The Chant of Savant

Friday 2 April 2010

Msimu uwa kula bila kulipa umewadia

NDIYO natoka kupuliza mabangi yangu. Natembea kama vile napaa nikiwaza jinsi ya kutumia na kutanua huku majuha wakiniramba miguu. Nina mpango kabambe wa kuukata baada ya kugundua njia rahisi katika ulimwengu wa majuha.

Napiga mbinja kama sina akili nzuri. Nahanikiza ifuatavyo:

Pesa, pesa, pesa kweli sabuni ya roho nasema.
Mwenye pesa, mwenye pesa kweli si mwenzio - we juha.
Ukinyaka pesa unaweza kulala kwenye ghorofa.
Ukiwa na pesa waweza kuwa raisi-wa majuha.
Ukiwa na pesa utakuwa mwizi wa miwa -mheshimiwa.
Ukiwa na pesa unaweza kuhonga majuha wakakupa kura ya kula - nasema.
Pesa, pesa, pesa kweli sabuni ya roho nasema.
Mada madaraka nayo ni kinga ya mengi.
Ukiwa nayo, wajificha nyuma yake.
Jambazi na muuaji aitwa mheshimiwa.
Kibaka na poraji, pia ni mheshimiwa.
Matapeli ya kughushi
Yaitwa waheshimiwa.
Muuzaji wa madawa hata mie mvutaji.
Waitwa mheshimiwa kisa una madaraka.
Tilitiliiii tilii tilliiiiii ngwili ngwililiiiii.

(Rudia kwa sauti na fikra mara tano).

Ni kweli. Ukiwa na fedha hata uwe fala hata choko na changu utaonekana mjanja. Ukiwa na madaraka ndiyo usiseme. Kila mchumia tumbo atakuramba viatu ili ajaze box lake aliitalo tumbo.

Ukiwa nazo wewe ni kila kitu. Ukiwa na madaraka unaweza kukufuru hata kujiona mungu mtu. Hata mkeo atakuwa mwenye madaraka na watoto wako watakuwa wateule hata kama ni vibaka.

Nimekumbuka shosisto mmoja anayetanua hata na midege na mishangingi ya kaya kwa vile bwana’ke ni mkuu. Nani alitarajia chinga kama yule kutanua vile na utaalamu wake wa chaki, tena wa shule za vidudu?

Mara hii mmemsahau jamaa yangu aliyejaza mke, watoto na ndugu zake kwenye ulaji kwa vile ana madaraka? Hana tofauti na mfalme.

Mmesahau Tunituni alivyowajaza vivyele na wakwe zake kwenye ulaji wa umma kwa vile alikuwa na madaraka? Madaraka ndugu yangu usifanye mchezo.

Ukihoji hili jikumbushe. Inakuwaje kitoto cha miaka kumi na ushei kinaula kwenye siasa wakati kinapaswa kuwa skuli kikijifunza mambo?

Kwani haya hayapo na hayafanyiki mbele ya macho yenu walevi nyie tena mkishangilia na kutangaza upuuzi huu bila kuchukia na kuchukua hatua?

Nani aliwaroga nyie ambao kila kitu kiko wazi mbele yenu?

Mna habari wimbo huu niliutunga mimi na kuimbwa na jabari la muziki almarhumu Marijani Rajabu aliyekuwa mshirika wangu enzi za Dar International na mtindo wetu wa ‘supa bomboka’ uliogeuka kuwa supa homola?

Ubeti wa pili haukuimbwa kwa kuogopa wenye madaraka kipindi kile hasa mzee mcho... wee koma! Hayo tuyaache.

Kwa vile majuha wanaamini kila upuuzi kiasi cha kuwa na matumaini hata yasipokuwapo, nitaunda kampuni hewa iitwayo Nimajuha Tunawala Kyoei yenye makao makuu kwenye prefecteur ya Nakagawa kule Ujepu. Baada ya hapo nitakwenda kwenye mabenki na kuhomola kama sina akili nzuri.

Nitasuka mipango na majuha wenye mamlaka kuwa tukiishapakua pesa toka kwenye mabenki yao basi wataula na kuwa wakuu. Nitawakaanga samaki kwa mafuta yao kutokana na ujuha wao.

Polisi wala TAKULA msipoteze muda kuniandama. Mie nitakula na mabosi wenu. Ukijitia kunifuata fuata tunakufukuza kazi. Nitawasiliana na Ewassa, Roast Tamu, Endelea Chenga na Iddiiliisha kwa Rashid tufanye vitu vyetu.

Wale watu wa mabenki ya kijambazi yanayowaibia majuha na walevi kaa chonjo. Kuna jogoo limeingia mjini kuwaliza. Bell of Tembo au Bunch of Thieves kaa sawa hamtaniepa kama EPA. Lazima nijikate pale BoT na kuhomola na kisifanyike kitu.

Nina kampuni mpya ya hapa kayani iitwayo Kagodo na ninakula na wakubwa wenu uchwara wenye tamaa kama fisi na ujuha kama kenge, ambaye akiona mvua inanyesha hukimbilia majini asijue mvua ni nafuu kuliko ziwa au mto! Ninao vifaa ndani ya mabenki yenu wakifanya ubeki wa kuyaibia mabenki uchwara.

Nina mpango wa kuagiza na kuingiza mashine ya kuchapisha pesa bandia na shahada za kula. Hapa mafisi watakao ukuu hawawezi kupona. Sina shaka na ufanisi wa mradi huu.

Hata ule mradi wa kuchomeka vipengele kwenye sheria nimeubuni mimi ili kuwasaidia wachovu waukwae name niule. Hivyo msimuandame mkuu wa kaya pale pakuu. Mie ndiyo karukarange niliyeanzisha mchezo mzima na kuusimamia kwa faida zangu binafsi.

Mie ni bora kuliko wale waramba viatu wehu wanaowaita wenzao wehu wakati wehu ni wao.

Mgosi Machungi wa Jose Makambale upo hapa? We ni mchovu. Huna kisomo ukiachia mbali busara zaidi ya kujikomba kama changu. Elewa hilo. Unapaswa kuwa ile mitaa yetu si Lumumba wala Idodomya.

Hata wale wachovu mnaowaita waheshimiwa ingawa hawana heshima zaidi ya uheshimiwa wa per diem, msiwalaumu. Wengi ni vihiyo walioghushi shahada zao ingawa wanalindwa na waharifu wenzao wenye madaraka.

N’shasema, madaraka hufanya hata fala kuwa mjanja ukiachia mbali limbukeni kuwa kiongozi. Nyuma ya kila kitu nipo mimi kidume hata kama ni mvuta bangi.

Bangi nivutayo ni kwa ajili ya ukombozi. Na ulevi nilio nao ni kwa ajili hiyo. Japo wehu wengi wananiona mwehu, nina hoja kuwa tunahitaji ukombozi wa kweli. Ukombozi umefika kwenye nyumba ya Mpayukaji shangilieni na kusherehekea hata kama ni mauti yenu.

Juzi shehena Ubwabwa alitabiri kuwa hakutakuwa na uchafuzi na wenye majina yanayoanza na herufi “s” wataula asijue wengine wameishaliwa! Yuko wapi rafiki yangu Sixx zaidi ya kuishia kuwa pumba tupu?

Kadanganywa na Sefuri Madevu na Karumekenge aliyemtabiria kuwa ataendelea kuula. Akijidanganya na kudanganyika ajiandae kwenda kunyea debe na kina Chazi Teillar na baadaye Hummar Bashari wa Sudan.

Mie natabiri. Kama Karumekenge ataendekeza tamaa na taashwisi za Madevu, amini natabiri. Atanyea debe na hawara yake mpya.

Wanadhani hatujui kuwa makubaliano na matambuano na matambiano wanayotutambia nayo kwa kutambuana kinafiki kumesababishwa na EU? Tunajua kila kitu ingawa hatusemi.

Mkakati mwingine niliopanga ni kuhimiza wakimbizi wapige kula ili majuha wenu wale. Kama hamjui jueni. Kule makambini wakimbizi wamekuwa wakitumiwa kupiga kula.

Hii ndiyo siri ya ushindi wa vishindo vyenye kualika mshindo baada ya kimya kingi cha walevi wanaoanza kuamka. Wajinga ndio waliowao. Mwalimu wangu Daktari Slaa usinibaini. Nikipata kumi, tano zako.

Msimu wa kula bila kulipa unawadia. Kaa chonjo saa mbaya walevi mtaliwa sana siyo kama kule nyuma. Vyangudoa wa kihabari na kisiasa wataanza kuhama kambi. Naona majagu yanakuja upande wangu na jana nilikuwa na RB, ngoja niwatoke
Chanzo: Tanzania Daima.

No comments: