The Chant of Savant

Wednesday 5 May 2010

Kikwete wa kweli alipojifunua



NILIWAHI kuandika makala kuwa Rais Jakaya Kikwete ni mtu mwenye masikio madogo na kinywa kikubwa, nikimaanisha anasema mengi na kutosikia lolote.

Hii ilitokana na Kikwete kutupiwa tuhuma nyingi na asijibu hata moja, ukiachia mbali kupuuzia ushauri wa kuwawajibisha wasaidizi na wateule wake waliobainika wazi kushiriki vitendo vichafu vya kifisadi.

Kwa wanaokumbuka Kikwete alivyopuuzia ushauri wa Watanzania kumtaka awafukuze wasaidizi na wateule wake waliotuhumiwa kughushi vyeti na kupoteza pesa za umma, wanajua nimaanishacho.

Kwa wanaokumbuka jinsi Kikwete alivyokataa kujibu tuhuma zilizotolewa na wapinzani hata wazee maarufu wa chama chake kuwa ushindi wake uliwezeshwa na kupatikana kutokana na pesa za EPA, ukiachia mbali kuwa mtumwa wa mafisadi kama alivyosema mzee Joseph Butiku, wakati wa kongamano la kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Novemba mwaka jana.

Hata mashambulizi haya mazito yalipotoka, Kikwete alijitahidi kutojibu huku akiwaacha, Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, ajibu kwa hoja nyepesi na kashfa ambazo kwa kiasi kikubwa zilimshushia heshima mzee Makamba.

Tangu alipoingia madarakani mwaka 2005, Kikwete alijitahidi kutojionyesha alivyo, akiacha ile sifa ya uchangamfu na ukaribu kwa watu wa kada mbalimbali.

Hata hivyo, sifa hii ilianza kuingia walakini alipoanza kuwa mbali na watu huku akitumia muda mwingi ziarani ughaibuni kiasi cha wakosoaji kusema nchi ina ombwe la uongozi.

Katika hili walimtaka Kikwete afanye maamuzi mazito badala ya kukimbia matatizo kwa ziara za ughaibuni ambazo zimelalamikiwa kula pesa ya umma bila sababu.

Hakuchi hakuchi kuchele! Juzi baada ya kutoalikwa kwenye kilele cha Sikukuu ya Wafanyakazi Mei Mosi na tishio la mgomo wa wafanyakazi nchi nzima, vilimfikisha ukingoni, kiasi cha kukutana na wazee wa Dar es Salaam haraka haraka na kurusha makombora ambayo yalitafsiriwa kama kuishiwa subira, ukiachia mbali Kikwete wa kweli kudhihiri.

Hili lilikuwa ni kombora la aina yake kwa Kikwete kutokana na aina ya lugha na hadhira alivyotumia.

Alikaririwa akiwashambulia wafanyakazi na hasa viongozi wao akisema: “Mie ndiye mwajiri mkuu nisikilizeni mimi, msimsikilize Mgaya (Kaimu Katibu Mkuu TUCTA) mtafukuzwa kazi wala Mgaya hamtamuona! Mtapoteza haki zenu…akili ni nywele, kila mtu ana zake, mtu mzima dawa.”

Licha ya kutofaa, kauli hii itafsiriwa kama tishio kwa wafanyakazi na shambulio binafsi kwa Mgaya.

Kwa wanaojua dhima, heshima na uzito wa taasisi ya urais, licha ya kushangaa walisikitika kuona rais anajishusha hadi kushutumiana na mtu mdogo kwake.

Kwa wanaokumbuka shutuma lukuki kwa marehemu Baba wa Taifa zilizorushwa na Christopher Mtikila, kuwa Mwalimu alikuwa Mrundi na upuuzi mwingine, Mwalimu alipotakiwa kujibu tuhuma aliwakemea waliomshauri hivi kwa kuona kuwa hawakuwa na busara.

Kwani angeanza kujibishana na Mtikila, heshima yake ingeshuka na Mtikila kuwa maarufu.

Kwa mzee mwenye busara, mtoto anapokutukana huwa humjibu, kwa kuogopa kuonekana mtu mzima hovyo.

Hata kichaa akikuvua nguo huwezi kufukuzana naye. Utalinda heshima yako kiakili.

Ushahidi wa hili unaweza kuliona kwenye majibu ya Mgaya baada ya kushambuliwa na rais.

Alikaririwa akisema kuwa kitendo cha rais kumsema mbele ya hadhara kimemuongezea umaarufu mkubwa kwenye jamii.

Hii maana yake ni kwamba amejishushia heshima, ingawa Mgaya hakutaka kuonekana asiye na busara kwa kusema hivyo wazi wazi.

Aliongeza kuwa Rais Kikwete, alipaswa kutambua kuwa yeye ni kiongozi wa nchi, ambaye hatakiwi kutoa maneno kama kiongozi dikteta.

Wengi waliosikia maneno ya viongozi wa wafanyakazi kwenye kilele cha Mei Mosi walishangaa kusikia makombora ya Kikwete.

Kwani walikuwa wameweka bayana wasivyo na ugomvi na Kikwete, bali watendaji wake, japo hakuna tofauti kati ya watendaji na aliyewateua.

Walishangaa sana kuona alivyowalipa.

Bila kupindisha maneno, ukweli ni kwamba rais alijishusha sana na kuamua kujibizana na kiongozi wa wafanyakazi, kwa sababu tu ya kutetea masilahi ya taasisi yake.

Ningekuwa yeye, hiki kingekuwa kitu cha mwisho kufanya. Kikwete alipaswa kutoa majibu ni kwanini wafanyakazi hawakupaswa kugoma na si kuwatisha.

Maana kugoma au kutogoma ni haki yao ya kikatiba. Rais hapaswi kufinya au kuteka haki za kikatiba za raia. Bila wao hana lolote.

Anawahitaji raia kuliko wanavyomhitaji, hasa kipindi hiki kuelekea uchaguzi, ambapo serikali ya Kikwete haijawaridhisha wengi. Rejea kughubikwa na tuhuma za ufisadi, matumizi mabaya ya fedha za umma, kutotimiza ahadi zake, kutotoa majibu ya maswali yanayoulizwa na wapiga kura na wananchi na mengine mengi.

Kama kuna mtu alimshauri kujibu mapigo kwa staili ile, amempoteza na huyu si mshauri bali adui yake.

Kilichotakiwa hapa ni hekima na subira na si kutishana. Maana hata kama rais ni mwajiri mkuu kama alivyosema, hizo kazi anazoajiri watu si zake bali za wananchi waliomwamini kumpangisha Ikulu kwa muda tu.

Hivyo, rais hakupaswa kukwepa jukumu na wajibu wake wa kupokea na kuyatatua matatizo na malalamiko ya wafanyakazi.

Je, alitaka waende kwa nani iwapo watendaji wake walifeli? Kama alivyosema yeye ni mwajiri na kiongozi aliyekasimishwa dhamana na umma.

Japo Kikwete kaishawatibua wafanyakazi, anapaswa kutumia busara zaidi kuliko vitisho.

Maana hata nchini Ufaransa (1848) na Urusi (1917), wafanyakazi walipotishia kugoma, watawala kwa kiburi waliwakejeli na kuwatisha, hatimaye wakatupwa nje na kubakia historia ya kutia kinyaa.

Kwa wale walioaminishwa wakati wa kampeni kwamba Kikwete ni mtu msikivu, mvumilivu, tumaini lililorejea na sifa nyingine kemkemu, sasa wana picha tofauti baada ya Kikwete wa kweli kujifunua kwao.

Nimalizie kwa kumnukuu nabii Paulo, Wagalatia 3:1 akisema: “Enyi Wagalatia msio na akili ni nani aliyewaroga; enyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu...?”

Kwa vile Kikwete wa kweli amejifunua, wafanyakazi wekeni nukta.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 4, 2010.

No comments: