The Chant of Savant

Tuesday 19 January 2010

Maalim Seif, usimkwaze Karume

HAKUNA ubishi. Katibu Mkuu na mtu mwenye ushawishi mkubwa katika Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharrif Hamad, anazidi kujichanganya na kutaka kuuchanganya umma.

Alikaririwa hivi karibuni akitaka Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar, Amani Abeid Karume, aongezewe muda wa kukaa madarakani siku tatu baada ya yeye kusema hana mpango wa kukiuka katiba kuongeza muda mwingine juu ya ule uliotajwa na katiba.

Alikaririwa akisema: “Baada ya kutafakari, mimi binafsi naungana na wale wanaotoa wito wa kuchukuliwa hatua ya kusogezwa mbele kidogo uchaguzi mkuu wa Zanzibar mwaka huu.

Aongezewe kipindi cha kati ya mwaka mmoja au miaka miwili, ili kutoa nafasi kwa Rais Karume kukamilisha kazi njema aliyoianza.”

Huyu bwana anatuchanganya licha ya kujichanganya. Hajui kuwa Karume hakuwa akifanya kazi yake bali ya wananchi. Kwanza aambiwe wazi. Hakuna kazi ya Karume. Pili, aelewe Karume hakusomea hiyo ‘kazi’, hivyo kazi hiyo inaweza kumaliziwa na mtu yeyote. Nani kamwambia Zanzibar itapata rais mwenye kufanya kazi mbaya na si njema?

Je, huku ni kuishiwa kisiasa na kimkakati kiasi cha mtu aliyegombea urais mara nyingi tu na kushindwa kuamua kujipiga mtama?

Demokrasia gani isiyoheshimu katiba? Kama seif, kama Augustine Mrema ameishiwa udhu wa kugombea baada ya kushindwa mara nyingi na kuamua kuacha basi awaachie wengine wenye udhu waongoze.

Hivi Seif bado hujui kuwa kuvunja katiba kwa namna yoyote ni kosa la uhaini? Je, haya ndiyo matunda ya makubaliano ya faragha ambayo yanaanza kuonyesha masilahi binafsi kuliko umma?

Kumbe wanachama wa CUF waliotaka kumtia adabu baada ya kutangaza walichoona kama usaliti hawakukosea? Je, hii ndiyo sababu ya kufanya makubaliano kwa niaba ya chama kuwa siri na mali ya Maalim Seif na Karume? Je, Serikali ya Muungano itajipinga na kukubali usaliti huu wa mchana?

Je, Seif hajui kuwa Karume anajua katiba ya chama na nchi yake kiasi cha kusema wazi hataki kuongezewa muda?

Hakika hii ni usanii (political gimmicks). Maalim anahitaji msaada hata kama kaahidiwa vinono haviwezi kuja kwa kuvunja katiba. Je, hapa nani anataka kumtumia nani kati ya Karume na Seif?

Kwanini Seif hakujiuliza swali moja kuu na muhimu kama kweli anatetea masilahi ya umma na si yake binafsi. Kwanini Karume ametambua haki ya mshikamano wa Wazanzibari baada ya kumaliza muda wake kama ni kweli?

Kwanini muafaka unaoihusu jamii-hasa vyama vikubwa viwili hasimu vya siasa na pande mbili za nchi na si watu wawili- ufanyike kwa usiri mkubwa kama hakuna namna kama Seif anavyoanza kubainisha huku akiwa ameachwa peke yake baada ya mwenzie kutamka wazi hataki hicho Maalim anachoona kama ni nusra ya Zanzibar.

Je, Serikali ya Muungano itakubali kudhalilishwa wazi wazi kwa kuonyeshwa kama haina mamlaka na sehemu moja ya nchi ukiachia mbali kushindwa kutatua matatizo ya Zanzibar ?

Inabidi Maalim akumbushwe kuwa Karume hawezi kuukata mkono ambao umemlisha kwa miaka kumi, yaani Serikali ya Muungano. Hata akiwa mwizi wa fadhila akafanya hivyo, anajua madhara yake kutokana na nguvu na namna ya kufanya mambo ya serikali hii.

Kwanini Maalim anataka kutumia makubaliano ya mdomo tena ya watu binafsi kuvuruga katiba mbili, yaani ya Muungano na ya Zanzibar?

Je, ameshauriana na wanasheria wake au amekurupuka asijue hili haliwezekani? Je, huu ni mwanzo wa mwisho wa Maalim baada ya kuonyesha wazi kuwa hawezi kukivusha chama? Swali moja litamuandama Maalim hata Karume. Kwanini muafaka baina ya Karume na Hamad na si CCM na CUF kama kweli una nguvu kisheria? Maelezo?

Mbali na ufafanuzi wa hivi karibuni -ulioonyesha kuwa pigo kwa CUF- wa Makamu wa Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, hakuna kauli rasmi kutoka CCM.

Rais Kikwete hajazungumzia hili kwa kinaganaga na kwa namna inayostahili kama mkuu wa chama na serikali. Je, hakushirikishwa? Kama hakushirikishwa ni kwanini?

Kama alishiriki anagwaya nini wakati katiba aliyoapa kuilinda inataka kuvunjwa? Kama anashiriki na hataki kuhusishwa, je, anajua mambo yatakavyoharibika mbele ya safari au hajui-ajenda ya siri - kuvunja katiba tena wakati wa kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu?

Kwanini Maalim amegeuka ghafla hata bila kuchelea aliyowahi kusimamia na kusema huku nyuma ukiachia mbali kuwaacha wanachama na wafuasi wake hoi? Kuna nini nyuma ya pazia?

Je, ule uvumi kuwa Maalim anadhani anaweza kuchukua dola hivyo kuhitajika na Karume kumlinda unaanza kuwa ukweli? Je, Karume alisema hataki kipindi kingine kama geresha bwege akijua kuwa msukumo wa CUF utaifanya CCM isalimu amri?

Hivi Maalim anadhani hatujui kuwa siku zote amedai ushindi wake uliibiwa na Karume huyo huyo na CCM? Hili swali ndilo linalowasumbua CUF. Ushindi wao umerejeshwa lini?

Je, unataka kurejeshwa kwa makubaliano ya siri ambayo kisheria hayawezi kuleta maana wala kutekelezwa? Kwanini Maalim amekuwa akimlaumu Karume baba kuwa alifanya makubaliano ya Muungano kwa mdomo na sasa anarudia yeye?

Kwanini muafaka nje ya CCM kama hakuna namna? Jiulize tena. Kwanini kwa usiri mkubwa na bila kutarajia hivi? Wengi wanajiuliza. Na kwanini saa chache kabla ya uchaguzi na kwa faida ya nani kama siyo Uzanzibari kutangulizwa mbele ya Utanzania? Je, watafanikiwa?

Kitu kingine kama si ubinafsi ambacho Maalim alipaswa kujiuliza ni haki za wale walioathirika kwenye sakata hili.

Kwanini baada ya miaka tisa ya Karume kuwa madarakani? Je, hapa haki za wale waliopoteza maisha, mali na kugeuzwa vilema kwanini hazikuzingatiwa kama hakuna namna?

Wapo wanaoota wakisema serikali ya mseto yaja. Kwa katiba gani na sera ipi? Ukweli ni kwamba hakuna kitu kama hiki. Hizi ni ndoto za mchana na bahati nzuri CCM wameishalitolea jibu hili.

Rejea ufafanuzi wa Makamu wa Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, hivi karibuni: “Watu wanatakiwa kuelewa kuwa hakuna muafaka wowote wa kudumu ulioafikiwa baina ya vyama hivyo, bali kilichotokea ni CUF kumtambua Rais Karume tu na hakuna makubaliano mengine. Kutokana na uamuzi huo, CUF inaweza ikapata nafasi mbili za uwakilishi katika Baraza la Wawakilishi.”

Maalim, usimkwaze Karume. Kaishasema wazi hataki kuongeza muda. Hata CCM haina mpango huo. Kama makubaliano yanalazimisha hivyo, jaribu njia nyingine ambayo haikudhalilishi wala kuvunja katiba. Kwanini ulazimike kulamba matapishi yako?
Chanzo: Tanzania Daima Januari 20, 2010.

No comments: