The Chant of Savant

Thursday 2 April 2009

Kikwete, lini utatangaza mali zako?


HIVI karibuni, rais wa Urusi, Dimitry Medvedev, alitangaza azma yake ya kuweka wazi utajiri na mapato ya familia yake ikiwa ni kuthibitisha dhamira yake safi ya kupambana na ufisadi.

Ikumbukwe. Rais huyu ameingia madarakani jana ikilinganishwa na rais Jakaya Kikwete ambaye tunapoandika kipindi chake kinaisha huku hajatangaza mali zake na familia yake. Hakika hii inaleta utata ukiachia mbali kushindwa kutimiza ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi wa 2005.

Na bila shaka alichaguliwa kutokana na ahadi alizotoa ingawa zimegeuka kuwa sanaa kama wasemavyo watani wake.

Kuwakamata mafisadi kutokana na ukaribu nao kumemshinda rais. Hata kutangaza mali zake nako ameshindwa! Hivi mwakani wakati wa uchaguzi atawambia nini Watanzania wamwelewe? Je Kikwete anaogopa nini kutangaza mali zake?

Pamoja na ufisadi wake, Benjamin Mkapa angalau alitangaza mali zake ingawa nayo ilikuwa kama danganya toto. Kwani baada ya kuchuma hakufanya hivyo alipokuwa akiondoka madarakani.

Tukubaliane. Mtu anayeshindwa au kuogopa kutaja mali zake na familia yake hawezi kuwa safi wala kupambana na ufisadi licha ya kutoa mfano mbaya kwa walio chini yake kama tunavyoona kwenye ukimya wa Kikwete ambao umekuwa kiota cha ufisadi.

Kitu kingine ambacho kinatia wasi wasi kuwa Kikwete hawezi kupambana na ufisadi zaidi ya kuwa kikwazo cha vita hii ni ile hali ya mkewe kuwa fotokopi ya Anna Mkapa.

Hakuna ubishi. Mzee Mkapa sasa yumo msambweni kutokana na tamaa za mkewe na nduguze. Hili limejirudia kwa Kikwete. Mkewe, Salma Kikwete sasa anaendesha NGO mashaka iitwayo WAMA. Nimewahi kumwandikia kuonyesha kutoridhika kwangu na biashara hii ambayo ni ufisadi wa kutumia vibaya ofisi ya rais. Bahati mbaya hadi naandika hajanijibu.

Kwa nini nasema Salma hana tofauti na Anna? Kwanza ameonyesha wazi anavyopenda kutumia madaraka ya mumewe. Soma logo ya WAMA kwenye wavuti yake ya wamafoundation.or.tz.

Kuna maneno yasemayo ‘WAMA Foundation the office of the First Lady of the United Republic of Tanzania.’ Kisheria hakuna ofisi ya ‘First Lady of the United Republic of Tanzania.’ Fungua katiba yetu viraka. Pamoja na udhaifu wake haina mamlaka haya. Je yanatoka wapi na kwa nini rais anaridhia yawepo kama hana faida nayo?

Tumeona kwenye sakata la kashfa zinazomkabili Mkapa kuwa nyingi zimeasisiwa na kutekelezwa na mkewe. Na tunashangaa kwa nini Kikwete hataki achukuliwe hatua. Je haogopi na mkewe baadaye yasimkute ambayo yanapaswa kumkuta Anna Mkapa? Je mtu wa namna hii anaweza kupambana na rushwa wakati imejaa uvunguni mwa kitanda chake?

Hata ukisoma ‘pre-amble’ ya WAMA hukuti popote iliponukuliwa sheria iliyoanzisha WAMA! Hata ukiangalia wavuti wa EOTF ya Anna Mkapa ya eotfz.org hakuna kitu kama hiki.

Huu ni ushahidi kuwa, NGO hizi zilizoanzishwa baada ya waume zao kupata madaraka, hazipo kisheria na zipo kama ofisi za mfukoni za kujineemesha. Anayepinga hili anipe ushahidi kisheria. Je madaraka ya rais hapa hayajatumika vibaya tena dhidi ya wale waliomchagua?

Huu ndiyo utawala wa kienyeji aliosema Hassy Kitine ingawa hakufafanua. Huu ndiyo upogo na kile wazungu huita myopia kama siyo mania.

Kuna haja ya kuliangalia suala hili kwa umakini. Kuwa karibu na rais isiwe waranti ya kujitajirisha kwa kulihujumu taifa. Muasisi wa taifa hili Mwl. Julius Nyerere aliwahi kumkaripia aliyemfuatia zilipoibuka shutuma kuwa mkewe alikuwa anatoa vimemo kwa watu kwenda kuchukua mikopo benki.

Hii ilimkera sana Mwalimu kiasi cha kuonya; msipende kusikiliza ushauri wa wake zenu. Mambo ya chumbani yasitumike kuamua au kuendesha mambo ya taifa, na kweli, Mwalimu kwa kipindi chote cha urais wake hakuruhusu madaraka yake yatumiwe vibaya na familia yake.

Leo tuna watu wamejaza watoto na wake zao kwenye ulaji chamani na NGO halafu watu hawa hawa watuhadae wanaweza kupambana na ufisadi. Huu ndiyo usanii wanaosema watoto wa mjini.

Kisaikolojia, taifa lipo kwenye kuelekea katika uchaguzi mkuu wa mwakani. Je kama Kikwete ameshindwa kutaja mali zake kwa miaka mitano akitegemea kugombea tena, atafanya hivyo kwenye ngwe ya mwisho ambayo mara nyingi watawala mafisadi huitumia watakavyo wakijua hawatasimama tena kwenye uchaguzi.

Rejea Mkapa alivyochapa kazi vizuri kipindi cha kwanza akaivuruga vibaya kwenye lala salama ambapo mazimwi na ujambazi kama EPA, Tanpower, ANBEN, Fosnik na mengine yaliasisiwa. Je Watanzania bado tunajirahisi na kujiruhusu kumpa Kikwete ngwe ya pili atufanyie aliyotufanyia Mkapa?

Mpumbavu ni yule ang’atwaye mara mbili kwenye tundu moja au awekaye mayai kwenye kapu moja. Je tu wapuuzi kiasi hiki?

Kuna kashfa zinazohusisha chama cha Kikwete yaani CCM. Chama chake kimetajwa kwenye kashfa karibu zote zinazohusisha wizi wa mabilioni ya pesa lakini hakijatoa utetezi kwa vile ushahidi ni kile wanasheria huita ‘water tight.’ Hili likiongezea kwenye ukimya wa Kikwete na hali ya familia yake, kama watu watatumia akili vizuri, ndiyo inammaliza kabisa.

Je kuna haja ya kuirejesha CCM iliyoshiriki kwenye Kagoda, EPA, Meremeta, Deep Green Finance na hata Richmond ambaye alikuwa mbia wake kwenye mradi wa kujenga bomba la mafuta toka Dar es Salaam kwenda Kigoma na Mwanza ambao uliishia kuwa wizi mtupu?

Leo sitasema mengi. Natoa changamoto kwa Kikwete kutangaza mali zake kabla ya kumaliza muhula huu ili hata atakapogombea angalau tujue kama ni safi au la. Hili la mkewe kuwa na NGO halimsaidii zaidi ya kuwa kishawishi. Ni kipofu kiasi gani kuanguka alipojikwaa jana Mkapa?

Kwa wananchi, uchaguzi wa mwakani, ajenda kuu iwe ni nani anafaa kupambana na ufisadi maana tumechoka na usanii na ufisadi.
Chanzo: Tanzania Daima Apr. 1, 2009.