The Chant of Savant

Thursday 9 December 2010

Je ni kweli Makinda amechongwa na kusimikwa na mafisadi?





Kuna tetesi zinazunguka kuwa spika wa Bunge Anne Semamba Makinda ni chaguo na zao la mafisadi. Tetesi hizi zinazidi kupasha kuwa Makinda alipachikwa na mitandao ya CCM ya kifisadi na akajirahisi na kukubali kutumika kulipizia kisasi kwa spika aliyemaliza muda wake Samuel Sitta.

Kimsingi waliolipiza kisasi kwa Sitta hawakufanya hivyo kwa Sitta bali taifa. Maana kama siyo kulenga kulidhoofisha bunge na hoja zinazoiumbua serikali, basi wamelenga kwenye uchaguzi mkuu wa 2015. Hapa bila shaka, hawakutaka mtu anayeweza kuruhusu bunge hata kuridhia uandikwaji katiba mpya ambayo ndiyo nyenzo ya kutupatia serikali makini, safi na yenye visheni. Je mkakati huu utashinda? Je umma unaoathirika na siasa na serikali za majaribio utaendelea kufumbia macho genge hili ukiachia mbali madhira mengi liliyokwisha kuusababishia?

Pia huu ulikuwa mwanya wa pekee wa kupambana na uchakachuaji tulioshuhudia kwenye uchaguzi uliopita. Hivyo basi, hii maana yake ni kwamba 2015, kama mkakati huu utafanikiwa, tutaona mengi ya kuchusha na kukera kiasi cha kujikuta kwenye machafuko. Hapa ndipo waliosuka mkakati huu hawakuona mbali.

Si hayo tu. Shutuma hizi, licha ya kumdhoofisha, zinamuondolea udhu na imani ya wananchi spika Makinda.

Je tetesi hizi ni uongo au za kuweza kufutika chini ya busati au kufanyia kazi? Je tetesi hizi zaweza kujifia hivi hivi? Je tutegemee nini toka kwa mtu wa namna hii?

Kutokana na uzito wa asasi anayoongoza, kuna haja ya Makinda kujitokeza na kuua uvumi huu. Je ni kweli Makinda alipitishwa na waliompitisha ili kumkomesha Sitta? Je kama ni kweli, huu si ushahidi wa udhaifu wake kuwa anaweza kumtumikia kila kafiri ilimradi apate chake? Je kwa nafasi yake nyeti hivi hii inamwacha kwenye hali gani zaidi ya kumpotezea heshima na imani toka kwa umma?

Makinda anaweza kuwa na sifa zote za kuwa spika. Ana uzoefu tokana na kuwa mbunge kwa muda mrefu ukiachia mbali kuwa naibu spika. Anaweza kuwa na nia nzuri na taifa. Lakini yote haya yanamomonyolewa na madai kuwa alichomolewa huko aliko kuwa kuja kutumikia mafisadi katika kuwalinda na kulipiza kisasi kwa wabaya wao. Huu bado ni mchezo mchafu hata ungepewa msamiati mzuri vipi utabakia kuwa mchezo mchafu. Hapa ndipo Makinda anapaswa kuja na kuueleza umma kuwa yeye si chaguo la mafisadi bali CCM katika ufunuo wake mpya wa kuwajali kina mama.

Makinda, kama kweli hajachomolewa alikochomolewa na kutumika kulipiza kisasi, ajitokeze basi ajitetee na kutoa msimamo wake. Na katika kufanya hivi atoe majibu yanayoingia akilini badala ya kupiga siasa kama walivyozoea.

Ingawa umma ulitangaziwa kuwa zamu hii CCM imeamua kuwakumbuka kina mama, hili kidogo linatia shaka. Kwanini sasa na si siku zilizopita? Kwanini Makinda na si wengine wenye udhu na sifa kemkem zaidi yake?

Wengi wanashangazwa na mapenzi ya ghafla ya CCM kwa kina mama. Mbona hawakuwafikiria wanawake kwenye vyeo vingine? Ni mara ngapi tangu zama za Benjamin Mkapa wameshauriwa wateua mwanamke kushika nafasi ya waziri mkuu bila kufanya hivi? Hii maana yake ni kwamba madai kuwa Makinda ametumika kumkomoa Sitta yanaingia akilini. Hii inamwonyesha Makinda ima kama fisadi au mwenye tamaa anayeweza kutumiwa na mtu au kundi lolote akiweka kando maslahi ya taifa.

Kwa madai kama haya, utendaji wake lazima uingie dosari. Je Makinda atautumikia umma au wale waliomuumba na kumuibua? Bila kujibu hoja hizi Makinda ataendelea kuchukuliwa kama mtu rahisi wa kuweza kutumiwa na yoyote tena kwa madhara ya taifa. Je Makinda tunayeambiwa alifinyangwa atakuwa tofauti na kuibua wa kweli? Time will surely tell.

Mtu anayeweza kutumiwa kirahisi na haraka hivi hafai kusimamia mhimili wa dola achia mbali ofisi ndogo. Mtu wa namna hii ni kifaa katika mikono ya wengine. Hafai. Mtu ambaye haoni ubaya wa mafisadi hawezi kuona uzuri wa kuwaandama. Nisingependa spika wangu adhoofike na kudhalilika hivi.

Kitendo cha Makinda kufinyangwa {kama ni kweli na atakaa kimya) na watu wenye harufu mbaya ya ufisadi tena walio karibu na rais Jakaya Kikwete kinaondoa maana nzima ya mgawanyo wa madaraka. Nani asiyejua kuwa watu hawa wana ushawishi mkubwa kwa rais kiasi cha kuonekana kama wao ndiyo wanaongoza nchi? Rejea wengi wao kuwajibishwa na bunge lililopita lakini rais huyu huyu akawapigia debe na wakarejea bungeni. Rejea wosia wa baba wa taifa kuwa CCM imetekwa na mafisadi. Rejea wosia wa aliyewahi kuwa katibu wa CCM, marehemu Horace Kolimba kuwa CCM imepoteza mwelekeo. Tuseme. CCM imegeuka kokoro ambalo huzoa kila uchafu katika kusaka samaki.

Rejea wengi wao kuwa ndiyo wenye funguo za vyanzo vya pesa ya kampeni ya Kikwete mfano EPA ambayo hajawahi kujitenga nayo lau kwa kutoa utetezi au maelezo.

Leo sitasema mengi zaidi ya kumtaka Makinda ajitokeze na kuondoa utata huu uliogubika kuteuliwa na hatimaye kuchaguliwa kwake na CCM kuwa spika. Na asiishie hapo. Kwenye utendaji wake atumie viwango tulivyoshuhudia kwenye bunge lililopita badala ya vile vya mafisadi- awape nafasi wabunge kuja na hoja zenye kulinda maslahi ya taifa na si kuwaminya ili kuwafurahisha na kuwaokoa mafisadi waliomfinyanga.

Makinda, amka ujisemee badala ya kuacha uvumi kuendelea kuzunguka wadhifa wako.
Chanzo: Tanzania Daima Desemba 7, 2010.

2 comments:

Anonymous said...

Wee Mhango acha kumtukana mama wa watu: kuchongwa na kusimikwa ndio nini? Au ulitaka kusema amechomekwa? Si unajua tena wale madereva wa daladala wanavyochomekea! Kama ni hivyo ninakubalina nawe - amechomekwa na mafisadi.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Mpendwa Anonymous,
Shukrani kwa kunitembelea na kudondosha ujumbe ingawa sikubaliani na uoni wako. Mie simaanishi zaidi ya kutengenezwa na si kuchomekwa kwa maana unayokusudia au kusimikwa kwa maana uliyoteua.
Muhimu ni yeye kujitokeza na kukanusha vinginevyo watu wataendelea kuaminia amechongwa, kusimikwa hata kuchomekwa kwenye ofisi ya spika bila stahiki.