The Chant of Savant

Monday 30 August 2010

Tuhoji 'mafanikio' ya Kikwete









Taarifa kuwa kuna wabunge wa Chama Cha Mapinduzi zaidi ya kumi wamepita bila kupingwa si za kufurahisha hasa katika kipindi hiki tunapojigamba kukomaza demokrasia.

Hivi karibuni, kabla ya kuanguka akihutubia wafuasi wa chama chake, rais Jakaya Kikwete alijisifu kuwa amefanikiwa kustawisha demokrasia na haki za binadamu. Je ukiangalia hali halisi aliyosema Kikwete ni kweli au siasa na ghilba?

Ni mafanikio gani ambapo, karne ya 21, eti mtu anapita bila kupingwa? Tumejaribu kupitia baadhi ya majimbo na kushangaa. Hebu chukulia kwa mfano, jimbo la Karagwe ambapo mbunge aliyemaliza muda wake licha ya kukabiliwa na tuhuma za rushwa eti amepita bila kupingwa! Inashangaza sana. Je haya ndiyo mafanikio Kikwete anayopigia upata ya kukuza demokrasia? Mbona wale watuhumiwa wa kughushi vyeti vya taaluma wengi wao wamepita? Mbona mbunge Samuel Chitalilo aliyebainika kughushi vyeti na kuwadanganya wapiga kura hata watanzania amepeta bila kufikishwa mahakamani na sasa anastaafu na kupewa kiinua mgongo kwa jinai hii?

Kikwete alikaririwa akisema eti anajivunia kupambana na ufisadi! Hili nalo ni ajabu la maajabu. Kikwete amepambana na ufisadi gani iwapo watuhumiwa wakuu kama Andrew Chenge, Edward Lowassa, Basil Mramba na wengine wakipeta? Huku ndiko kupambana na rushwa kweli?

Yako wapi maisha bora kwa watanzania wote tuliyoahidiwa? Inatisha sana. Wakati Kikwete akijivuna kuwa amekuza demokrasia hasa haki za binadamu na upashanaji na upokeaji habari, siku aliyoanguka, wananchi walifichwa picha ya tukio kiasi cha kuondoa hata zile zilizokuwapo kwenye mitandao kipindi kidogo baada ya kuwekwa.

Kikwete angekuwa mkweli basi angetaja hata kinachomsumbua hivi sasa hadi akaanguka mara kwa mara. Kama alichomaanisha alikimaanisha kweli basi atuondoe kwenye shaka kuhusiana na afya yake ambayo imezua minong'ono mingi.

Tuhoji mafanikio ya Kikwete bila kuogopa mamlaka yake na chama chake. Tuhoji kwa ajili ya faida ya vizazi vijavyo nasi. Maana ni haki yetu na nchi hii ni yetu si ya Kikwete wala CCM. Huwezi kuwandanganya watu mchana kutwa wakakuacha bila kuhoji. Tujalie kuwa Kikwete alimaanisha alichosema. Je hajui kuwa watanzania hawakupata picha kamili ya tukio ukiachia mbali maelezo yanayoingia kichwani?

Je Kikwete ambaye amejizungushia waramba viatu na wapambe waliomgeuza kipofu na kiziwi kuhusu vilio vyetu, haoni watanzania wanavyotaabika ukaichia mbali kungoja kuonja maisha bora kwa miaka mitano bila kitu?

Ingawa ni haki yake kujinadi ili achaguliwe, Kikwete atutendee haki-atwambie ukweli. Akiri pale alipokosea au kulega lega. Bahati mbaya sana, kwenye mikutano yake ya kampeni huwa hakuna fursa ya kuuliza maswali zaidi ya kuhubiriwa. Je huku ndiko kukomaa kwa demokrasia? Amekwepa hata kushiriki midahalo angalau aulizwe maswali. Je huku ndiko kukuza demokrasia na kutekeleza aliyoahidi?

Juzi nilisikia akijitapa kuwa hata ujambazi umepungua! Ebo! Hivi Kikwete alisoma habari za kifo cha Profesa mashuhuri wa sheria marehem Jwan Mwaikusa? Mbona kila siku magazeti yanafurika habari za majambazi 'kutesa' tena kwenye jiji anamoishi Kikwete-Dar es salaam ambayo si bandari salama tena bali bandar nakama?

Siandiki makala hii kwa chuki dhidi ya Kikwete bali upotoshaji uliojitokeza kutokana na tambo zake. Ukitaka kujua ninachomaanisha, kwa wanaoishi Dar, hebu nenda kwenye hospitali za Mwananyamala, Temeke na Amana uone wagonjwa wanavyorundikana. Hebu hoji matumizi yake hasa kwenye ziara zisizo na faida ughaibuni ambako, baada ya kuanguka wengi wanaanza kusema kuwa huenda kujitibia ingawa si imani yangu kuwa ni hivyo.

Ni juzi tumetaarifiwa na mkaguzi mkuu wa pesa ya serikali (CAG) kuwa, kwa mwaka jana tu,

zaidi ya shilingi 1,700,000,000,000 ziliibiwa kwenye idara za serikali. Je haya ndiyo mafanikio ya kujivunia ya Kikwete? Hapa bado hujaangalia mabilioni mengine yaliyoibiwa miaka iliyotangulia. Kama tutafanya hesabu ya kweli ya kutoa na kujumlisha kuhusiana na wizi wa pesa za umma chini ya Kikwete, hatutakuwa na haja ya kumrejesha madarakani. Ametuangusha sana hasa kwenye kudhibiti na kutumia pesa na raslimali zetu.

Nilimsikia akijisifia kuwa amepanua wigo wa mapato kwa kukusanya pesa nyingi karibu mara mbili ya zile zilizokuwa zikikusanywa na mtangulizi wake. Well done. Je amezisimamia vipi kuhakikisha hazichotwi na wezi wachache wateule? Kukusanya pesa nyingi na kufuja nyingi zaidi si mafanikio wala jambo la kujivunia bali la kutia aibu na kukatisha tamaa. Je tutaendelea kudanganywa hadi lini?

Si uzushi. Serikali ya Kikwete, kwa miaka mitano iliyokuwa madarakani, imetuangusha kwa mambo mengi. Ni juzi juzi waziri wa miundombinu, Shukuru Kawambwa alikaririwa hivi karibuni akionyesha mafanikio ya Kikwete kama ifuatavyo: “Ukiangalia utendaji wa bandari za nchi jirani na zetu utakuta za kwetu ziko chini sasa lazima tukae tujiulize kwanini tuwe na viwango duni vya utendaji kuliko wenzetu.”

Alitoa tamko hili baada ya kupata habari kuwa wateja wengi wa bandari ya Dar es salaam wameamua kupitishia mizigo yao nchi jirani kutokana na bandari ya Dar es salaam kukithiri kwa udokozi na wizi wa mizigo na ucheleweshaji unalonga kutengeneza pesa kwa njia ya rushwa. Je haya ndiyo mafanikio anayojivunia Kikwete?

Wako wapi watuhumiwa wa ujambazi wa kutisha wa EPA hasa kampuni la Kagoda linalodaiwa kumilkiwa na mbunge wa Igunga na swahiba mkuu wa Kikwete, Rostam Aziz?

Kuna swali kuu la kupaswa kujiuliza. Hivi Kikwete kweli angekuwa amefanikiwa kama anavyotaka tuamini, angehitaji kuchangiwa shilingi 50,000,000,000 na kusema kuwa takrima haiepukiki? Je huku si kushindwa vibaya sana kunakoitwa mafanikio?

Tuache utani kwenye mambo yasiyohitaji utani. Kikwete hajafanikiwa lolote. Na kwa wanaojua tabia ya binadamu hasa kwa kuzingatia uzoefu wa mtangulizi wake, akishapata ngwe hii ya lala salama, ata-mess zaidi.

Leo sitasema sana zaidi ya kuwataka watanzania hasa wapiga kura kuhoji na kuhoji na kuhoji hiki kitendawili ambacho Kikwete anakiita mafanikio wakati ni maanguko. Je huu ndiyo usanii ambao watani wake wamekuwa wakimtwisha? Mafanikio ya Kikwete hayawezi kupimwa kwa maneno yake bali hali za wananchi. Kwanini afanye mtihani halafu ajisahihishe mwenyewe na kujipa mia kwa mia wakati aliambulia nunge?

Watanzania tuache kuweka maisha yetu rehani kwa kunogewa na maneno na longo longo za wanasiasa wanaotutumia kama punda kubeba mizigo na madhambi yao. Kuna haja ya kufanya mapinduzi na kuchagua mstakabali wetu badala ya ushabiki wa kipumbavu unaoweza kufakamia kila uongo kwa kujali anayesema badala ya kinachosemwa.

Ajabu la maajabu ni ile hali ya kila kitu kusimamiwa na chama kilichotopea kwenye rushwa. Rejea yaliyojiri kwenye mchakato wa kura za kutafuta wagombea wa CCM. Hakika tuna kila sababu za kuhoji na kuhoji bila kukoma 'mafanikio' ya Kikwete ambayo ni mateso na maanguko ya umma.
Chanzo: Dira ya Mtanzania Agosti 30, 2010.

No comments: