The Chant of Savant

Tuesday 27 April 2010

Tuwaepushe First Ladies wetu na ukupe



Nakumbuka. Nilianzisha mjadalala juu ya utata kuhusu shughuli na maisha ya wake za marais-first ladies wa kiafrika. Ezekiel Kamwanga ameuboresha na kuudurusu kwa undani kwa kuzama kwenye historia kiasi cha kunishawishi nirejee hoja hii lau kuongeza utamu. Nitachukua mwelekeo tofauti ambapo marejeo yangu si historia bali kinachofanyika kwenye nchi ninayoishi-Canada.

Kuna , shuku, mkanganyiko hata hasira kuhusiana na maisha aghali yasiyo ya kikatiba ya wake za watawala wetu. Hivyo, leo nitaangalia maisha ya mke wa waziri mkuu wa Kanada; nchi ambayo haina rais. Hivyo hapa mke wa waziri mkuu anasimama sawa na mke wa rais yeyote wa kiafrika-First lady.

Kwanza lengo la makala si kumshambulia mtu bali kuangalia utata huu wa kikatiba unaosababisha hasara na hata umaskini wa kunuka kwa mataifa mengi maskini ya kiafrika. Kwa maana nyingine nalenga kumpunguzia mzigo mlipa kodi maskini katika nchi za kiafrika ikiwemo Tanzania.

Kutembea ni sehemu ya kujifunza. Hivyo, si vibaya kupeana uzoefu baina ya Kanada na nchi zetu maskini ziishizo kwa kuomba omba na kukopa kopa huku zikitawaliwa na watawala matajiri kupindukia hata kuzidi wale wanaozifadhili.

Ukimuuliza Mkanada wa kawaida jina la mke wa kiongozi wake ambapo kwa Kanada ni mke wa waziri mkuu, atakushangaa na kukosa jibu. Kwani kwake mke wa waziri mkuu siyo sehemu ya utawala wa nchi yake bali raia sawa na wengine.

Kama Mkanada huyu atakuwa na jibu la swali lako, atakujibu kwa swali: mke wa waziri mkuu ni nani katika nchi hii hadi akupasue kichwa au kukushughulisha? Binafsi niliwahi kupata jibu hili nilipotaka kujua maisha ya mke wa waziri mkuu wa Kanada Bi. Laureen Teskey Harper

Kusema ukweli, mke wa waziri mkuu hapa hana mamlaka yoyote kikatiba na kimaisha. Wala hajulikani eti kwa sababu mumewe ni kiongozi wa nchi. Wala hana ushufaa na misafara ya magari kama Afrika. Hana walinzi wala ukwasi na hata hatoi kauli za kisiasa wala kuonekana kwenye vyombo vya habari na sehemu mbali mbali za nchi ukiachia mara chake kuandamana na mumewe. Hana hata NGO ya kuhudumia sijui akina mama au watoto. Kama akitaka kuwa mwanasiasa, inampasa kupambana sawa na mtu yeyote kufikia kwenye ukuu na siyo kudandia mgongoni mwa mumewe.

Kama alikuwa mwalimu, daktari, mhasibu au mama wa nyumbani, ataendelea kuwa hivyo hata kama mumwe ana madaraka. Na anajisikia vizuri kuwa hivyo. Utamuona mitaani akipishana na wananchi wa kawaida kama mwananchi wa kawaida. Kuna kipindi wakosoaji wa waziri mkuu wa Kanada, Stephen Harper waliwahi kumrushia kijembe kuwa mkewe ni mpanda pikipiki. Harper aliwajibu kuwa kweli mke wake ni mpenzi wa kupanda pikipiki na hayo ni maisha yake. Hili liliwajengea heshima kubwa Harper na mkewe. Kwani walipa kodi wa Kanada wasingevumilia kumuona mke wa Harper akiwanyonya kisa eti mumewe ni waziri mkuu.

Kwa mke wa waziri mkuu cheo cha mumewe ni cha mumewe siyo chake wala hana haja ya kukidandia kuishia au kutegeneza pesa kama ilivyowahi kutokea kwenye awamu ya tatu Tanzania ambapo mke wa rais mstaafu, Benjamin Mkapa alianzisha NGO yake na kujiingizia pesa nyingi baada ya mumewe kuingia madarakani. Bahati mbaya mchezo huu ambao wengi huuona kama ufisadi umerithiwa na mke wa rais wa sasa!

Kubebwa au kudandia madaraka ya mume hapa Kanada huchukuliwa kama ufisadi, kutojiamini na ubaguzi wa kijinsia. Kama mama anataka madaraka basi afanye kama mke wa dikteta wa Uganda, Yoweri Museveni aliyeamua kugombea ubunge. Au hata mke wa rais wa Argentina, Bi. Cristina Fernández de Kirchner ambaye sasa ni rais baada ya kuchukua madaraka kwa kuchaguliwa kikatiba toka kwa mumewe, Fernández de Kirchner.

Nimelazimika kuandika makala hii baada ya kuona utata unaozunguka tabia na maisha ya wake za watawala wa kiafrika. Nchi ya jirani ya Kenya, mke wa rais, mara mbili, alifikia hatua hata ya kuwazaba makofi wananchi wa kawaida-waandishi wa habari. Ambapo mara ya kwanza alimzaba vibao mpiga picha wa The Daily Nation na mara pili MC katika sherehe fulani kwenye viwanja vya ikulu. Ilikuwa ni aibu na mshangao ambavyo vilimgharimu mumewe, Mwai Kibaki, ambaye urais wake hadi sasa unasemekana ulipatikana kutokana na wizi wa kura. Hii ni baada ya wananchi kulipizia kisasi kutokana na tabia mbaya na uvunjaji wa katiba na haki za binadamu wa mkewe.

Nchini , karibu kila kashfa inayomhusu rais mstaafu Mkapa inamhusisha mkewe pia. Wengi wanaualiza mantiki ya kutomfikisha mke huyu wa rais iwapo hana kinga kama mumewe ambaye ameponyoka kutokana na kuwa na kinga na wale waliomfuata kufanya kama alivyofanya yeye.

Kitu kingine kilichonisukuma kuandika makala hii juu ya wake za watawala wetu, ni misafara ambayo nimewahi kuishuhudia jijini Dar es salaam na kwingineko hasa wakati wa maonyesho ya saba saba ikiwa ni ya wake za marais. Hawa wanapata wapi fungu la kutumia misafara na walinzi namna hii wakati katiba yetu haina kipengele hata kimoja kinachozungumzia cheo cha first lady? Je huu siyo ufisadi na kumtwisha mzigo mlipa kodi wetu maskini? Je rais anajua kuwa hali hii inachafua madaraka yake? Je nao wake za marais wamekuwa hoi kiasi cha kudandia madaraka ya waume zao? Mbona wakati wa kuchagua na kuapa alichaguliwa mtu mmoja yaani mume?

Mke wa waziri mkuu wa Kanada hufanya shughuli zake kama mke wa mtu. Akitumia piki piki yake huenda hata kuwachukua watoto wake Benjamin na Rachel shule. Je ni mke wa mtawala gani Afrika anaendea watoto wake shule zaidi ya mashangingi ya serikali? Je huu siyo wizi wa kawaida anaofanyiwa mlipa kodi maskini?

Hata Wakanada wanampenda na kumheshimu mke wa kiongozi wao kwa vile yeye siyo mzigo kwao wala haonekani kuwanyonya kwa kutumia cheo cha mumewe. Kwanini na wake za watawala wa kiafrika wasifuate mfano huu maridhawa ambao unawaongezea heshima badala ya kuonekana kama wadandizi na wezi kupitia migogo ya waume zao?

Mke huyu wa waziri mkuu anaishi maisha yake sawa alivyokuwa akiishi kabla ya mumewe kuingia madarakani. Ahitaji makandokando ya watawala yaani misafara na walinzi kwani hamuogopi mtu na hamuiibii mtu. Je wake wa watawala kiafrika wanamuogopa nani?

Mke wa waziri mkuu wa zamani wa Uingireza Tony Blair, Bi. Cherie Blair ni mwanasheria kama alivyo kabla ya mumewe kuwa kiongozi. Aliwahi kushitakiwa na kupigwa faini kwa kutolipia tikite kwenye treni jijini London. Je ni mke wa mtawala gani anapanda treni na kujilipia nauli? Je tunawafadhili wake wa wakubwa kwa utajiri gani wakati sisi ni omba omba wa kunuka tunaotegemea wafadhili?

Kingine kilichonisukuma kuandika makala hii ni kile kilichotokea katika mji mkuu fulani wa nchi ya Ulaya. Mtawala mmoja wa kiafrika alikuwa ziarani katika nchi fulani. Alipata fursa ya kusalimiana na kuongea na raia wa nchi yake waliokuwa wakiishi nchini mle. Alipomaliza kuongea, mkewe aliyekuwa ameandamana naye kwenye ziara hiyo, alipewa fursa ya kuwasalimia wananchi. Alianza na maamkuzi ya chama chama chake. Wacha wananchi washangae na kuchukia. Maana wote hawakuwa wanachama wa chama cha mumewe. Ilibidi mumewe amkatize kwa kusema. "Unadhani wote ni wanachama wa chama cha mumeo?" Ilikuwa ni aibu ya mwaka ingawa kutokana na mazoea machafu ya watawala wetu hawakulichukulia hili kwa uzito uliostahili. Mbali na hii nimelijadili hili kwenye kitabu changu kinachotarajia kutoka cha NYUMA YA PAZIA na kuligusia kidogo kwenye kitabu kipya ambacho kipo mitaani cha SAA YA UKOMBOZI.

Kuna kitu kingine kuhusiana na mke wa waziri mkuu wa Kanada. Nacho ni haandamani na mumewe katika kila ziara azifanyazo nje ya nchi. Maana kufanya hivi ni kumtwisha mzigo mlipa kodi. Ikumbukwe. Walipa kodi wa Kanada ni matajiri kuliko wa kwetu. Lakini bado wanapinga viongozi wao kutumia madaraka waliyopewa na umma vibaya.

Matukio haya mawili yaani lile la Lucy Kibaki anayeitwa Tyson na la mke wa waziri mkuu wa Kanada, yanaweza kuonyesha ni kwa jinsi gani uwajibikaji na matumizi mazuri ya pesa ya umma lilivyo tatizo katika bara la Afrika. Wachambuzi wengi wanakubaliana kuwa tatizo la umaskini barani Afrika linachangiwa na ufisadi kama huu kuliko hata majanga ya kimaumbile au kutokuwapo mlingano katika biashara na nchi tajiri. Hapa hatujagusia serikali kubwa zisizo na ulazima za waume wa wadandizi hawa. Hatujagusa familia zao na marafiki na walamba viatu wengine waliojizungushia wanaolipwa na kodi ya makapuku wetu.

Katika hili kama siyo kichwa ngumu na uchoyo, ushamba na roho mbaya, Afrika hasa Tanzania ina pa kuanzia. Baba wa taifa hili hakuwahi kumruhusu mkewe Bi. Maria Nyerere kudandia madaraka yake wala kuanzisha NGO za uongo na ukweli ili kupata pesa haramu ya haraka. Hata leo bibi huyu anaheshimika kuliko wake wa marais wote waliwahi kuitawala nchi hii.

Hata hivyo katika nchi nyingi za kiafrika, kuna nafasi isiyo rasmi ya mke wa rais, waziri mkuu na hata makamu wa rais kuyatumia madaraka ya waume zao kuwaumiza walipa kodi. Wengine wanakwenda mbali hadi kutumia ofisi za waume zao kufanyia biashara kama tulivyoona kwenye mfano wa mke wa Mkapa.

Kuna tatizo jingine. Nalo ni watoto wa watawala kuwa watawala wadogo. Nchini Kenya wakati wa utawala imla wa Moi, watoto wa Moi walikuwa kama marais wadogo kiasi cha kujichotea mabilioni ya shilingi toka kwenye hazina ya nchi hiyo sawa na ilivyotokea hivi karibuni kwa mtoto wa rais mstaafu Mkapa aitwaye Nicholas pamoja na mkewe Foster walioanzisha kampuni ya Fosnik kwa pesa inayosemekana ilipatikana kifisadi.

Je kuna haja ya kuruhusu wake za watawala wetu kulewa madaraka kama Lucy Kibaki au kutumia ofisi zetu kutafutia mtaji kama Anna Mkapa?
kwa vile kila mwananchi ni mdau wa maendeleo ya nchi yake lengo la makala hii ni kuonyesha dira ya nchi yetu. Tumpe changamoto rais wetu na walipa kodi wetu kupiga vita wizi huu wa madaraka ambao ni kinyume kabisa na katiba. Na katiba yetu, ikibidi, itamke wazi kuwa mtu yeyote anapokuwa rais basi asitumie madaraka yake kiubia na familia yake au marafiki zake. Maana kufanya hivyo ni kuihujumu nchi na kuiongezea umaskini. Hata ziara za rais zisiwe sehemu ya mkewe kufanyia utalii wa kuijua dunia.

Katika sakata la ufisadi linalomkabili rais mstaafu Mkapa wapo wanaouliza mantiki ya mkewe, mtoto wao na mkazamwana na marafiki zao kutoshughulikiwa. Maana tunaambiwa Mkapa ana kinga. Je hawa nao wana kinga? Iko wapi katika katiba yetu? Je wake za watawala wetu hawaishi kifisadi bila ya wao hata sisi kujua?
Chanzo: MwanaHALISI April 21, 2010.

2 comments:

Anonymous said...

Well said Mkwazi! Well said, indeed.

Njonjo OK said...

Huna hoja, kimsingi unachosema ni kuwa tufanye vile kama wa Canada. what makes them better than us? why not them copying from us?