The Chant of Savant

Tuesday 25 August 2009

CCM yetu na vioja vya ufisadi


NIMEFARIJIKA kusoma habari kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeunda mkakati wa kuwanyamazisha makada wake wapinga maovu! Hongera CCM. Kwani wanaopinga ufisadi wanapinga sera ya chama na wanatishia amani ya matumbo yetu wakubwa. Hawana mapenzi mema na taifa letu.

Vikao vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC), vilivyomalizika hivi karibuni, kwa kujipiga kifua na “kusoma alama za nyakati”, vimetoa karipio na onyo kwa wanaochukia ufisadi. Hapa wananchi, ambao ndiyo wanufaika wa maendeleo haya, wanapaswa waandamane kuunga mkono msimamo huu.

Wapo walioota ndoto za mchana wakatumia Bunge wasijue nalo ni mali yetu.

Hebu kwanza soma nukuu hii toka kwa mtu ambaye namheshimu sana na kumuona kama mzalendo, John Chiligati, “Kwa hiyo tumesema inatosha, hapo tulipofikia tusiendelee mbele. Wanaoropoka hovyo ni walevi na tumeona kuna kundi dogo ambalo limejiona kama ni wateule wa kuzungumzia sakata hilo (la ufisadi) bila ya kujua wabunge wote wana haki ya kuzungumzia suala hilo, lakini kwa utaratibu tena kwa kupitia katika vikao vya kamati za wabunge.”

Lazima vizabizabina wapashwe. CCM ina wenyewe na wenyewe ni wale mnaowaita mafisadi. Mafisadi ni nani kati ya nyinyi msiokubali kuunga mkono sera za mafanikio za Rais Jakaya Kikwete ambaye ameishatekeleza ahadi zake zote? Japo ni lugha ya kitapeli, siku hizi hata dua kufika lazima uwe tajiri kama alivyosema jambazi mmoja ajifichaye kwenye majoho.

Soma nukuu hii kuhusu CCM kumuenzi rais mstaafu Benjamin Mkapa kama shukrani kwa kuridhia mradi wa kupigiwa mfano ulioingiza serikali ya sasa madarakani chini ya uzalendo wa EPA.

Chiligati, tena bila wasiwasi anawapa, “Mkapa anastahili pongezi si kejeli! Anastahili heshima si dharau! Na anastahili kuenziwa si matusi!”

Hebu nimuulize, kwa nini tusimpongeze Mkapa kwa kujitwalia machimbo yenu ya makaa ya mawe ya Kiwira na kuidhinisha pesa yetu itunufaishe Benki Kuu? Kweli tunastahiki kumheshimu Mkapa. Alitufundisha kuufaidi urais na familia zetu na nyumba zetu ndogo.

Wanaosema alifanya biashara haramu Ikulu; wajinga hawa. Hawakujua: rais huwa hakosei na nchi yote ni mali yake? Tumuenzi Mkapa kwa kuwasahau akina Nyerere waliotuwekea mtima nyongo hadi tukachelewa kuula. Acheni roho mbaya, bila ufisadi nchi haiwezi kwenda popote. Muelewe. Tunaposema nchi tunamaanisha sisi. Nchi ni sisi na sisi ni nchi.

Lazima kaka Chiligati atetee hata kama mtasema ni upuuzi. Soma hii upasuke, “Hayo yote ni mambo mazuri, lakini bado Watanzania wanaona kuwa alichokifanya Mkapa kilikuwa ni kazi bure, jamani sisi ni watu gani tusiokuwa na shukrani, yaani kila jambo kwetu ni baya, tukumbuke kuwa nchi hii ilikuwa katika hali ya kuwa mufilisi; ilikuwa haikopesheki, lakini sasa tunakopesheka.”

Je, kauli hii haimuenzi mzee Ali Hassan Mwinyi ambaye alitoa taarifa ya utendaji wa serikali yake wakati akiondoka madarakani? Mzee Mwinyi kafurahia sifa hizi kiasi cha kushiriki kwenye kigwena chetu.

Nakumbuka. Alieleza alivyokuta nchi bila vitu madukani wala akiba na akaacha ziada. Hakuna aliyewahi kukanusha. Kuthibitisha hili Mkapa aliondoka hata bila kuaga achia mbali kutoa taarifa kama alivyofanya mtangulizi wake. Kwa maana kila kitu kilikuwa bomba. Mkapa alikuta “muflisi” akaacha ujasiriamali.

Aliuminya mzunguko wa shilingi huku uchumi ukinawiri baada ya kukabidhiwa mikononi mwa wawekezaji “waaminifu” kiasi cha Jakaya Kikwete kutoa ahadi ya kurekebisha mikataba aliyoingia Mkapa ili iwe bora zaidi. Hamkuona alivyotekeleza hili haraka na kwa ufanisi? Asiyeona hili basi hana macho.

Tuache matusi. Kila Mtanzania anapaswa kumuenzi Mkapa kuanzia mkewe na watoto wake waliochuma utajiri haraka haraka kwa njia halali, Kikwete aliyeweza kuingia madarakani kwa madai ya kutumia pesa ya EPA, Chiligati na wengine wengi walionufaika na neema za Mkapa. Watanzania hawana sababu hata moja ya kutomuenzi mtu aliyewafundisha jinsi ya kutumia mali zao huku wakiendelea kuwa matajiri kama alivyowazidishia utajiri Kikwete.

Wengine wanaopaswa kumuenzi Mkapa ni wawekezaji wa kupigiwa mfano kama Net Solution Group, IPTL, Kagoda, wezi madini yetu, Fosnik, DevConsult, Tanpower na waheshimiwa wengine.

Tukirejea CCM kutaka kuwanyamazisha wanaopinga ufisadi, huu ni mwito na onyo kwao kuwa hawana chao ndani ya CCM. Hivyo, watafute mahali pengeni wanakofaa ambako wanajiona kuchukia na kupambana na ufisadi, wakati si mbaya.

Karipio hili la jumla linawalenga Samuel Sitta, John Malecela na mkewe Anna, Dk. Harrison Mwakyembe, Lucas Selelii, Aloyce Kimaro, Christopher ole Sendeka, William Shelukindo na wengine walioonyesha wazi kuchukia ufisadi. Je, watafyata mkia au kuchukua hatua kuiadhibu CCM kabla haijawapatiliza? Watajijeijei.

Kwa wanaojua historia ya CCM, tukubaliane; hata mwanzilishi wake Mwl. Nyerere alitabiri kuwa atakayeisumbua, sorry, atakeyeijenga CCM atatoka CCM. Je, wakati wa utabiri huu kutimia umetimia ambapo vigogo wanaojulikana kwa kuchukia ufisadi watajitoa au kuendesha upinzani mkali ili kuipa changamoto ya kuimarika zaidi?

Je, haya ni madhara ya lile ombwe la mawazo na visheni lililosemwa au kutamalaki kwa mafisadi kwenye nyadhifa za juu chamani? Sisi hatuchukii wala kuogopa upinzani ili mradi usitake kutia kitumbua chetu mchanga. Hivi unategemea nini unapokuwa na vihiyo, sorry wasomi kama Tambwe Hiza, kama wasemaji wa chama?

Hakika CCM ni chama cha matajiri tena mnaowasingizia kuwa mafisadi kama alivyowahi kuonya Mwalimu. Wanakisaidia chama kupeta. Hivyo, si wabaya mnavyodhani. Wanachama wetu wote ni mafisadi na matajiri kwa mujibu wa wakosoaji. Unadhani umma ungetuzimia ingekuwa vinginevyo? Hauwezi kukubali kuendelea kutumika kama nepi kusafisha uchafu wa walafi wachache wenye madaraka nje ya chama wanaowataka ama kuachana na CCM. Kwani CCM ni mama au baba yao? Tokeni msitusumbue. Tuache tule vyetu kwa amani. Msitujazie mbu.

CCM ina haki ya kidemokrasia kufanya uamuzi wowote, hili la kuhalalisha nyenzo hii ufisadi na kuwanyamazisha wanaouchukia linatufariji na lipaswa nalo kuenziwa ukiachia mbali wapiga kura kuchukua hatua ya kuipa zawadi CCM kama ilivyotokea nchi jirani kwa chama cha KANU.

Je, Watanzania wataendelea kujirahisi na kukubali kutumiwa na kuteswa na manyang’au wachache hadi lini? Waguswe wapi na vipi ili washtuke? Kuonyesha CCM inavyowaheshimu, inadiriki kutoa mipasho ilhali tangu ichaguliwe haijawahi kushindwa kutimiza ahadi hata moja ukiachia mbali kutenda mema kuliko hata ya rais aliyetangulia. Je, hawa wasioona mema haya si kuwageuza wananchi majuha na mataahira wa kutupwa?

Badala ya wachukia ufisadi, kuiandama CCM, wanapaswa waienzi kwa kutimiza ahadi yake kuona kuwa ufisadi hauwi tatizo nchini mwetu. Wanafahamu. Maanguko yao hayatatokana na kupinga ufisadi bali upofu wao wa kutoona neema na matendo mema ya serikali inayoendeshwa na watu wema wanaoitwa mafisadi wakati mafisadi ni wale wanaoupinga ufisadi.

Dawa si kuandamana na kupatilizana, bali kuachana na jinai na ubabaishaji wa kuandama ufisadi wakati ni mfumo mzuri kwetu. Mmesahau wosia wa Mkapa kuhusu uwekezaji?

Je, ukweli ni upi? CCM imeishiwa na inapaswa kupumzishwa haraka iwezekanavyo? Maana ni hatari na aibu kwa nchi. Sorry, namaanisha ni imara na inapaswa kuongoza vipofu milele. Hakika, CCM sasa ni chama cha Mafisadi rasmi.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 26, 2009.

No comments: