The Chant of Savant

Friday 11 December 2009

Nabembea sipumziki hata msemeje

KUNA watu hawana maana kabisa. Wananalalamika eti mkuu wao nimekaidi ushauri wa daktari wangu ambaye siku hizi anaonekana kutojua chess inavyochezwa. Eti ananitaka nipumzike kurukaruka ughaibuni!

Hajui ziara zinavyoniingizia mipesa ukiachia mbali kutalii na bi mkubwa. Mpuuzi huyu. Nani apumzike? Nani anaweza kushiba madili na maraha? Thubutu yake! Wakubwa huwa hatuchoki ama kukinai ulaji. Unakula huku Bi mkubwa na mashoga zake kule. Vitegemezi vinavuta huku; maswahiba nao wanachomoa huku mradi mwendo mdundo.

Tuache utani. Kula bila kulipa ni raha hamna mfano. Hebu fikiria. Wanakijiwe wanachanga pesa na kukupa utumie bila kuwa na mhasibu. Wanategemea nini? Panya hataacha vya dezo hata awekewe mtego. Mimi ni kama lisirikali la jamaa yangu. Huchangisha watu pesa kwa njia mbalimbali, kodi, faini na njia nyingine halali na haramu ili litumie kwenye upuuzi kama kuruka ruka.

Japo linatumia vibaya, nani atauliza iwapo ndilo alpha na omega? Ukitumia vibaya unaitwa fisadi. Ukitumia vizuri unaitwa mzalendo kama Mchonga.

Hebu niongee kwa herufi kubwa kila mtu aelewe. Sipumziki ng’oooo. Si mimi, Bi Mkubwa, vitegemezi vyangu wala maswahiba wangu. Lazima niendelee kupeta tena na tena. Wenye wivu jinyongeni. Kosa ni nini? Walevi Wadanganyika niliwaweka sawa wakanipa kura ya kula.

Sasa nakula nyie mwachonga midomo. Jamani nieleweni. Sipumziki. Nitapumzika siku ya kufa au walevi watakavyostuka kuwa nawatia kitanzini wakanitimua. Zaidi hapo sipumziki.

Sharti mjue. Sikio halishibi kusikia wala jicho kuona. Wahenga walisema. Nami sichoki kujirusha wala kuona maajabu ya dunia kama bembea la juzi.

Wakosoaji hawajui. Ninapokuwa nje nakula maraha napumzisha akili. Hivi hamjui kijiwe kilivyo moto kutokana na kashfa za wizi wa kashata na kahawa uliofanywa na washirika zangu kina Kanji na Eddie?

Kazi ya kujitetea nimemuachia mgosi Joe Machungi wafunge makamba walevi wajue mimi ni Yusufu wao mkombozi. Hamuoni anavyopayuka kama Sufii Fyatu huku akiwaita watu wehu wakati naye ni mwehu?

Mnadhani mzee wangu huyu anapenda kuadhirika? Njaa jamani. Asipopayuka kunifurahisha namtimua kupotea kwenye rada ya kijiwe. Najua na anajua simpendi wala hanipendi. Hapendwi mtu bali ulaji hata kama ni kwa kujidhalilisha ilmradi mkono uende kinywani.

Binadamu tumeumbwa tofauti. Wapo wanaoweza kuuza utu na watu wao ilmradi mkono uende kinywani. pia wapo walio tayari kufa njaa kuliko kujigeuza watumwa wa matumbo yao. Hawa ni wachache kama almasi duniani.

Wapo walio tayari hata kujigeuza vyangudoa ilmradi tonge lishuke. Hawa ni wengi hasa kwenye siasa za kisasa za kijiwe. Ila mimi simo.

Usicheze na ulaji tena wa bure hasa usawa huu wa kuvurugika kwa uchumi wa dunia. Muulize yule jamaa wa madevu au yule mchungaji Mtikisa waloijifanya vijogoo wakati ni watoto wazuri tu. Tumewafanya nini na wako wapi? Tumewalambisha kashata wamenywea na kuwa watoto wazuri. Jamani nifanye nini ili muelewe? Na lazima mwakani mtanipa tu mtake msitake.

Kwanza mjue mie nilichaguliwa na Mungu kuja kukiokoa na kukitumia kijiwe. Hivyo msiponichagua laana ya Mungu itawandama hadi mtubie kwa kunipigia magoti mkiwa uchi kama wanga. Nami sitawasamehe. Utamsameheje mtu anayeingilia ulaji wako na maraha yako na short wako?

Kuna wapuuzi wanasema eti nisipewe ulaji tena kwa sababu sikufanya kitu! Hebo! Hamkuniona nabembea ukiachia mbali kuumua deni la kijiwe? Eti wanasema hawatanichagua.

Mimi kwa taarifa yenu sitegemei vijikura uchwara vyenu. Nina fuko la noti. Hamjui sabuni ni pesa ya roho, sorry, pesa ni sabuni ya roho?

Ingawa nashutumiwa kutumiwa na mafisadi, mjue. Natumiwa kweli na mafisadi. Nami nawatumia ninyi. Kwa hiyo hapa ni kutumiana mtindo mmoja.

Kwa vile wanakijiwe wengi ni maskini na wajinga, nikiwahonga kashata, tangawizi, kahawa hata sigara kali kama wanasiasa wanavyohonga wadanganyika wao, kuku, nyama choma, lift kwenye mashangingi yao, T-shirts, Khanga na upuuzi mwingine na wanaachia kura na wanasiasa wanakula kwa ulaini.

Nami kadhalika na kashata na kahawa vyangu. Jamani mmeambiwa raha jipe mwenyewe usisubiri kupewa utakesha bure. Upo hapo?

Kama hujaelewa jiulize yale madude kama EPA, Meremeta, ANBENO, Tanpower, Richmond, Kagoda, Deep Green Finance na mengine yalianzishwa na kina nani?

Hii ndiyo njia ya kujilipa baada ya kuwahonga waroho na wadanganyika. Juzi nilisikia mjumbe mmoja wa kijiwe akisema eti mimi ni mtumwa wa mafisadi asijue naye ni mtumwa.

Asingekuwa mtumwa si angewachochea walevi wanitimue? Kwanza nani kamwambia ang’ang’anie kijiwe chetu kama yeye si mtumwa wa mafisadi wangu? Kitoe kama kweli wewe kidume.

Nasema tena kwa kinywa kipana. Yeyote anayejisikia anapunjwa au kubanwa akitoe. Sina shida na mtu. Sibembelezi mtu ati. Nitabembelezaje wakati ninao washitiri wangu na ni bingwa wa sanaa za kuwaweka sawa walevi wangu? Nawajua walevi wangu nao wananijua. Kama kondoo hunifuata hata machinjioni ingawa wanajua mwisho wao ni pale kweye majili.

Pia ieleweke. Siibi peke yangu. Hivyo kifo changu ni cha wengi walionizunguka na wasingependa walevi wanitimue. Maana kufanya hivyo kutakuwa mwisho wa matanuzi yao. Hata wakinitimua, watakayemchagua atakuwa wangu hivyo atanilinda taka usitake.

Mara hii jamani mmesahau sera yetu tukufu ya kulindana na kufadhiliana! Kweli walevi ni walevi hata ukiwapa juisi bado watalewa. Watashindwaje kulewa iwapo wanalewa hata maneno na kukalia matumaini kama paka akaliavyo mkia wake akadhani amekalia kochi ?

Hebu nitazame ujitazame. Wakati wewe unayekodoa mimacho na kukabwa na mafunda ya hasira ukikonda, mie na bi mkubwa tunanenepeana kama paka wa dukani kwa pesa ya kijiwe chako. Siku hizi mambo kubembea ati.

Ni majambazi na vibaka wangapi wanaitwa waheshimiwa kwa sababu ya kupata? Ni wazinzi na wauaji wangapi wanajazana kwenye nyumba za ibada? Unadhani wote waliofungwa walitenda makosa au walio huru hawavunji sheria? Shauri yako karagabaho.

Tuache masihara. Picha ya kubembea imeniletea noma sana. Sababu? Kuchagua wapiga picha vihiyo kama huyu Misupu.

Du! Mbavu zinauma. Lakini sipumziki. Ngoja niseme taratibu walevi wasiipate wakasema nipumzike.

Wabillahi tawfiq.

Chanzo: Tanzania Daima Dec. 9, 2009.

No comments: