The Chant of Savant

Sunday 29 August 2010

Sababu za watanzania kutoichagua CCM mwaka huu


















Niseme mapema. Mwaka huu sitaichagua CCM. Naamini sababu za kutofanya hivyo zinashawishi. Natoa sababu zifuatazo:

Mosi, ufisadi- CCM na serikali yake, licha ya kushindwa kukabiliana na ufisadi, hazijawahi kukanusha kuhusika na kashfa za Richmond, EPA, CIS na nyingine ambazo zilizamisha mabilioni hata matrilioni ya shilingi za umma. Ni juzi tu mwanasheria maarufu Mabere Marando alidai EPA ni mradi wa CCM ulioanzishwa kupatia pesa ya kumwingiza madarakani rais Jakaya Kikwete ambaye si yeye wala chama chake wamekanusha tuhuma hizi. Na hii si mara ya kwanza tuhuma hizi kutolewa. Hazijawahi kukanushwa. Ijulikane. Tuhuma hizi ni nzito na hazisahauliki wala kufichika hata kuziacha zijifie.

Pili, matumizi mabaya ya fedha za umma. Rejea ziara zisizo na faida za rais na mkewe nje na kuficha majina ya wajumbe wanaoandamana nao. Pia rejea ununuzi wa magari ya bei mbaya (mashangingi) ambapo inadaiwa serikali inamilki zaidi ya mashangingi 6,000 na kujilipa per diem. Pia kuna hili la ujenzi wa nyumba za mabilioni za watendaji wa serikali. Rejea kashfa za BoT na TANESCO.

Tatu, matumizi mabaya ya raslimali za umma. Rejea ubinafsishaji wa kifisi, mgao usio wa lazima wa umeme na nchi kukaa kizani kwa mwaka mzima karne ya 21 huku wezi wachache wakichota mabilioni kwa kutumia Richmond na serikali ikikaa kimya. Hapa hujagusa misamaha ya kodi yenye kila harufu ya rushwa.

Nne, viongozi wakuu wa serikali kutotaja mali zao kama wanavyotakiwa na sheria. Je kama siyo wezi wanaogopa nini? Je wanatoa picha gani kwa wananchi hasa kuhusiana na uwajibikaji wao? Je wana mali kiasi gani?

Sababu ya tano ni uzembe-kuibiwa pesa nyingi kwenye wizara na taasisi za umma ni juzi tu tuliambiwa kuwa mwaka jana kiasi cha shilingi 1,700,000,000 kiliibiwa. Hebu piga picha kwa nchi yenye bajeti ya trilioni 11 na ushei. Hii maana yake ni kwamba kilichoibiwa kwa mwaka mmoja ni sawa na 1/5 ya bajeti ya taifa ambalo hutegemea wafadhili kwa asilimia 40 ya bajeti yake. Je huu ni uzembe kiasi gani? Je kwa miaka mitano ya utawala wa kisanii zimeibiwa trilioni mamia mangapi? Je haya ndiyo maisha bora?

Sita, dhambi ya kujuana. Vyeo vingi hasa vya juu vyenye malipo manono vimekuwa vikigawiwa kwa upendeleo na kujuana. Rejea kwa mfano rais kumteua rafiki yake waziri mkuu mfukuzwa Edward Lowassa aliyeboronga baadaye kuthibitisha ubaya wa hili.

Sababu ya saba ni kutamalaki kwa rushwa. Rejea yaliyojiri hivi karibuni kwenye uchaguzi wa ndani wa kura za maoni wa CCM. Hawawezi kukwepa. Tena wamekamatwa na TAKUKURU yao.

Nane, masimamango. CCM na viongozi wake wamekuwa wakitusimanga kuwa watatuletea maisha bora wakati, kimsingi, wanaposema maisha bora kwa wote wanamaanisha wao, familia zao, marafiki zao na wawekezaji wa kweli na uongo.

Tisa, kutotimiza ahadi hata moja. Mwenyekiti na mgombea wa CCM aliyechangiwa mabilioni alituahidi mambo mengi hasa pepo. Kuna haja gani ya kumchagua kwa kutulipa jehanamu mahali alipoahidi pepo? Yako wapi maisha bora kwa watanzania ukiachia mbali watu wake wa karibu ambao hata wakiiba au kughushi vyeti hawaguswi?

Tisa, ni uongo. Hakuna serikali yenye kusema uongo kama ya CCM. Kila mtu anawahadaa wananchi kuwa ataweka maslahi ya nchi mbele wakati ukweli wanaweka maslahi ya chama na yao binafsi mahali pa maslahi ya taifa. Na hii ndiyo siri ya mafisadi kila aina kutamalaki na kuneemeka chini ya CCM ambayo watani wake huiita Chama Cha Mafisadi. Bahati nzuri Kikwete aliwahi kusema ana orodha ya majambazi, mafisadi, wala rushwa, wauza mihadarati na wengine wengi. Amezifanyia nini hizi orodha?

Kuna hili la ukosefu wa usalama. Rejea mauaji ya vibaka, vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi wakati majambazi na mafisadi yakilindwa.

Sababu nyingine ni kupanua ukubwa wa serikali bila sababu. Rejea kuundwa mikoa mitatu na kugawanya baadhi ya wilaya kwa maslahi binafsi ya kisiasa kichama na makada wake. Tunataka huduma bora si ukubwa wa serikali ya kishikaji.

Kutosimamia uchumi wa nchi vizuri. Rejea kwa nchi yenye tamalaki ya madini kuwa maskini kuliko hata nchi zilizotoka kwenye majanga jana tena ndogo kama Burundi na Rwanda. Je pesa ya raslimali zetu inakwenda wapi na kumnufaisha nani iwapo watu wetu wanazidi kuwa maskini?

Utawala mbovu usio na mipango wala ubunifu. Rejea maisha magum na ukosefu wa mbolea pembejeo na masoko kwa wakulima na kejeli ya kilimo kwanza wakati ni uwekezaji ubinafsishaji na ufisadi kwanza.

Kuua elimu, rejea kuwa na matundu mengi yaitwayo madarasa yasiyo na vifaa wala walimu.

Kuchusha na kuchoka kwa CCM. Rejea maneno ya baadhi ya waliowahi kuwa viongozi wake kuwa CCM haina mwelekeo na imetekwa na wafanyabiashara nyemelezi. Hayakunushwa zaidi ya wahusika kuuawa au kukolimbwa kama ilivyokuja kujulikana baadaye.

Kuna hili la migongano na migawanyiko ndani baina ya makundi ya kimaslahi au mitandao. Makundi haya yanakula muda na pesa nyingi ya umma kwenye kumalizana badala ya kutatua matatizo ya wananchi yaliyofanya wahusika wachaguliwe. Hawa wengi wao ni wabunge wa CCM wanaojiwakilisha kwa kuwahadaa wananchi kuwa wanawawakilisha.

Pia sitaichagua CCM kutokana na kuua demokrasia. Rejea kutokuwapo kwa tume huru ya uchaguzi na msajili wa vyama kutumika kuviua na kuviminya vyama.

Matumizi mabaya ya vyombo vya dola. Rejea polisi kutumika kuwanyanyasa wananchi huku walimu wakitumika kama ajenti wa uchaguzi wa CCM.

Umaskini na maisha duni kwa umma na maisha bora kwa watawala. Rejea kurundikana kwa wagonjwa mahospitalini hadi wanne kitanda kimoja na wanafunzi mia darasa moja huku kikundi cha watu wachache kikiogelea kwenye kila neema ambazo ni mateso ya umma.

Uchakachuaji wa haki na hata mafuta. Hili mmeliona kwenye magari ya ikulu na uchaguzi wa CCM. Kila kitu kwa sasa ni kuchakachua!

Uhujumu wa uchumi. Rejea kikundi cha watu wachache kupeana tenda za ujenzi wa barabara na majengo yasiyofikia viwango hasa mashule na zahanati.

Kuwekeza kwenye siasa badala ya maendeleo ya kiuchumi. Rejea ukweli kuwa CCM iko tayari kuwalinda wanasiasa wake fisidi kwa gharama ya uchumi wa nchi na wananchi. EPA na Richmond ni mifano mwanana.

Chanzo: MwanaHALISI Agosti 23, 2010.

1 comment:

Anonymous said...

Heri wewe umesema!