The Chant of Savant

Tuesday 10 August 2010

Ni siku ya kuchakachua na kuchakachuliwa

MWENZENU nimechoka na uhuni unaoendelea kwenye kaya ambapo fisi wanajitahidi eti kuwania kuwasemea kondoo. Sina hamu kwa niliyoshuhudia mwenyewe kwa maninga yangu. Msianze kusonya sonya. Acha niwaeleze kisa.

Si juzi nikajipeleka mwenyewe kwenye rubaa za siasa za gulio la uuzaji wa haki lililopewa jina la kampeni ambazo ziligeuka za uchafuzi na uchakachuzi wa demokrasia, sorry- uchaguzi wa kura za maoni.

Wazungu wangesema the masquerade, some jet-set smoothies call electoral process whilst it is actually monkey biz! Sorry sana waliwa na wadanganyika. Mwenzenu msinihesabu humo. Nipo na kijiwe changu natesa na kupeta. Sina maradhi ya bulimia wala myopia kama nyinyi.

Ndiyo watu walikuwa wanakula kwa kuona na kutoa kura ya kutoona mbele. Sikujua kuwa kumbe kujinyonga si lazima utumie kamba tu. Hata kura yaweza kukunyonga.

Zamani nilikosea kudhani kuwa majambazi ni wale tu wanaotumia bunduki nisijue na kalamu yaweza kuwa silaha hatari hasa ikitumiwa vibaya! Sikujua kuwa kumbe na usomi waweza kuwa ujuha hasa unavyotumika kichwa chini miguu juu!

Nani alijua kuwa majambazi ya wazi kama Endelea Chenga aka Mzee wa Vijisenti, Roasttamu, Bazie Bozo Notimbili, Abdu Kagoda, Eddie Ewassa, Mustafu Mkulu na wengine wangerejeshwa tena bila kupingwa.

Nani alijua kuwa vinyemelezi vya mafisadi kama Janvier Mgosi Makambale, Emmy Nchimvi, na wengine wangerejeshwa?

Nashukuru Mungu matapeli kama Chitaahira wa Chitalilio, Niziro Kadamage na Dororos Camara wametoswa mwongo huu.

Roho iliniuma nilipooana wale madaktari feki walioghushi vyeti wakipeta. Mmewasahau akina Makorongo, Bill Lukuwi, Meli -Nyagu, Chengeni Rafu, Mwambalakaswa na wengine walioghushi mkuu na genge lake wakawakingia kifua kwa vile wanakula pamoja?

Je hawa waliowapitisha hawajapitisha kitanzi chao baadaye? Nyie ngojeni. Wakianza kuwachakachua nisisikie gendaeka akijiliza na kulalamika kama kichanga ambacho hukojoa kitandani kikahanikiza kulaumu na kulia lia.

Hakuna jamii inayopaswa kuhurumiwa kama ile inayojihadaa kwa kugeuza haki bidhaa tena isiyo na thamani kiasi cha kupokwa na majambazi. Niliwaona wengi tena ambao huwezi kuwadhania. Walikuwapo wasomi, wababaishaji hata matapeli tena kwa wingi tu.

Kutokana na jinsi watu walivyomwaga mifweza (chafu na safi), vijisimu, na upuuzi mwingine, nilijifunza kitu kimoja-kumbe kambale wote wana sharubu! Nitaeleza baadaye hasira na mstuko vikipungua siyo kuisha maana haviwezi wakati ndiyo zali linaanza.

Niliona watu na mijitu. Wa mkuu kule wanahonga na wa wadogo nao kule wanahonga kila kinachoweza kufakamiwa na walevi wa danganyika hii. Heri ningejiendea kwenye jamhuri ya pili ya visiwa ambao hawakupoteza muda na uchafuzi bali kura ya maoni ya kuchanganya kondoo na fisi mbuzi na mbwa mwitu. Tuyaache.

Urafiki wa mbuzi na fisi huleta matokeo hatari hasa kwa mbuzi na faraja kwa fisi. Watajuta baadaye baada ya kushindwa kutumiana.

Hakuna kituko kilichoniacha hoi japo hai. Nani angeamini kuwa wale jamaa zetu wa kukuru kakara za kukuza na kudumisha rushwa nao wangeingia na sanaa zao?

Hawakutaka kubaki nyuma katika mechi hii ya kuonyesha ukichaa ufisi na ufisadi wa kila aina. Tukukuru nao wanafunga kamba huku. Kule mitandao ndiyo usiseme hadi kwenye runinga huku rubaa za kimataifa tukimkosa mtalii ambaye kwa sasa amestaafu ili afanye usanii kwa ajili ya muhula mwingine.

Kambale wote wana sharubu kama nilivyodokeza hapo awali. Mdogo anazo, mkubwa na mkubwa sana. Kadhalika kwenye kaya rushwa ni kuanzia chini kwenda juu na juu kuja chini kushoto na kulia. Huyu anajigamba ana bilioni kadhaa.

Rushwa imeshambulia kiwili wili kizima na kukibadili hadi kugeuka kama kansa ya kudumu (chronic cancer) kwenye kiwiliwili ( kaya). Miguu inayobeba mwili mzima (wazalishaji) imeoza. Tumbo (wanaowanyonya wazalishaji) nayo imeoza bila kusahau ubongo (wasomi). Jamii imeoza na kuzidi kuangamia kwa gonjwa hili.

Nani amsaidie nani? Tuliodhani ni madaktari hao ndiyo usiseme. Ni mahututi wa kufa kesho. Baya zaidi tumeridhika na kujiweka tayari kuangamia kwa pamoja kila mmoja kwa siku yake. Tumegeuka mateka wa matendo na mawazo yetu. Anayewatanabahisha wenzake anachukiwa na kuonekana kama kichaa wakati vichaa ni wale wanaopuuzia ushauri.

Tumegeuka kama panya kuguguna kila kitu hata msingi wa kaya! Tumegeuka wa hovyo kuliko hata panya. Maana wao ni hayawani.

Yule ana milioni kadhaa ya kukwapua na kuchangiwa na wezi wenzake hata wasio. Huyu anahonga na kuahidi vyeo kwa wawezeshaji au tuseme walamba viatu. Yule anahonga vinokia, manywaji, makulaji na hata lifti. Ukitaka kuijua hii soma kitabu cha Mpayukaji kitakapotoka kiitwacho NYUMA YA PAZIA.

Utayaona mafisi yanavyosherehekea nyuma ya pazia huku mbele ya hadhira yakijafanya makondoo na njiwa wakati mashetani na minyama mwitu ile ile leo juzi jana na kesho!

Hii ni kansa ambayo imepakwa mafuta na kuitwa mafua ya mauda wakati ni gonjwa tena hatari la kudumu. Vipofu wamegeuzwa waoni wakati ni vipofu. Kwenye kitabu cha SAA YA UKOMBOZI, Nkwazi Mhango ambaye ni pacha wangu anamaliza kitabu kwa swali dogo lakini lenye maana kubwa zuri na zito liulizalo: Je kipofu aweza kumuongoza kipofu?

Mara huyu kakamatwa mara yule kahonga vinokia, mishiko tuliyokuwa tukiwashitakiwa wachora maandishi sasa iko kwa wanuka jasho njaa na ukapuku!

Kila mtu sasa ni mwema na kila kitu ni chema ufalme wa mungu usifike. Mungu mwenyewe siyo Yehova, Allah wala nani bali Mulungula.

Je mungu mulungula anapotawala unategemea nini? Swali la mwisho ni toka katika kitabu cha SAA YA UKOMBOZI. Je kipofu akimuongoza kipofu inakuwaje? Na mwizi akiongoza mwenye mali inakuwaje? Hapa ni sawa na kusema kila kambare ana sharubu CCM
Nasikia harufu ya EPA mpya. Acha niishie kabla ya kulishwa rushwa kwa ajili ya kuniibia kwa miaka mitano.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 10, 2010

No comments: