The Chant of Savant

Saturday 4 July 2009

Mene mene Tekel u-Pharsin



JAMANI mnaosoma unabii huu mjue ni wa serikali ya kifisadi ya ndotoni ya Mtukufu Mpayukaji Msemahovyo - chaguo la Mungu. Hivyo msije mkafanya makosa mkanichukia bure, kuwa nimewakwaza mkidhani nisemayo yanaihusu serikali yenu tukufu ya KISHIPA yaani Kikwete, Shein na Pinda.

Leo, nazungumzia tulivyopitisha bajeti ‘ngwengwe’ baada ya kuwatandika bao la kisigino wabunge wa Bunge letu la ndotoni. Wengi wa wanakijiwe walikuwa wamepania kuikwamisha eti kwa sababu ni ya kujipendelea na uchaguzi wa kijiwe mwakani.

Ingawa tunawajua walivyo hovyo, tulizinyaka toka kwa mashushu wetu. Hivyo hatukufanya ajizi. Tulijiandaa kuwatia adabu hasa kwa kuwatisha kuwa kama wasingeipitisha bajeti mishahara yao licha ya kuifyeka, tusingewalipa kwa vile pasingekuwa na pesa ya kufanya hivyo.

Kutokana na ufisi, ufisadi na ubinafsi wa wabunge wetu wa kijiwe, wale viherehere wote waliokuwa wamejiaibisha kwa kuapa wangeikwamisha bajeti mbona walifyata mikia na kufakamia matapishi yao kama mbwa!

Penye udhia penyeza rupia walisema wahenga. Hii ilifanya kazi kweli kweli hasa ikizingatiwa kuwa jamaa zangu wako bungeni kujineemesha kwa kuwaongopea wanuka jasho kuwa wanawawakilisha wasijue wanawakilisha matumbo yao!

Basi, bila ajizi tulimbonyeza spika wa kijiwe, mheshimiwa Six Meno Sam awatishe wabunge. Kwa kuwa letu moja, aliamua kuwasomea katiba viraka ya kijiwe isemayo Mheshimiwa Mpayukaji anaweza kuvunja bunge la ulaji iwapo wabunge wangemkosea adabu kwa kutaka kuingilia ulaji wake.

Kifungo cha 20 (7) (c) cha katiba yetu kinasema wazi kuwa wakati wowote Mpayukaji atavunja Bunge na kuwalamba bakora wabunge hata kuwafunga watakapokataa kutia muhuri makufuru yake.

Mpayukaji ana mamlaka ya kuyatumia vibaya mamlaka (power to abuse power). Yeye ni Mungu hapa duniani awatawalaye walevi na asifanywe kitu. Yeye na nyumba yake na marafiki zake wametukuka na hawakosei hata wakikosea si kosa. Hivyo, wabunge nao kwa kujua uhovyo wao, walifyata mikia na kuanza kuisifia ili wapewa ulaji wao.

Kuonyesha tulivyo wajanja, wapo waliojipendekeza hata kutumia misahafu kutulaani kwa kukwamisha mambo. Ajabu ukiwaona kina Mbwa Mwitu ambaye tunamtania kuwa ni Mzindikakaya, wanaofanya hivyo walivyo na harufu ya ufisadi unakosa maana ya misahafu!

Hata hivyo, tusiwalaumu sana. Ni wangapi wanashika misahafu kuapa kuitumia nchi kwa kuwahadaa waliwa eti wataitumikia nchi? Hamkumsikia yule jamaa aliyepinda kwa mizengwe akisema eti Tunituni Makapi ni mcha Mungu wakati ni kibaka wa kawaida?

Siku hizi viapo havina maana kama zamani. Mtu anaweza kuapa tena mbele za watu akatenda kile alichoapa kutotenda na walevi wakaendelea kumuamini. Hamjamsikia Njaa Kaya anavyowabamiza mkenge kweupe nao wakiendelea kukalia matumaini kama waathirika?

Ni wangapi wanaapa altareni au kwa shehe kuwa watakuwa kitu kimoja katika shida na raha lakini umaskini au mabalaa yanapopiga hodi wanaachana? Ni wangapi wanavunja amri ya sita wakati wameoa au kuolewa? Nenda Idodomya ujionee.

Huu ndiyo ujanja. Unatumia misahafu kuhalalisha dhambi zako kama Belshazzar wa Nabkadnezza. Ingawa maandishi ya Mene mene Tekel u-Pharsin tayari yako ukutani. Sisi hatujali. Walevi wakija kushtuka tutakuwa tunakunja jamvi na kuwaachia mkangafu wao baada ya kurarua kama tumbusi na fisi. Tutakuwa tumeishauozesha kama inzi.

Pia ifahamike. Maandishi haya yanatulenga sote. Maana siku gharika likija hakuna atakayenusirika. Tutazamishwa wote. Kwani tumeiharibu ardhi takatifu wote. Kila mmoja ukiondoa vichaa watoto na wanyama, ana mchango katika kufuru hii.

Kaya ya walevi kwa vituko hakuna mfano duniani mna habari? Kuna watu wa majoho eti walitaka tulaaniwe kwa kuingilia ulaji wao! Mbona wao wanakula sadaka ya Bwana na hakuna anayewalaani?

Eti wengine wanasema waziri wa fedha na kuchuma aachie ngazi kwa sababu waligundua alilambishwa akasamehe kodi kwa baadhi ya sekta. Hivi wanataka ale polisi siyo? Katika nchi ya walevi kujiuzulu ni dhambi isiyosameheka na kuwajibishana ni matusi ya nguoni.

Kwanza nani amuwajibishe mwenzake iwapo wote tunanuka? Nani huyu awe wa kwanza kutupa jiwe iwapo kila mtu ana ka-ulaji wake na ka-serikali kake kama Kagoda na Richmonduli katika nchi ya Ahaha?

Tatizo ni kwamba walevi wengi hawajui serikali inavyofanya kazi. Wanashikilia kuwa tuliwaahidi kwenda Kanani. Ebo! Kanani nyinyi ni Wayahudi? Hatuwezi kufanya kosa hili. Maana tukiwapeleka kule mtaichafua nchi takatifu kiasi cha kulaanika kama nyinyi.

Hivi kuna nchi takatifu kama yenu iliyozungukwa maziwa, mito , vilima huku ikiwa imejaa vito kuliko yoyote? Hapa tuambizane ukweli. Haikulaaniwa ardhi yenu bali nyinyi na nafsi zenu.

Mlilaanika pale mlipoanza kutumia matumbo na makalio kufikiri badala ya ubongo. Mlilaanika mlipoanza kujifikiria badala ya jamii. Mlilaanika na mtalaanika kwa kuwa woga na wanafiki tena kwa nafsi na maisha yenu.

Mnataka muambiwe mara ngapi? Mbona maandishi ya Mene mene yako ukutani miaka kibao. Mnayasoma na kuyaacha pale pale? Hii inakumbusha kisa cha mbuzi. Akivamia shamba kula mahindi akirushiwa jiwe anadhani msamalia mwema kamrushia mahindi zaidi!

Hadi yamkute ndipo anatia akilini. ‘Too late’. Jilaumuni badala ya kutulaumu sisi. Yamekaa ukutani hadi yanaanza kuliwa na mchwa! Ajabu kila fala anajifanya mjuaji na kila mjuaji anageuzwa fala na bado watu wanadai mambo yako sawa!

Bwana wee, ngoja nitimke kwenda kufaidi chai na mahanjumati ya bilioni 19 za brother Mstaafu Mkulu.
Chanzo: Tanzania Daima Julai 1, 2009.

No comments: