The Chant of Savant

Friday 2 April 2010

Hoja ya Slaa isijibiwe kisiasa

KUGUNDULIKA kuwa kuna vipengele vililingizwa kwenye muswada ambao umeishajadiliwa na Bunge na kupitishwa na kusainiwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa sheria, ni jinai ya aina yake na pigo kwa rais na waliomzunguka, ukiachia mbali kuwa kashfa na udhalilishaji wa aina yake kwa Bunge letu.

Ingawa jana Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika taarifa yake iliyotoa msimamo wa serikali alisema hakuna kilichokosewa, jamii haijaelewa hasa kutokana na kauli yake ya kwanza ya kukiri kuwapo kwa vipengele vilivyochomekwa nje ya Bunge.

Jinai hii iliibuliwa na mbunge machachari wa Karatu-CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, ambaye ni Katibu Mkuu wa chama tajwa. Pia ameonyesha umakini mkubwa katika kufuatilia mambo licha ya kuwa tishio kwa serikali.

Dk. Slaa alikaririwa akihoji: “Bungeni hatukusema nani anatakiwa kukagua timu ya kampeni ya nani, lakini kwenye kipengele ambacho kimo kwenye sheria iliyosainiwa na rais inaonyesha kwamba timu za kampeni za mgombea urais zinatakiwa kuhakikiwa na Msajili.”

Aliendelea: “Katika sheria iliyosainiwa na rais kuna kifungu cha 7 (3), ambacho hakikuwepo kabisa kwenye muswada uliojadiliwa na kupitishwa bungeni. Kwa kweli nimeshangazwa sana kwa sababu rais amedanganywa katika hili.”

Slaa aliendelea: “Timu za kampeni za mgombea ubunge, zinaonyesha zinapaswa kuhakikiwa na makatibu tawala wa wilaya na kwa kesi ya wagombea udiwani, timu zao za kampeni zinapaswa kukaguliwa na makatibu tarafa, nani kaichomeka hii?”

Hebu angalia ubabaishaji na majibu ya kisiasa ya anayepaswa kuwa mtaalamu wa sheria, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Fredrick Werema aliyekaririwa akisema: “Kama kweli ikithibitika, tuko tayari kuomba msamaha na kurudisha bungeni suala hili ili lifanyiwe marekebisho… namhakikishia Dk. Slaa kuwa tutarudisha bungeni ili makosa hayo yaondolewe.”

Suluhu si kuondolewa kifungu husika bali kuwajua waliovunja katiba na kulidhalilisha Bunge na kuwahujumu wananchi. Werema hataki hili kwa sababu ajuazo!

Kama kuna aibu ambayo imewahi kumkumba Rais Kikwete, hii basi ni mama ya aibu zote. Hata ile ya Arusha ni cha mtoto. Inakuwaje rais makini anasaini muswada uliobunguliwa na kuwa sheria asivunje sheria?

Je, katiba yetu inasemaje kuhusiana na jinai hii? Je, ni nani hawa waliochomeka upuuzi wao kwenye muswada huu na kwa ajili ya nani? Je, imekuwaje wakajiamini kutenda jinai hii?

Je, ni kwa sababu wanajua wanavyowasaidia wakubwa hivyo kutoweza kuwawajibisha kama walivyofanya kwa mafisadi wa EPA, Kagoda ikiwa baba yao?

Je, walitumwa na Kikwete mwenyewe au chama chake? Vyombo vya habari vilikaririwa vikisema kuwa rais alifura kutokana na kashfa hii.

Jibu hapa si kufura. Ni kujiuzulu au kuwawajibisha wanaohusika na jinai hii ambao bila shaka wanajua upole wa Kikwete na mfumo wetu chakavu wa wakubwa kutumia madaraka vibaya wakijua wako juu ya sheria.

Ingawa Kikwete huwa hajibu tuhuma, katika hili itashangaza kama atakaa kimya kwani ni kashfa inayomuonyesha kama rais asiye makini.

Je, kiongozi wa aina hii si hatari kwa taifa kuliko hata hao wanaomtumia? Je, ina maana rais huwa hachukui muda kusoma masuala anayoletewa atie saini?

Mbona anapata muda wa kuongea na kina Didier Drogba na kusafiri nje? Je, kiongozi wa namna hii anatufaa kwenye karne ya 21 yenye kila aina ya ujanja na changamoto?

Hawa waliotenda jinai hii hata kama wanafahamu udhaifu wa rais, wanamdharau, wanalidharau Bunge, wanawadharau Watanzania kwa ujumla na hata wakitaka wanaweza kuiangusha serikali.

Wamemgeuza rais kama mtani wao. Hata hivyo, rais alionywa kuhusiana na uteuzi wa wasaidizi wake. Alionywa kuhusu ubaya wa kuchanganya urafiki na shughuli za umma, leo hii hayo yanayomkuta ni malipo ya kadhia hiyo.

Kosa kama hili lingetendwa kwenye nchi zilizoendelea, hakuna shaka rais angewafukuza wahusika siku hiyo hiyo.

Kwa vile watu wetu huwa wanaonekana kama walevi wa madaraka, waliohusika kwanza hawajulikani na wanaendelea kutanua.

Wazee maarufu wa CCM waliwahi kushauri rais asiruhusiwe hata kugombea muhula wa pili, wakakaripiwa na kuitwa wendawazimu.

Hapa kuna tishio jingine. Kama serikali ya Rais Kikwete inaanza kupotosha na kuvunja sheria hivi, je, kwenye uchaguzi itakuwaje?

Kimsingi, huu ni ushahidi kuwa serikali haina udhu wa kuweza kuendesha uchaguzi huru na wa haki. Wizi tuliozoea kwenye chaguzi zetu utaongezeka kutokana na wanaotaka kuendelea kutawala kuvurunda kiasi cha kutostahiki kuchaguliwa kwa haki.

Huwa nina swali moja ambalo limegeuka wimbo wangu wa jogoo. Je, watanzania washikwe wapi ndipo washtuke? Kashfa zote zilizoharibu maana ya maisha kwao zimetendwa na wahusika wanaendelea kupeta huku Watanzania hawa hawa waathirika wakiendelea kutulizwa kwa nyimbo na mashairi matamu yakisindikizwa na vinanda vya watabiri uchwara na viongozi wa upinzani waliochoka hadi kukipigia debe chama wanachosema wanakipinga.

Je, tatizo letu kama taifa ni nini? Je, upuuzi huu wa kupachika mambo yao kwenye sheria ni mchezo waliouzoea kutokana na wabunge wetu wengi kutokuwa makini na kufuata per diem?

Watahangaishwa na nini iwapo wanaweza kughushi vyeti wakaendelea kuula?

Je, rais amesaini nyaraka ngapi chafu zilizochomekwa kama sheria hii? Huu ni ushahidi tosha kuwa tunatawaliwa na sheria zilizochomekwa.

Ajabu kuonyesha tulivyo na taifa lisilofikiri wala kuthubutu, hata baada ya kashfa hii kufumka, vyombo vya habari havikukerwa kiasi cha tahariri zake kumtaka rais na serikali yake wawajibike mara moja! Maana wamegusa patakatifu pa patakatifu.

Mwalimu Julius Nyerere alituachia urithi wa maana wa kuandika vitabu na kuvisoma. Ajabu watawala wa kizazi hiki wana rekodi ya kuzurura na kuizunguka dunia bila hata kuandika kitabu kimoja.

Katika kitabu changu cha Saa Ya Ukombozi niliongelea tabia hii chafu ya rais wa nchi ya kufikirika kuletewa makaratasi ayasaini bila kuyasoma kiasi cha walioko chini yake kutumia mwanya huu kutaka kuuza kijiji bila ya yeye kujua kutokana na kuwa bize akifanya ziara ughaibuni.

Upole wa Kikwete sasa umevuka viwango vya kuvumiliana. Tusimuogope. Maana taasisi ya urais ni yetu si yake.

Tumwambie apishe wenye uwezo waongoze badala ya kuendelea na kuwa na watu wasio makini ambao wamegeuzwa muhuri bila kujijua kubariki hujuma kwa taifa.

Pamoja na majibu ya serikali kuhusu suala hili, jambo hili inabidi lirudi tena bungeni ili lijadiliwe na kupatiwa majibu ya uhakika.

Vinginevyo tunachelea kwamba siku moja, waliompotosha rais, watasababisha asaini waraka wa kuwauza Watanzania wote naye akiwamo, asijue.
Chanzo: Tanzania Daima.

No comments: