The Chant of Savant

Wednesday 18 August 2010

Huu ni msimu wa hongo na uongo

JUZI kwenye runinga yangu tena kwa maninga yangu nilimuona msanii mkuu ambaye si vizuri kumtaja jina kwa vile kila mtu anamjua hata ndege akiwafunga kamba wakulima aliowasahau kwa karne!

Sikushagaa. Maana huu ni msimu wa hongo na uongo mtindo mmoja. Waliokuwa wamekutelekezeni sasa wanajifanya wenzenu tena wanaokupenda nusura ya kukata roho kama hawakuoni. Ni mapenzi ya kweli au ya uongo usiniulize. Tumia bongo lako maana bongo bila bongo utaliwa tu tena ukijiona.

Wakati wa kutumia matumbo badala ya ubongo umepitwa na wakati hasa kipindi hiki kigumu cha kutiwa majaribuni.

Baada ya kushuhudia usanii na hii jinai nilijiuliza swali moja kuu-je kwa miaka yote hii ulikuwa wapi hadi leo uwaone wanafaa kama kweli wanafaa ukiachia mbali wewe kuwafaa? Hata hivyo, nilipata jibu kuwa wakati wa kula kwa kura lazima kila sanaa ifanyike ili ulaji wa dezo upatikane. Hapa mtaimbiwa ngonjera na nyimbo nzuri za maisha safi wakati ukweli hakuna cha maisha safi bali ulaji mchafu wa kiroho wa kujuana na kulipana fadhila.

Kuna kipindi huwa nashangaa dharau hii hasa kwa hawa jamaa zetu waliohukumiwa kifungo cha maisha cha mateso kwenye mashamba yetu. Li-sirikali liliwatelekeza zamani na kufunga ndoa na wachukuaji na wafanyibiashara wenye kutia kila aina ya shaka.

Eti leo kiranja wake anakwenda kuwageuza majuha jamaa zangu hawa kwa kuwapa vijijembe vya kisasi, uongo uitwao Kilimo First wakati ni Uchukuaji na Uwekezaji First. Je, hii si kuwageuza shamba la bibi? Je nao hawana hata akili lau ‘common sense’ kujua wanaliwa? Kwa nini wasipokee upuuzi huu ambao mie naona ni rushwa halafu kura wakatoa kwa wale wanaoona wanafaa kama walivyopania kufanya wafanywakazi wa kaya hii?

Nasema hivi kutokana na Wadanganyika kuwa na tabia ya kulalamikalalamika wanapojikuta wamebanwa mkengeni wasijue jinsi ya kujinasua. Utaiona imetoa mimacho kama panya kwenye mtego.

Mnalalamika nini wakati matatizo mengine mnajitakia kwa ujuha na tamaa zenu. Naona lile limetoa mimacho kwa hasira na kutaka kupasuka. Soma au acha lakini vidoge ntakupa. Maana huu ndiyo wajibu wangu kama mtume wa Mungu.

Kwanza, jamaa mwenyewe alishawatolea nje akisema raha mjipe wenyewe yeye awape karaha? Sasa anawafuatafuata nini kipindi hiki cha kuvuna asipopanda kama kweli nyinyi si majuha anayoweza kuyachezea kila mahepe? Mkiambiwa ukweli mnafura.

Ni kweli acheni ujuha mtaendelea kuliwa. Hivyo vijembe, vicheko na tabasamu bila kusahau kupiga picha za kipuuzi pamoja siyo ‘big deal’ ndugu zanguni. Mwaliwa ati hata kama hamtaki kusikia ukweli huu. Narudia mwaliwa ndugu zanguni kengeukeni msiukwae mkenge tena wa mchakachuaji huyu.

Huwa nashangaa mapenzi ya namna hii ya kibubusa na kushtukiza huchipuka wapi! Hivi hao wanaowapa hongo zitokanazo na mabaki ya chumo la wizi kwa nini msiwaulize waliwafanyia nini iwapo kila siku tunapata taarifa za wizi wa kutisha kama ule wa juzi wa 1,700,000,000.

Unajua haya ni madafu ambayo ni sawa na shilingi ngapi? A cool one point seven trilioni! Sorry nimechukia hadi ung'eng'e ukanitoka. Namaanisha shilingi za madafu trilioni moja nukta saba karibu na mbili.

Hizi ukipewa ‘mkulimwa’ unaweza kutumia shilingi milioni moja kila siku kwa maisha yako yote na zisiishe. Unaambiwa hii pesa imeibiwa ndani ya mwaka mmoja. Je ndani ya miaka mitano zimeibwa ‘zillions’ ngapi?

Hapa kitu muhimu kufanya ni kwa waliwa kuchangamkia hongo wanazopewa kuwaaminisha kuwa wanawajali na kupiga kura yako kwa wengine. Maana siku ya siku ikifika ni wewe Mungu wako na kura yako.

Hii ndiyo njia ya wanjanja kuonyesha ujanja wao na sio ukale na ujuha ambao huwafanya wahusika kuwachukulia waliwa kama waliwa tu na si wana kaya wanaostahili kutendewa haki.

Hakuna haja ya kuogopa. Tulishuhudia waliwa wa nchi ya Nyayo miaka ile wakiwapiga chini kina Kanuu kiasi cha kuwatoa kwenye historia za siasa za taifa lile ambalo hivi karibuni limepiga hatua nyingine mpya kwa kuondokana na Katiba viraka kama ya kaya.

Hawa ndio wanaweza kusema ni wajanja ambao hawako tayari kuchakachuliwa na kuchuliwa kama jamaa zangu wa hapa ambapo wamegeuzwa mtaji na mafisidunia wakubwa na wadogo. Upo hapo mwanangu? Kazi kwako.

Mambo yao ya kuchukua na kuweka waa yanapaswa kuwageukia. Nanyi mnachukua mnalamba na mnatoa kura nje ili tuone kama watakula jeuri na longolongo zao.

Nijuavyo huu ni mchezo wa karata tatu. Mara hii mmesahau kisa cha matapeli pale Migomigo ambapo mwenye dhahabu feki alimuuzia mwenzie aliyemlipa pesa feki mchezo ukaishia pale kila mmoja akiondoka anajiona mjanja wakati si kweli?

Kama muhula huu watu watapigwa chini litakuwa somo kubwa na zuri kwa wale wengine watakaopata ulaji wa kutokana na ‘kura’ zenu. Hapa ndipo mtaachana na mauti ya kuku kulishwa nafaka kavu akazalisha mayai yenye virutubisho lukuki asiyokula.

Kuku hula asichozalisha na kuzalisha asichokula kwa vile ni kuku. Mwajua ni kwa nini? Kuku kanyimwa ubongo. Maskini hayawani huyu! Ubongo wake haujai hata kijiko atawezaje kung'amua mambo kama nyinyi wenye bongo zinazochemka lakini mkatendewa kama kuku nanyi mkajirahisisha?

Juzi nilikumbuka mambo mengi. Nilikuwa napitia album yangu ya kale na kumuona mzee Musa Mchonga akisaidiana na wananchi-enzi zile-kujenga majengo ya shule, dispensari na mambo mengine. Alikuwa akichapa kazi kavu kavu.

Baada ya kuvuka ukurasa huo niliangalia picha za mkuu wetu bin Sharmutah akifanya kama mzee Musa. Ni mbingu na ardhi. Nani angeamini jamaa anashika ‘kurego’ ilhali kapiga magoti kwenye mkeka ili asichafuke?

Ukilinganisha viumbe hawa wawili ni sawa na kuwalinganisha Lusifa na Yesu au Abujahari na Mtume Mohammad. Hayo tuyaache. Kazi kwetu kutumia akili vizuri siyo kama kuku wa kwenye kisa hapo juu.

Muhimu ni kukubali na kuelewa kuwa msimu wa kuliwa tena bila kunawa wala kuomba ndiyo huu na habari ndiyo hiyo. Nasikia harufu ya wizi wa kula.

Du! mbona yule kavalia kama ndata! Acha niishie kabla sijamkata mitama. Maana siku hizi nawaonea kama sina akili nzuri. Ya kweli hayo? Tusichimbuane wala kuchakachuana.

Khalas kweisine.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 18, 2010.

1 comment:

Mzee wa Changamoto said...

Mwl umewaza vema. Nami niliwaza NYAKATI hizi na kuziandika hapa http://changamotoyetu.blogspot.com/2010/07/them-i-themhypocritesnasio-fontaine.html