The Chant of Savant

Tuesday 12 January 2010

Je kuna mpango wa kukolimba wapinzani wa Kikwete?





Katika nchi zinazotawaliwa na serikali dhalimu na chafu, watawala hukaa madarakani kwa muda mrefu wakitumia mbinu chafu mbali mbali. Vitisho, wizi wa kura, hongo, wizi na hata ulaghai hutumiwa sana katika kufikia malengo yao ya kukaa madarakani kinyume cha utashi wa watawaliwa.

Katika kufanikisha hili, vikundi vya kijamii kama vile vijana, wanawake, matajiri, matapeli, waandishi wa habari hata wana taaluma hutumika. Kadhalika vikundi vya kidini hutumika. Hii ikichangiwa na ujinga, uroho, umaskini na tamaa za wahusika, watawala-wenye pesa na madaraka-huvutia kila wachumia tumbo.

Hivi karibuni vikundi uchwara vya kidini vimejiingiza kwenye siasa chafu vikiwaunga mkono watawala ili vipate lau makombo ya ufisadi. Rejea maandamano yaliyokuwa yameandaliwa na viongozi wa kidini wa mitaani kutaka kupinga wale wanaomkosoa rais. Kutokana na ujinga na umaskini kiakili wahusika hawakujua kuwa kumpinga au kumkosoa rais ni haki ya kidemokrasia!

Hivi karibuni mtu aliyejipachika utabiri katika Afrika mashariki na kati, shehe Yahya Hussein alikuja na mpya. Alitabiri kuwa atakayesimama kumpinga rais Jakaya Kikwete kwenye uchaguzi ujao atakufa ghafla! Hii inatisha na ni jinai. Amejuaje iwapo kisayansi hata kiimani binadamu hakujaliwa kujua ya kesho? Je huyu jamaa anatumiwa kutisha au kupeleka ujumbe kuwa atakayejitokeza ndani ya CCM kama ambavyo hali inaonyesha atashughulikiwa kama alivyofanyiwa katibu wa zamani wa CCM Horace Kolimba? Je hili likitokea jeshi la polisi litaacha kumshughulikia mhusika kwa vile anamtetea rais? Je ametumwa na rais kuwatisha wale anaoona wanaanza kutaka asipewe nafasi ya kugombea awamu nyingine? Je huu si uhuni?

Kutojua sheria wakati mwingine huleta ushujaa wa kipumbavu. Inakuwaje mtu mzima kiumri atabirie watu vifo asijue ikitokea anawajibika yeye kisheria?

Kinachoonyesha kuna namna, ni ile hali ya shehe Yahya kumfagilia Kikwete kiasi cha kudai atashinda kwa kishindo wakati hata kampeni za uchaguzi hazijaanza kisheria. Je kwanini shehe Yahya amesema hivi tena kwa kujiamini kama hakuna njama hii chafu? Je hii si taarifa kuwa tutake tusitake tumchague tusimchague lazima Kikwete, kwa mbinu ajuazo, ashinde hata kama hana sifa?

“Natabiri kuwa Kikwete ndiye Rais mpya wa mwaka 2010 na atakayempinga katika chama chake atakufa ghafla. Natabiri ushindi wa Rais Kikwete mwakani utaleta serikali ya mseto Tanzania Bara na Tanzania Visiwani," alisema Shehe Yahya.

Bahati mbaya sana, taifa letu limegeuka la washirikina na mataahira wanaoweza kulishwa kila uchafu. Ni juzi juzi tumeona kwenye vyombo vya habari mchungaji wa kujipachika Getrude Rwakatare akionyesha “mchawi’ aliyekuwa na mfupa wa binadamu bila wahusika kuchukuliwa hatua! Inakuwaje karne ya 21 tunaruhusu upuuzi kama huu? Kwanini hatujifunzi kutokana na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yaliyoasisiwa na kuchochewa na waganga njaa na wachungaji uchwara kama hawa? Ingekuwa si hivyo wachumia tumbo hawa wangeona aibu na kuogopa kusema upuuzi wao. Kwa wanaokumbuka kilichompata shehe Yahya alipokuwa mkuu wa kitendo cha masuala ya kidini Bakwata chini ya marehemu shehe mkuu Hemed Jumaa, atakumbuka alivyotimuliwa bila hata yeye kutabiri hili lingemtokea. Tulimuona akilialia kwenye vyombo vya habari akiwafokea waliomuuliza ni kwanini hakuweza kutabiri hili.

Inakuwa hatari sana pale watawala wanapotegemea na kuamini watu kama hawa ambao kimsingi hawana utaalamu wowote bali utapeli na uganga njaa. Hebu jionee mwenyewe uganga njaa na utapeli ulipo kupita nukuu hii ya shehe Yahya: "Kwa hiyo Kikwete alirithi urais huu kutoka kwa Nyerere. Ngoja awamu ijayo, mwachie Mkapa, kauli hiyo bado haijafutwa kwani mirathi kutoka kwa mwalimu ni ya awamu mbili.’

Hivi ni mtanzania gani hajui kuwa Nyerere alimkataa Kikwete kutokana na kukodisha ndege kwenda kuchukua fomu Dodoma bila kueleza yeye na mwenzake Edward Lowassa walipokuwa wamepata hiyo pesa? Nani hafahamu kuwa Nyerere alimwambia Kikwete kuwa hana ukomavu kisiasa na aliokuwa ameshikamana nao wameoza ukiachia mbali kutokuwa na sera wala udhu wa kuwa rais? Shehe Yahya asitufanye wote wapumbavu tusio na kumbukumbu wala kujua historia ya jana.

Huyu mshirikina inapaswa aambiwe na kuonywa kuacha kuutukanisha uislam (kwa kuutumia kupiga ramli) ukiachia mbali kutaka kumtumia marehemu baba wa taifa kuhalalisha utapeli wake. Asimtumie kwa vile hawezi kujibu ameisha kufa. Hii ni kashfa kwa Nyerere kusema aliridhia ufisadi. Nyerere hakuwa kipofu, juha hata mjinga kiasi cha anachotaka kuonyesha huyu anayeitwa shehe.

Kuonyesha ni kwa jinsi gani anavyotapa tapa anataka kupindisha ukweli kuwa aliyerithi madaraka toka kwa Nyerere ni Kikwete badala ya Ali Hassan Mwinyi!

Shehe Yahya anazidi kuonyesha ujuha wake pale anaposema: "Natabiri kuwa kutatokea maandamano makubwa ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa wabunge wa pande zote za vyama vya upinzani na CCM kuhusu wizi wa kura,"

Haiwezekani rais ashinde kwa kishindo halafu wabunge wake wasipewe kura sambamba naye ili kumrahisishia kutawala. Huu ni uganga njaa wa hali ya juu.

Angalia ukihiyo mwingine: "Zanzibar, CUF imeshinda, wewe ukiona mtu anamkaribisha mshindani wake nyumbani basi ameshindwa," alisema Shehe Yahya.

Maskini mtabiri wetu hajui kuwa kilichotokea Zanzibar hakilengi anakoelekea kutokana na CCM kuweka wazi kuwa hawana sera ya serikali za mseto! Kwanza si kweli kuwa CUF imeshinda. Ingeshinda mwenyekiti wake prof. Ibrahim Lipumba asingesema kumtambua rais wa baraza la mapinduzi, Amani Karume ni kamari ya kisiasa (political risk).

Zanzibar hakuna ushindi kwa CUF zaidi ya kutaka kutumiana na kuzidiana ujanja ambapo mmoja anadhani anaweza kumlewesha mwenzake wakaingia kwenye uchaguzi halali akashinda asijue mwenzie anampigia mahesabu ya kujenga mshikamano haramu wa kizanzibari ili aweze kugombea ngwe nyingine kinyume cha katiba! Utabiri , uganga na siasa wapi na wapi?

Kuna haja kwa wapinzani wa nje na ndani ya CCM kutafuta haki mahakamani kwa kufungua kesi ya kutaka shehe Yahya aeleze alipopata habari hizi chafu na mpango mzima ili kuzuia watu kukolimbwa na hatimaye kuja kuambiwa ilitabiriwa.

Kuna haja ya kumshauri Kikwete kuachana na kutumiwa na waganga njaa hata kama ni kwa kumpa matumaini yasiyokuwepo. Umefika wakati wa kuliondoa taifa kwenye ushirikina na ufisadi wa kiimani na kiakili.

Je kuna mpango wa kuwatisha au kuwakolimba wanaompinga Kikwete?

Lazima watanzania wajue. Kama kuna mtu atakayesimama kumpinga Kikwete na akafa tujue ameuawa kama alivyobainisha shehe Yahya. Na hili likitokea mtu wa kwanza kuwajibishwa awe shehe Yahya. Kwani inaelekea anajua mpango huu mchafu. Ndiyo maana haogopi kusema hadharani. Mkutano wake na vyombo vya habari ni ushahidi tosha wa hili mahakamani.
Chanzo: Tanzania Daima Jan. 13, 2010.

No comments: