The Chant of Savant

Thursday 9 September 2010

Salma Kikwete anapiga kampeni kama nani na kwa pesa ipi?

Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Mama Salma Kikwete (kulia) akisalimiana na Mwenyekiti wa UWT mkoa Dodoma Fatma Tawfiq alipowasili katika uwanja wa ndege Mkoa wa Dodoma jana.katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mh. James Msekela. Tarehe 28 Agosti 2010.

JUZI niliona habari kuwa mke wa rais Jakaya Kikwete aliyetambulishwa kama mwenyekiti wa WAMA, Salma Kikwete, akimnadi mgombea wa ubunge CCM, jimbo la Mafia, Abdulkarim Shah.

Swali la kwanza lililonijia ni: kama WAMA ni asasi isiyo ya kiserikali ya kutetea wanawake wote wa Tanzania wakiwemo na wa vyama vya upinzani, inakuwaje mwenyekiti wake amnadi mgombea wa CCM?

Je, kweli WAMA iko kwa ajili ya maendeleo ya wanawake wote kama jina lake au kutumika kama chombo cha kukusanyia pesa kwa ajili ya familia ya Kikwete na chama chake? Je kwa kujiingiza kwenye siasa, bado WAMA inaaminika? Je WAMA si taasisi ya nyuma ya pazia ya ulaji ya CCM kwa mgongo wa ikulu?

Nikiri. Nimekuwa na picha mbaya ya WAMA si kwa sababu nina ugomvi nayo bali hali halisi. Nikikumbuka yaliyotokea kwa EOTF ya Anna Mkapa iliyoishia kuwa kichaka cha ufisadi kwa kutumia ikulu, sina imani na amani na WAMA.

Kuondoa utata basi WAMA iitwe WAMACCM yaani Wanawake na Maendeleo wa Chama Cha Mapinduzi. Hili likifanyika sitakuwa na ugomvi na WAMA ingawa kama mchezo wa kutumia mali za umma na serikali kufanya shughuli za kisiasa kama ilivyo utaendelea, vitanilazimisha kuwashukia tena. Huu ni wizi hata kama unafanywa na wakubwa. Wizi ni wizi na si mzuri.

Niliwahi kuuliza ingawa sikujibiwa. Kwanini kila shughuli ya WAMA inaonekana kuwa ya kidikteta kwa maana ya kusimamiwa na mtu mmoja-Salma kiasi cha WAMA kuwa Salma na Salma kuwa WAMA?

Kwa nini iote baada ya bwana mkubwa kuingia madarakani kama lengo si ulaji kwa kutumia mgongo wa ikulu kama EOTF?

Hata ukiangalia mpangilio wa watendaji wake unagundua kuchanganya mambo kiasi cha kuumbuka au kuufichua ukweli ulioko nyuma ya pazia. Kwa mfano kwenye watendaji wa WAMA kuna mtu aitwaye Anande Munuo ambaye ametajwa kama secretary to the first lady siyo to the chairperson. Hii ni nini kama siyo kufanyiana usanii?

Habari tajwa inaendelea kusema kuwa Salma alikuwa kwenye ziara ya siku moja kisiwani Mafia kuwahamasisha wanachama wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) kuwachagua wagombea wa CCM! Je hapa kuna swali tena? Je huu si ushahidi wa kimazingira kuwa asasi hii ni hatari kwa demokrasia kwa sababu kuu mbili:

Mosi kutumika kisiasa kwa manufaa ya Kikwete na CCM. Na pili kuanzisha katika wakati na mazingira yanayotia shaka ukiachia mbali shughuli zake kutia shaka vile vile. Mbona hatuoni taarifa ya ukaguzi wa hesabu za WAMA kila mwaka? Nani ataikagua iwapo hata mume wake amegoma kutaja mali zao na WAMA ikiwemo?

Hapa hujagusia mapokezi mazito anayopewa kama mke wa mkubwa kila anapokwenda m ikoani hata nje ya nchi anapokusanya pesa kwa mgongo wa ikulu. Bado hapa hujadodosa misafara mirefu ya magari anayoandamana nayo. Kama nani chini ya katiba yetu viraka? Je huku si kutumia vibaya madaraka kwa mumewe? Leo utasoma habari za Salma akifanya kazi ya CCM kesho mwanae wa kufikia, Ridhiwan akimnadi baba yake kabla ya baba mwenyewe. Je hapa si kutengeneza ufalme wa familia ya Kikwete jamani?

Najua Salma ni mwalimu. Wengi wangedhani, kama kweli angekuwa ana uchungu na watanzania, basi angewekeza kwenye elimu badala ya siasa za nyuma ya pazia. Asingepata muda wa kuwania nafasi chamani bali kutumia muda wake kama first lady kuhamasisha elimu iliyosahauliwa na utawala wa mumewe. Hata hayo maendeleo yasiyoonekana anayohamasishwa yanakwamishwa na serikali ya mumewe iliyokumbatia ufisadi na kujuana.

Tusiseme bila ushahidi. Wako wapi kina Kagoda ambao wanazidi kutesa huku wanaowapinga wakiteseka? Wako wapi kina Richmond wanaotukoga kila uchao kuwa urafiki wao na Kikwete si wa barabarani na hauwezi kuvunjwa na vyombo vya habari? Leo fisadi ananyea ofisi mchana anatimuliwa lakini anaitwa mstaafu! Tangu lini mharifu aliyekiri kwa kujiwabisha akawa mstaafu? Au ni kwa vile wastaafu wa kweli kama vile waliokuwa wafanyakazi wa Jumuia ya Afrika Mashariki tumewadhulumu na kubadilisha maana ya mstaafu? Kama Salma na WAMA yake wanapigania maendeleo kweli, kwanini asimwambie mumewe kuwa maendeleo hayawezi kupatikana katikati ya ufisadi na ubabaishaji?

Wakati Salma akiwatumia wanawake na ikulu kumpigia debe mumewe, mumewe naye anatumia magari ya umma kujipigia kampeni! Hivi nchi hii imerogwa na nani na itapona lini?

Je, kwa tabia hii na ufichi huu Salma anajitofautisha vipi na ma-first ladies mafisadi kama Grace Mugabe bingwa wa kufuja pesa ya umma, mareheme Stella Obasanjo aliyewahi hata kutoa amri ya kufungia gazeti, Lucy Kibaki aliyewahi kuwachapa waandishi wa habari bila kusahau, Nana Kanadu Rawlings aliyewahi kutajwa na mumewe kuwa ni binadamu pekee ambaye angeweza kumdhibiti Jerry Rawlings rais wa zamani wa Ghana?

Je, kitendo cha mke wa rais kutumia taasisi isiyo ya kiserikali kuwahadaa na kuwahonga kina mama hakitoshi kuwa ufisadi? Kwanini wapinzani wasichukue hoja hizi na kuwabwagia watanzania wajue nchi yao inavyoliwa kwa mgongo wa rais? Haya ni matumizi mabaya ya mamlaka yanayokinzana na utawala bora na wa sheria anaojisifia kutekeleza rais Kikwete. Wapinzani wakiuonyesha umma madudu yake, licha ya kufichua ubovu wake, watakomesha tambo na uongo wa Kikwete ambaye kwa miaka mitano hajafanya lolote la maana zaidi ya kulinda ufisadi na matumizi mabaya ya raslimali na fedha za umma.

Pia kwa kufichua hujuma ya WAMA angalau wananchi watajua siri ya kampuni hii kuundwa pindipo rais Kikwete alipoingia madarakani na si kabla. Kwa kuiandama hata kuifutilia mbali WAMA tutaepusha wake za marais wajao kuendelea kutuibia kwa kisingizio cha NGO na visingizio vingine ambavyo kimsingi vinaonyesha hizi NGO zinaanzishwa kwa minajili ya kujitajirisha na kuzitumia kupitisha rushwa kwa wapiga kura kama inavyofanya WAMA.

Ningeshauri WAMA iitwe MAWA au Maulaji ya Wake (za Wakubwa). Ukitaka kujua ninachomaanisha nenda uangalie wadhamini wa WAMA. Ni mke wa makamu wa rais na mgombea wa urais wa CCM Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, Zakhia Meghji waziri wa fedha wa zamani, Balozi Mwanaidi Majaar, Sophia Simba waziri wa Kikwete, Blandina Nyoni katibu wizara Regina Lowassa mke wa waziri mkuu aliyetimuliwa na wengine wakubwa tu. Hapa WAMA haijawa mradi wa ulaji wa wake za vigogo na vigogo? Je hawa hawajateuliwa kutokana na kujuana na bi mkubwa aliyempa ushauri mumewe awateue mashoga na washirika wake katika kusaka ngawira?

Hakika WAMA imeficha mambo mengi ambayo umma unapaswa kuyajua hata kuhoji.

Wapinzani na watanzania ibomoeni WAMA. Kwani inatumika kutuhujumu kwa mgongo wa ikulu na ni alama ya matumizi mabaya ya madaraka, ulafi, ufisadi na udhalilishaji wa taasisi ya urais.

Je, Salma anapiga kampeni kama nani na kwa pesa ipi?

Chanzo: Tanzania Daima Septemba 8, 2010.

No comments: