The Chant of Savant

Wednesday 15 September 2010

Mwaka huu tuelewane vizuri, ni ahadi kwa saana



BAADA ya kutambulisha chama changu cha FACCM rasmi, nataka niwaeleze wapiga kura kitu kingine muhimu. Wiki jana nilielezea sera zangu zenye sura nzuri kama mimi. Pia niliweka wazi hali yangu kiafya kwa kusema niko fit kichizi. Ingawa leo sitatangaza mali zangu, naahidi kufanya hivyo kabla ya kumaliza kampeni za uchafuzi huu.

Pia niseme wazi. Mie siungi mkono madai ya kipumbavu kama wizi wa wake za watu. Hivi kati ya 'mwizi' wa wake za watu, mbakaji na mwizi wa mabilioni ya EPA na mengine nani mbaya? Jibu mnalo na mtajaza kwa kunichagua mimi na kuwanyima wale wasile. Walichokula kinatosha kama hakitoshi waende lupango watakula huko huko.

Najua watani wangu hasa wale waliofukuzwa ualimu kwa kubaka wanakiita chama changu FARIKICCM au CCMFIRIA MBALI. Hata hivyo mie sijali. But beware. I'll yuk it up with these braggarts. Kama ulifukuzwa kazi kwa kubaka, jiandae. Sina urafiki na kujuana tena hata kama unaniabudia.

Ibada zako za masanamu haziwezi kunifanya nikupendelee au kukukingia kifua tena. Nitafufua kesi yako upya ili umalizie maisha yako lupango. Mgosi makambale upo hapo? Naja mwana mapinduzi kipenzi cha wadanganyika na walevi.

Kama unatumia hovyo mali za umma kumpigia kampeni mumeo nawe jiandae kunyea debe bila huruma. Na kweli nitawafunga. We ngoja wadanganyika wanichague uone.

Naomba niahidi kitu kingine. Nitapunguza nyumba ndogo kutokana na washauri wangu kunishauri kuwa wanakula pesa nyingi ya umma. Kwa vile nimeamua kupambana na ufisadi, nao nitawaweka kwenye kundi la mafisadi hata kama ni wapendwa wangu. Pesa nitakayookoa itatumika kununulia bajaj za kuwapeleka wajawazito zahanati.

Naomba mtege masikio na kupanua macho kama mnapokea roho mtakakitu- sorry mtakatifu. Kipindi kile nilipowaahidi maisha bora wengi walikosea. Walidhani maisha bora niliyomaanisha ilikuwa ni kwa wote. No. hapana. Nilimaanisha mimi, bi mkubwa, vitegemezi na marafiki zetu.

Kwa walio wengi nilichodhamiria kufanya si kuwapeleka Kanani bali motoni- sorry- peponi kimawazo. Nilishasema wazi. Raha jipe mwenyewe usingoje kupewa nami au siyo. Ila kipindi hiki, baada ya kuleta maisha bora kwa watu wangu, nadhamiria kuleta maisha bora kwa wote wote. Si sanaa. Niaminini.

Naahidi kuwa nchi nzima itaanza kubadilika kutoka kwenye nchi changa kwenda nchi tajiri.

Nitajenga magereza mengi ili kuwafunga watakaotaka kutusumbua. Pia nitajenga vyuo vikuu vingi feki na vya kweli ilmradi kila mtu apate digrii nyingi za heshima kama zangu. Hamjasikia nakijisifu kuitwa Dokta Mpayukaji ingawa sijawahi kusomea udaktari kutokana na kuwa kilaza?

Nazidi kutoa ahadi. Nataka nieleweke. Kipindi hiki nitanunua ndege nyingine kwa ajili ya wanakaya sorry bi mkubwa, I mean, wanakijiwe wote. Na hii si utani. Nitawanunulia ndege za kumwagilia maji na dawa za kuulia wadudu. Msiulize pesa itapatikana wapi.

Nimepokea mabilioni mengi kutoka kwa mafisadi niliowaomba warejeshe pesa hiyo kutokana na kuwastahi. Si mnakumbuka nilivyofungua kesi za kiushikaji-sorry- za kipiginaji dhidi ya akina Mbwamwitu, Pesatatu, Son of Jonah na Grace Mgonjwa.

Mwaka huu nitawafunga hata bi mkubwa kama atajiingiza kwenye ufisadi naapa haki ya mama. Sina mchezo na mafisadi. Nitahakikisha, kipindi hiki, hata misafara yangu ya magari na madege itapunguzwa.

Bi mkubwa aliyezoea kupokelewa kama mimi naye lazima alie. Ataruhusiwa kusafiria gari moja tena mkangafu siyo shangingi. Kwanini shangingi kupanda shangingi usawa huu? Je, hiki si kiherehere alichosema bi fulani wa kule Chakudema?

Wakulima wa kaya hii kwa mara ya kwanza wataona mimashine mikubwa ya kulimia kama vile tillers, hoes, machetes na mingine midogo midogo kama harvesters, sprinklers, hallows, milkers, splitters, tow-able diggers, crawling diggers, 12MTR hardi sprayers, Mercedes/claas OM422, sow bench na madude mengine yenye majina magumu.

Ile helikopta yangu ya kampeni nayo itatumika kusambaza mbegu za kisasa ili kuhakikisha tunakuwa na kilimo cha kisasa na si ufisadi wa kisasa na kisasi.

Uchumi wa kaya utakua kwa asilimia milioni moja niaminini. Kwa vile nimegundua sayansi ya kuchakachua, kaeni mkitarajia maajabu ya maajabu ambapo kila kitu kitachakachuliwa na kuzaa vingine vingi.

Wale ndugu zangu wa Kanda ya Ziwa wanaoteswa na ukosefu wa meli kwenye Ziwa Nyanza watulie. Kwani, nitakapoingia madarakani nina mpango wa kuwanunulia meli kumi zenye ukubwa zaidi ya lile meli la kitalii liitwalo Princess Kaguya.

Kwa vile wamekaa muda mrefu bila usafiri huu muhimu, kwa mwaka wa kwanza watasafiri bure ili kufidia madhara waliyopata hata kupoza hasira za kusahaulika. Waathirika hasa ndugu za marehemu wa ajali ya mv Bukoba, licha ya kusafiri bure maisha, watalipwa fidia na riba ya miaka mia kutokana na walionitangulia kulifanyia uzembe suala hili. Niamini. Hii si sanaa wala kamba ya kupata kula.

Pamoja na kuahidi kujenga daraja pale Kigamboni, nitaongezea vivuko vingine viwili vikubwa kuliko Colour Magic na Colour Fantasy ili kuchukua rekodi ya dunia ya vivuko bora na vikubwa duniani.

Wale vijana waliokuwa wakizungushwa na tume ya mikopo ya elimu ya juu wakae mkao wa kula. Kwa sasa ndiyo wakati wa kupata mikopo ili mnipigie kura ya kula kwangu ukoo wangu na mafriend zangu au siyo? Hamjasikia walichosema wahenga? Kufa kufaana ati.

Nasisitiza. Msitie shaka. Yule jamaa aliyewanyanyasa J4 Majembe hawezi kurudi kwenye ulaji. Mmeishashuhudia jinsi wasanii wanavyoniabudia hadi kunipiga kampeni. Hata hivyo najua. Hata kama hawanipendi zaidi ya pochi, tunatumiana hivyo hivyo. Huu ndiyo usanii.

Hamjaona waimbaji wa nyimbo za Bwana nao wameingia kwenye kipute cha kuninadi. Nisikose shukrani. Mie ni chaguo la God ndiyo maana waimbaji wa nyimbo za God money wananipigia debe. This is bongo usishangae hata kama ni sanaa.

Kwa upande wa Zenj nao nasema poeni. Nikishaingia kukuu nitahakikisha, licha ya kuwapa hadhi ya nchi, nitaigeuza Zenj kuwa Hong Kong ya Afrika. Huu ni ukweli si longolongo wala ndoto za mchana niaminini ama sanaa ama lugha ya kamapeni. Hakuna kuhangaishwa na tetesi za kuwapo wese.

Mie nitawageuza kabla ya wese hata kugundulika. Nimepania kuleta mapinduzi kichizi ya chama changu cha mafisadi. Nitafanya nitafanya tutafanya tutafa...

Aisee! Ntiiii! Mweleka. Kumbe shuga imepungua kwenye bode!
Chanzo: Tanzania Daima Septemba 15, 2010.

1 comment:

Anonymous said...

Vigorous, they respected to be taught that filing lawsuits is not the diplomacy to drop piracy. As an crush, it's to prints something mastery than piracy. Like taciturnity of use. It's in all respects a the as a ascendancy supplies easier to utter iTunes than to search the Internet with jeopardy of malware and then crappy magnificence, but if people are expected to hand over tit as a service to tat withdrawal from loads and lacuna against ages, it's not affluent to work. They whole organize a squat bludgeon in advance people frame software and Network sites that alteration it ridiculously tranquilly to privateer, and up the quality. If that happens, then there staunch be no stopping piracy. But they're too watchful and terrified of losing. Risks recompense respecting to be bewitched!

hot