The Chant of Savant

Saturday 27 June 2009

Sherehesho la hotuba ya bajeti


NAMSHUKURU Subhana. Bajeti yangu inazidi kusifiwa na wote. Bajeti hii ya ukombozi na uchaguzi imevunja rekodi kujadiliwa na kupendwa. Jamaa wa majoho wameipenda kiasi cha kutaka niwe mkuu!

Ingawa wasiojua uchumi na kuchuma waliiponda eti kwa kuondoa misamaha ya kodi kwa asasi zisizo za kiserikali na mawese, hawakujua tunabana matumizi ili kupambana na mvurugiko wa uchumi duniani!

Kama waziri wa pesa na kuchuma, najipiga kifua nikisema ni bajeti ya karne. Uliwahi kusikia wapi bajeti yenye kuwatengea walevi bilioni 19 kwa ajili ya chai na vitafunwa? Haijawahi kutokea duniani isipokuwa Bongolala.

Kama tunalia vile! Bajeti iko wazi. Mkiilinganisha na bajeti za nchi nyingine mtaona mantiki. Kwa wenzenu hakuna hata senti moja ya maji ya kunywa wakati ninyi mna mabilioni ya chai na mahanjumati!

Wenzenu wamepiga marufuku mashangingi. Sisi tunataka kuwapa raha. Tunazidi kuyanunua kama hatuna akili nzuri na sifa ya taifa letu inakua.

Kama mtatupa kula tena mwakani, mtegemee bajeti yenye pesa hata ya manywaji kwa sana. Tuliwaahidi maisha bora kwa wote. Sasa mnataka nini iwapo mnakunywa chai ya mabilioni?

Nchi yenu imeokoka na kuslimu. Ndiyo maana tumepandisha bei za ulevi kuwaepushia adha ya kulewa na kutwangana makofi, kutenda maasi na kupayuka hovyo.

Pia tumepandisha bei ya vinywaji baridi ili kuepusha magonjwa ya unene na kisukari. Ndiyo sababu nuzuhu ya kutenga mabilioni kwa ajili ya chai.

Kwa kunywa chai sana , tutapakuza soko ambapo wakulima wa chai watanufaika na nchi kuingiza mapato mengi. Pia nchi itaingia kwenye kitabu cha maajabu cha Guinness kwa kuongoza kunywa chai duniani.

Pia wapingaji wasije wahadaa. Hatujapiga marufuku soda. Mnaruhusiwa kunywa soda wakati wa sherehe.

Na kwa upande wa kilevi, wenye pesa na madaraka watakuwa wanakunywa kwa niaba yenu. Wao hata wakilewa hawatendi dhambi na wakizitenda wanasamehewa. Ni wateule wa Mungu.

Pia wananchi wataruhusiwa kunywa bia wakati wa kampeni za uchafuzi mwakani. Kipindi hiki hawawezi kuhesabiwa dhambi, kwa kitambo, watageuka wateule wa Mungu.

Nisisitize. Takrima mbofu mbofu zinapigwa marufuku. Atakayetaka kutoa takrima atoe suti badala ya fulana na kofia.

Atoe mbuzi mzima baada ya vipande vya nyama choma. Ili kushushia, waheshimiwa watabanwa na sheria watoe kreti ya bia badala ya bia moja moja.

Kuhakikisha hili linafanikiwa, napendekeza serikali itoe pesa chini ya kanuni ya bailout. Hii itawezesha wakubwa kupata mishiko mikubwa kwa ajili ya kufanya mambo makubwa wakati wa kampeni.

Kuonyesha tulivyo mbele ya wengine, tumekopa pesa hii kwa riba ya asilimia 11. Kwa vile tuna huruma na kuna uchaguzi, tutawakopesha wazito kwa riba ya asilimia mbili. Mungu awape nini jamani? Majipu siyo? Kwa taarifa yenu, tumeweka masharti rahisi ya uchukuzi wa pesa hii.

Hakika mwakani mtaona na kuonja maajabu. Lifti za mashangingi zitapigwa marufuku. Na badala yake zitatolewa lifti za ndege ili umma uonje raha tunazokula kwa niaba yake.

Pia serikali itaongeza mshiko tokana na kodi ya ongezeko na thamani (VAT). Baada ya kuzinyakua nyumba za umma tumeona tutoze kodi ya ongezeko la thamani kwa wapangaji ili wawe na uchungu wajenge nyumba zao. Kila nyumba hata iwe ubavu wa dog ikipangishwa tunaitoza VAT ili kukuza uchumi.

Ndugu zangu walimu hili lisiwatishe. Tumepanga kuwajengea nyumba za ghorofa kila ilipo shule. Tumewapendelea baada ya kichaa mmoja kuwalamba bakora.

Badala ya kuwanunulia watoto matoi yaitwayo vifaa vya maabara, tumeona tuanze nanyi. Hata kama watoto wataendelea kukalia mawe msilaumu.

Hatukatai kuwanunulia madawati. Tunataka wakalie mawe ili wasikie uchungu wa kusoma. Maana wakikaa kwenye masofa watajisahau kwa raha na mineso.

Pia tumepanga kuongeza marupurupu na mishahara ya waheshimiwa wabunge kama watapitisha bajeti hii bila ubishi na kuchokoana.

Ingawa mmoja wao juzi katulaani mawaziri, tumemsamehe na tumeishapenyeza watu wetu kumshughulikia ili asiendelee kupayuka hovyo.

Pia wafahamu. Bajeti itapita watake wasitake. Najua wapo waliokamia kuikwamisha wasijue sisi tuna akili na mamlaka kuliko wao!

Chini ya katiba yetu ya ulaji, tutamwambia Bwana Kipaza sauti Six atumie Ibara ya 90 kifungu cha pili sehemu 'B' ya Katiba, nanukuu: mkuu atalazimika kuvunja Bunge iwapo litakataa kupitisha bajeti iliyowasilishwa na Serikali.

Kwa vile waheshimiwa wetu hamna ubavu na hamjiamini kwenye majimbo yenu kutokana na tabia yenu ya kupenda kukaa Bongo mkifanya biashara zenu, ukiondoa wabunge wa upingaji, hakuna mbunge wa genge letu atafanya fyoko zaidi ya kupiga kura ya ndiyo.

Na hii ndiyo sababu tunajiandalia bajeti kwa kuangalia maslahi yetu. Tunajua wazi kifungu cha 90 kipo kuwatia adabu na mkafyata mikia. Upo hapo?

Isitoshe wahishimiwa wa Bongo na wabongo kwa mkwara nawajua sana mtapiga mikwara yenu uchwara lakini serikali itakapochimba wake mtanywea.

Mkijifanya kujua jua hata haya marupurupu tunayowahonga tunayanyofoa tuone kama mtakula polisi.

Angalia bajeti inavyowapendelea. Nchi nyingine zimepiga vita mashangingi. Sisi tunazidi kuwapa kama hatuna akili nzuri.

Nyinyi, kama tutalinganisha na kipato cha taifa letu, mna mishahara na marupurupu makubwa kuliko hata maseneta wa kwa Obama.

Kule ukiwa seneta au mwakilishi hakuna cha dereva, mfagiaji, shamba boy wala mlinzi kama tulivyowafanyia. Wala huko wenzenu hawapigiwi saluti kama nyinyi. Sasa mnataka serikali yenu iwape nini?

Nimalizie kwa kutoa ushauri kwa ndugu zangu wa majoho.

Mnajua ni kwa nini tumeondoa misamaha ya kodi? Pamoja na wenzenu wachache kuitumia kujitajirisha kama jamaa wa TRA, mmechonga sana mkitusakizia kuwa tunaongoza kifisadi na kifisi na hatupambani na ufisadi. Unadhani bila ufisadi kuna mtu angependa siasa. Shauri yenu.

Muda hautoshi. Naomba kutoa hoja na kukaribisha maoni.

Makofi kutoka kwa wahishimiwa hata kama mmenuna kwa kulazimishwa kupitisha silaha za maangamizi kwa pesa ya walalahoi.
Chanzo: Tanzania Daima Juni 24, 2009.

No comments: