukuzwa.

Sababu ya kujiuzulu? Yeye na wenzake “aliokufa” nao eti ama walishindwa au kumshauri vibaya mwenyekiti yaani rais Jakaya Kikwete! Ni ajabu! Kwani hana uwezo wa kutumia akili? Je, kumshauri mwenyekiti ni kumfanyia maamuzi? Je, ni mara ngapi rais anashauriwa na upinzani na vyombo vya habari afanye maamuzi magumu anadharau na kusikia ushauri wa akina Makamba wa kukana kuwapo ufisadi serikalini mwake?

Ajabu ya maajabu, CCM hawakutaja “ushauri mbaya” aliowahi kupata Kikwete toka kwa kina Makamba!

Zengwe hili lilipewa jina tamu la kujivua gamba. Je, CCM ina magamba mangapi? Wahusika hawakutaka kujibu swali hili. Kwa yaliyonenwa baada ya kikao, ni kwamba CCM inataka kuwahadaa Watanzania kwa kuwaaminisha kuwa imejivua gamba la ufisadi. Hata hivyo haiingii akilini. Maana hakuna siku Yusuf Makamba na wahanga wenzake waliwahi kutuhumiwa ufisadi zaidi ya kutumiwa na mafisadi papa kuwatetea.

Je, kweli CCM imejivua gamba au inajigamba tu? Gamba gani imejivua iwapo imewaogopa hata watuhumiwa wa wazi wa ufisadi?

Eti wanafanya usanii kusema wamewapa siku 90 wajiuzulu wenyewe. Je, wasipotaka kujiuzulu CCM itawachukulia hatua gani? Kimya! Je, wakiamua kufa na mwenzao Kikwete kama ambavyo Makamba ameamua kufa na wenzake Kikwete na CCM watakuwa salama?

Je, CCM wametumia shinikizo la siku 90 kama njia ya kistaarabu ya kugwaya na kutaka kufunika kombe wanaharamu wapite na watanzania wasahau? Maana wangekuwa serious wangependekeza hata hatua za kuchukua.

Ukichukulia kuwa CCM ndiyo inaunda serikali, ingemaanisha inachosema basi wahusika wangefikishwa mahakamani haraka kutokana na kuwapo ushahidi wa wazi unaowahusisha watuhumiwa.

Ajabu CCM hiyo hiyo inayodai kujivua gamba, serikali yake ndiyo imo kwenye mchakato wa kulipia ujambazi wa Dowans! Na hao hao wanaotoa siku 90 ndiyo hao hao waliokuwa watuhumiwa walihusika na ufisadi! Je, hapa nani anamdanganya nani?

Je, hawa watuhumiwa wameanza kuwa gamba lini iwapo Kikwete mwenyewe alizunguka kwenye majimbo yao pamoja na vyombo vya habari kumshauri asifanye hivyo, kuwapigia kampeni akidai ni watu safi tena akilipwa per diem pesa yetu.

Hivi CCM na Kikwete wanadhani Watanzania ni wepesi kusahau kiasi hiki? Nakumbuka akiwa jimboni Monduli, alimuelezea Lowassa kama mchapa kazi hakuna mfano. Je, alimaanisha Lowassa ni fisadi hakuna mfano?

Je, kama Lowassa, Chenge na Rostam wanapaswa kujiuzulu, yeye Kikwete anangoja nini iwapo naye alishutumiwa kuwa fisadi kwenye List of Shame ya CHADEMA ukiachia mbali kuwakingia kifua na kuwapigia kampeni?

Je, hii maana yake si kwamba Kikwete aliwapotosha watanzania wa majimbo wanayowakilisha hawa watuhumiwa wakachagua watu wasiostahiki wala kufaa? Je, mtu wa namna hii anaweza kuaminika au chama chake? Je, akiwalipua wao wataacha kumlipua au tutegemee kushuhudia ambayo hayajawahi kushuhudiwa ambapo kunguru wataanza kupigana?

Je, ni watuhumiwa wa ufisadi upi wanaopaswa kuachia ngazi? Je, na watuhumiwa wa EPA wamo? Kama wamo akina Benjamin Mkapa mbona hawatajwi? Mbona Kikwete mwenyewe hatajwi na kupewa shinikizo ikichukuliwa ndiye mnufaika mkuu wa kashfa hii? Uzuri ni kwamba hajawahi kukanusha zaidi ya kukaa kimya.

Je, EPA si gamba sawa na Kagoda, Richmond, Dowan na Rada na ndege ya rais magamba waliyovaa watuhumiwa? Je, kughushi vyeti kwa baadhi ya mawaziri na wanachama wa CCM si gamba? Wizi wa pesa za umma kwenye wizara na serikali za mitaa si magamba? Je, mikataba ya kijambazi ya uwekezaji si gamba? Uongo nao si gamba?

Uchakachuaji nao si gamba jamani? Sasa kama magamba ni mengi, mbona CCM haijajivua gamba lolote zaidi ya kujigamba kwa kuwatoa kafara akina Makamba? Je, Watanzania wataingia mtego na ghiliba hii? CCM ina magamba zaidi ya milioni.

Ukisema ujadili magamba yote ya CCM utatunga kitabu. Je, CCM inapaswa kujivua gamba au kuvuliwa kama gamba la taifa? Je, CCM imejivua gamba lipi iwapo bado tunaona mengi yakizidi kutuna?
Chanzo: Tanzania Daima, Aprili 20, 2011.

No comments: