The Chant of Savant

Sunday 14 June 2009

Ngeleja anamsemea nani kati ya Kikwete, Mkapa na Serikali?


HAKUNA utani na matusi mabaya kwa Watanzania kama uliokaririwa juzi kutoka kwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.

Ni kichaa gani hata kuku angekubali kuwa kuna watu na akili zao tena wanaojiita serikali wangepitisha uamuzi wa kijambazi kwa kuunusuru mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira ambao una utata baada ya kutwaliwa na rais mstaafu Benjamin Mkapa, familia yake na marafiki zake?

Hivi karibuni Waziri Ngeleja, alikaririwa akitangaza uamuzi wa serikali “kuinusuru’ Kiwira kwa kutumia pesa ya umma ule ule ulioibiwa mgodi huu! Kwa kutaka kutufumba macho na Ngeleja alisema, “Yaliyopita si ndwele, kubwa ni kupata umeme,” Yapi haya yaliyopita? Kama ni kashfa ya Mkapa bado haijapita. Ili ilipite si budi afikishwe mahakamani na mgodi kurejeshwa kwa umma.

Ngeleja aliendelea, “Tutaukwamua ule mradi ili uwe wa mafanikio kwa taifa na jamii yetu ya Tanzania kwa ujumla.” Hivi kwanini kila anayetaka kuuibia umma anajifanya mkereketwa wa taifa ambalo analibomoa?

Mafanikio kwa taifa ni kuwakamata mafisadi waliaojitwalia Kiwira. Kama kuna taifa hapa si jingine bali lile la mafisadi wanaopitisha maamuzi ya kijambazi kwa kusingizia taifa.

Kwanini serikali iliyojitoa kwenye uchuuzi inajifanya msemaji na mwokozi wa Kiwira na isiwe hujuma dhidi ya umma?

Wakati mkitenda kufuru hii mkubuke. Ni serikali hii imesamehe kodi zipatazo sh 687,000,000 ndani ya miezi 10.

Hii ni sawa na aslimia 30 ya makusanyo yote ya kipindi hiki. Na ni sawa na aslimia 30 ya utegemezi wa bajeti yetu kwa wafadhili. Serikali hii ndiyo imefutika wizi wa EPA na wizi mwingine mkubwa chini ya busati! Je hii serikali ni ya nani kati ya kikundi cha wezi wachache wenye madaraka na wananchi?

EPA, Richmond , IPTL, TICTS na sasa Tanpower mnazidi kufutika chini ya busati na kuiba zaidi! ‘No. This is unbearably too much’.

Ngeleja, amelidanganya Bunge na taifa zaidi ya mara tatu kuwa angewafichua wamiliki wa Kiwira. Lakini mara zote amepiga dana dana na kufunika kombe! Na kama shida ni umeme, kwani Kiwira ndicho chanzo pekee?

Hapa tuambiane ukweli kuwa msimu wa uchaguzi umekaribia na vinatafutwa vyanzo na sababu za kupatia pesa kutoka kwenye hazina ya umma. Haiingii akilini serikali yenye hisa aslimia 30 ibebe mzigo wa kuokoa mradi ilhali mwenye hisa aslimia 70 amekaa tu.

Kisheria mwenye hisa nyingi ndiye mwenye majukumu na mapato mengi. Hata kwenye kuendesha mradi na kutoa maamuzi mwenye hisa nyingi ndiye mwenye sauti. Sasa inakuwaje kanuni hii inapindwa kama hakuna namna?

Tunaambiwa Kiwira Coal and Power Company (KCPC) ambayo ni kampuni tanzu ya Tanpower inamilki asilimia 70. Na hii ni kampuni inayodhaniwa kumilkiwa na Mkapa, familia yake na marafiki zake.

Je inakuwaje serikali inakubali kuingia ubia na kampuni zinazoshutumiwa kupatikana kifisadi tena kwa kuhujumu wananchi inaodai kuwatetea na iliyoapa kuwalinda wao na mali zao?

Kabla ya kodi yetu kuibiwa, waziri atwambie nani wamilki halali wa Kiwira na jinsi walivyoipata. Haiwezekani watu waibe mali ya umma kwa malipo ya sh 70,000,000 badala ya 4,000,000,000 halafu tuwaongezee pesa nyingine pasiwe na mchezo mchafu unaowahusisha wakubwa wetu wa sasa.

Isijekuwa wanaposema familia na washirika wa Mkapa wakamaanisha na mawaziri wake wa zamani ambao wengi ndiyo wanaunda Baraza la Mawaziri la sasa.

Je, bado serikali kwa kukopa maneno ya Mkapa, inadhani Watanzania ni wavivu wa kufikiri kiasi cha kutenda kufuru hizi?

Tuweke msisitizo. Kama serikali haina mpango wa kutuibia, isitoe hata senti moja kwa Kiwira hadi tujue nani mmilki wake na alivyoipata.

Hii ni sawa na jambazi anakuteka anaiba gari lako baada ya kukujeruhi halafu analigongesha na kuja kukuomba pesa ya kulitengenezea. Nawe, kama kichaa, unampa. Hata kuku, pamoja na kuwa na ubongo usiojaa kijiko, hawezi kufanya upuuzi huu.

Piga ua. Hii ni njama ya wakubwa wenye madaraka kutaka kutuibia ili kupata pesa ya kuhonga kwenye uchaguzi. Hakuna maelezo mengine yanayoweza kuingia akilini.

Ingawa rais Kikwete, kwa sababu anazojua mwenyewe, ameendelea kumkingia kifua Mkapa, wabunge wetu nasi kwa ujumla wetu tusimame imara na kuondosha wizi huu.

Ikiwezekana, kama hatajirudi, tumpigie kura ya kutokuwa na imani naye. Maana amekuwa kichaka cha uhujumu wa taifa na wizi wa pesa zetu. Atuambie anatawala kwa ajili ya nani kati ya wananchi na hayo makampuni ya kutia shaka anayokingia kifua.

Ni aibu na hasara kuwa anamaliza miaka mitano bila kutekeleza hata ahadi moja! Yako wapi marekebisho ya mikataba ya kijambazi ya uwekezaji iliyowawezesha kina Mkapa kutwaa mali ya umma? Iko wapi vita ya kupambana na ufisadi iwapo Kagoda inaendelea kuwa serikali ndani ya serikali?

Muhimu, kwa wahusika kutia maanani ni kwamba hata huko Madagascar na kwingineko umma ulipoasi utawala vidhabu walianzia huku tuliko. Kuna mwisho na unakaribia kama wananchi watatambua kuwa kikwazo cha maendeleo na majaliwa yao ni serikali za namna hii zinazo lala kitanda kimoja na mafisadi.

Huwezi kupora mali ya umma na bado ukawa na upogo wa kuchota pesa ya umma ule ule kuwakomboa waliouibia ukaendelea kudai unaujali na kuuheshimu. Hili ni tusi la nguoni kwa umma.

Huwa nauliza swali hili mara kwa mara. Je Watanzania washikwe wapi au wadhalilishwe na kuhujumiwa vipi ndipo wasimame na kuondosha dhuluma? Ajabu akitokea mtu akasema wezi na kina fulani, wanaamka mawaziri, bila aibu, kumtisha wakiwakingia kifua wezi!

Je hawa si wezi wenzao? Je hawa wanafaa kuendelea kuwa kwenye ofisi za umma wanaouhujumu? Wizi wa Kiwira utufungue macho tuasi. Hata farasi hufikia mahali akakataa kubebeshwa mizigo anapogundua anadharauliwa.

Muhimu, serikali iwafikishe mbele ya sheria wezi wa mali za umma badala ya kupanga kuwaongezea pesa nyingine kwa kuvunja hazina ya umma.

Na kama wabunge watabariki wizi huu watajivua uhalali wa kuwasemea wananchi. Watakuwa wameuonyesha walivyo kwenye madaraka kulinda mafisadi huku wakiuhujumu umma wanaotaka uwachague tena.

Isitokee. Shame on them!
Chanzo: Tanzania Daima Juni 10, 2009.

No comments: