The Chant of Savant

Friday 6 November 2009

Mie sikughushi, nichagueni mwakani jamani

NAITWA Mpayukaji Msemahovyo PhD (Economics) PhD (Abracadabra and Hoaxes) Masters (Lies and faking) Masters (Corruption and Bribing) Advanced Dip (EPA and Richmond), BA (Performance and Ngonjera) etc.

Kumbuka, tuna uchaguzi karibuni kwenye kaya ya Waliwa Wadanganyika. Hivyo, naanza kupiga kampeni hata kama tume haijatangaza hivyo.

Ukizingatia huu ni msimu wa kuvuna ambacho hukupanda kupitia kura ya kula, nimejiandaa kuwatumikia wanakaya. Hata kama sistahiki heshima, bado nimekamia kuitwa Mheshimiwa Mchumiatumbo. Siwezi kuacha ulaji huu wa bure upite iwapo matapeli wengine wanaweza kuufaidi kwa kutoa kila ahadi za uongo.

Nimeishaweka mikakati. Kwanza, nimeishajipatia shahada saba toka vyuo vifuatayo: Commonwealth Nonexistent University, Havazard, and Edenbug, Quacks’ Open University of the World (QOUW), New York na Make-believe University, Bangalore, India.

Kadhalika nimeishaongea na jamaa zangu (mnaowaita mafisadi) wa Kimanga na Kigabacholi kuchangia kampeni zangu ili nikishaupata uheshimiwa nihakikishe wanawekeza nchini.

Kwa vile nitakuwa mtunga sheria, tutatunga sheria za kuwapendelea kuwekeza na kujimegea neema mnazoita kutorosha mitaji.

Nitaanza na kuchangia miradi ya kinamama na vijana na baadhi ya shule kwenye jimbo langu. Yule rafiki yangu Sheikh Brigedia Ally atamwaga pesa kama hana akili nzuri kuwahonga wanakamati ya uteuzi wa wagombea chamani. Kwa dola 5,000 kila kichwa najua hakuna atakayeruka.

Sikutajwa kwenye EPA, Richmond, Meremeta, Kagoda na ujambazi mwingine. Hata kama nilipata mgawo wangu, inakuhusu nini? We usomaye waraka huu usimwambie mtu. Soma kimya kimya. Kwa taarifa yako, EPA yangu itatumika kuwalainisha walevi na wake zao kwa khanga, T-shirts, nyama choma na upuuzi mwingine. Ila kumbuka. Mimi si papa wala nyangumi. Ni safi kama Enderea Changa, Ewassa Eddie nk.

Kadhalika, nimeishapata makanjanja wenye njaa kama fisi kulipamba jina langu kwenye magazeti yao. Kaulimbiu yangu ni: ‘Mchague mkombozi chaguo la Mungu awavushe kwenda Kanani nchi ya mvinyo na nyama choma’.

Mimi si kihiyo. Pamoja na kutumia karne nyingi bila kuingia kwenye hekalu la Mungu, nimeishajiunga na baadhi ya makanisa na misikiti tayari kunipigia upatu. Kitaalamu naitwa Swindler Conman, PhD Phil, MA (Abracadabra and Hypothetical Thinking), BSc (Lies), Dip (Corruption and Mafia), Masters (Public funds Terrorizing), MBA, Masters (Money-making and Forgeries), etc. Watani wananikejeli eti ni mbunge wa tumbo. Mimi ni mzalendo wa kupigiwa mfano.

Shahada zangu zinahitaji mtu mwenye kichwa kinachochemka ambaye Waingereza humuita genius, hasa zile za MA in Lies and Hypocritical Thinking. Ni wachache waliweza kuzipata kama vile Tunituni, Dany kurap Hoi na wengine kama Bob Mugambe, Jack Zumari, Joweri Msaba na Yahya Jammeh.

Unajua? Mipango yangu ni mikubwa kuliko mlima. Hebu fikiria; nawatwanga Wadanganyika kwa kaulimbinu ya pili isemayo ‘nguvu mpya, mipango mipya uzalendo na mwanzo mpya’. Hakika walevi wataniamini kwa maangamizi yao baadaye.

Kwa kuanzia, nitakunywa nao bila kuwabagua ingawa ni wachafu. Nikisalimiana nao nitawataja majina wajue nawajua na kuwamaindi ingawa zote kamba tupu. Sitasahau kuwakumbatia huku nikikenua kama vile nawapenda. Pia nitahakikisha shangingi langu la VX linageuka daladala ya walevi. Nitawapeleka popote watakapo huku mke wangu akitumia NGO yake kugawa rushwa kwa njia ya misaada kwa akina mama na shule za misingi na sekondari kaya nzima.

Atawafunga kamba akina mama kuwa nikishinda atahakikisha akina baba wanapiga deki na kuosha watoto bila kusahau kuwavisha magagulo huku akina mama wakirejea usiku wa manane wakitoka kufaidi uhuru mpya.

Pia nitaanzisha mfuko wa kusaidia jamii uitwao “Swindler’s Anthropological Society of Thoughts” (SAST) ili kupigania haki za viumbe wote kuanzia mapapa, nyangumi, fisi, mafisadi, vikongwe na albino. Nitaitisha mikutano ya harambee kuchangia wagonjwa na mashule jimboni mwangu. Hapa nitanunua vyandurua 500 kwa ajili ya zahanati jimboni na madawati 200 kwa ajili ya shule za misingi. Pia nitanunua mipira na jezi kidogo huku nikivaa moja na kucheza kabumbu na vijana wa vijiweni wajue mimi ni mwenzao. Ingawa huwa nawaogopa kama ukimwi, mara hii nitakula boli nao huku msaa wangu wa Rolex wa bei mbaya nikiuacha hom maana wanaweza kuunywa wezi hawa wa kutengenezwa nasi.

Kumbuka, nimeishawaweka sawa wazee wa kabila letu kwa kumpa chochote kitu kiongozi wao. Usishangae kuniona nimevalia mavazi ya kiasili nikitawazwa kuwa kamanda wa vijana wa wilaya wa chama changu.

‘Nyumba yangu ndogo’ niliyozaa nayo toto la kiume na kulikana, nitairejea kwa haraka sana ili asitoboe siri zangu. Mwanaharamu wangu huyu atageuka ghafla kuwa mtoto wangu kipenzi na nitamuahidi mama yake kuwa nitampeleka sekondari nchini Uingereza. Kumuweka sawa kwanza, nitatafuta shule moja ya kimataifa ya uongo na ukweli nikifanya maandalizi ya kumrusha majuu. Nitamfunga kamba kuwa namuandaa awe rais wa nchi baadaye.

Wafa na nguna wajinga nitawaahidi kupigania bei za mazao yao. Hapa lazima nikope ujanja toka kwa Mheshimiwa Mizengwe. Nitaahidi trekta kila kijiji bila kusahau maji safi na umeme usiokuwa wa mgawo. Hapa Mwarabu wangu wa Dubai atanipiga tafu. Kuwaua kabisa, nitaalika wanafunzi wa chuo cha maji kuja kufanya tathmini ya mradi wa maji na umeme kwa vijiji vya jimbo langu.

Mbinu nyingine ni kumtetea mwenyekiti wa taifa wa chama changu cha UNM, yaani Ugali Nyama na Maharagwe kwa kila upuuzi atakaofanya. Nimeishatishia na kuapa kwa miungu yote kumnyotoa roho yeyote atakayempinga. Huwa naapa kwa kupandisha mwenembago kama morani wa Kimasai niapapo kwa miungu yote ya uongo na ukweli.

Wengi watadhani naota. Lazima niingie bungeni. Kwanza mie ni handisamu kama Njaa Kaya. Isitoshe ni kijana kinda wa miaka 59 ambaye hutabasamu hata kwenye msiba. Pili, mimi ni chaguo la Godi. Tatu ni mtaalamu wa sanaa hasa lugha tamu yenye kupumbaza na ahadi kem kem. Nne ni mtu wa watu. (Usiulize kama kuna mtu wa fisi). Tano nimeleta amani kwenye kijiwe na mifuko ya wapiga kura.

Nina sifa zaidi ya elfu na moja. Hivyo leo nakumegea. Inshallah nategemea kuelezea sera zangu huko tuendako, hasa jinsi ya kupambana na wizi wa kura na migawo ya umeme hewa na maji. Nitahakikisha natetea haki za wanyonge, hasa kwenye wizi huu uitwao multiparty hoax - samahani siasa za vyama vingi. Pia zingatia. Mbinu zangu ni mpya na hazijawahi kubuniwa wala kutumiwa na mtu yeyote isipokuwa mimi tu. Niachie hapa niende kuandaa nyavu za kuwanasa wajinga. Kaa chonjo saa mbaya! Wajinga ndio waliwao.

Khalas Kweisine

Chanzo: Tanzania Daima Nov. 11, 2009.

No comments: