The Chant of Savant

Tuesday 17 February 2009

Jamhuri ya mgongano wa kenge wenye makengeza

JUZI mzee mzima nilikuwa natafakari. Mara naiona nchi nzuri tu kwa juu ing’aayo kama kaburi wakati ndani ni mifupa na uozo mtupu!

Ni nchi iitwayo Jamhuri ya Mgongano wa Makenge wenye makengeza. Unajua ukiwa na makengeza hasa ya ubongo ukiachia mbali ya macho unakuwa huoni wala kuhisi vitu kama vilivyo. Nyuma unapaona mbele na mbele nyuma. Kiama unakiita neema na neema kiama.

Ukinyonywa unajiona unanenepeshwa na ukidanganywa unajiona umeambwa ukweli! Huu ndiyo ukenge uletao mgongano kiasi cha Jamhuri ya Makenge kengeza kuonekana kituko kitupu.

Majirani wa nchi hii huicheka na kuikebehi watakavyo. Wapo waliowahi kuifananisha na kusanyiko la makaburi au hata mainzi mafu. Sababu? Watu kuishi maisha ya kikondoo kiasi cha kutendewa kila upuuzi wasiamke na kufanya kweli.

Jamhuri hii iliyojaa makenge wenye makengeza makubwa hufanya mambo kikengekenge. Ilijaliwa madini si haba. Lakini waulize wana makengeza kama wanafaidika na madini yao. Afadhali hata ya Tanzania tuna wawekezaji wanaoweza kuwagharimia mawaziri wetu safari za kwenda kukaa kwenye mahoteli ya kitalii huko London kwa mama na Uswisi kupanga madili.

Hebu fikiria kwa mfano upuuzi alioufanya juzi spika Sammy Six kuzuia miswaada binafsi ya kuwawajibisha Makenge wajifichao nyuma ya utukufu. Nani hajui kuwa Makenge kama Johanson Mwananyika na Eddie O’shea ni mafisadi? Wanangoja nini kwenye ofisi za umma?

Kwanza, inabidi tumpe taarifa. Yake tunayajua alipokuwa Mkurugenzi wa The Insititute of Corruption (TIC). Alikwapua njuluku na kujenga mahekalu kule Masaaki. Tunalijua hili. Tunajua alivyo mchafu na mshirika wa majambawazi tajwa.

Anyamaze vinginevyo kijiwe kitamchukulia hatua. Pia aelewe nina mpango wa kuanzisha vuguvugu na kuwa mwanasiasa ili nieleweke, maana kila nikipiga vijembe wanajifanya hawapati kitu. Nitaanza kupayuka kama akina Mremax.

Turejee jamhuri ya mgongano wa Makenge wenye makengeza. Heri ya Tanzania ina serikali yenye heshima inayoweza kumiliki maelfu ya mashangingi na ndege ya bei mbaya kuliko Jamhuri ya Mgongano ya Makenge wenye makengeza inayotawaliwa na kuliwa na mfalme na watu wake watakavyo.

Wanaweza kufanya kila upuuzi bila kuulizwa wala kuwajibishwa. Nani amesahau kufuru ya kina Eddie Ewassa na Ben Makapu Tunituni na Anna Tamaa aliyerithiwa na hatari aitwaye Salama Kikwekwe?

Huyu mama anadhani hatujui anavyoiba kupitia kwenye mashirika ya hiari? Mbona Michelle Obama hafanyi upuuzi huu? Hawezi kwa sababu amekula vitabu na siyo mroho kama hawa kina Tamaa na Hatari wetu. Anaona mbele. Haoni usawa wa pua kama Six, Kikwekwe na majambawazi wenzao.

Kutokana na mwanya huu, watawala wa Makengeza ni wakwasi wa kutupwa. Wanakula na kusaza huku wananchi wakitopea kwenye utapiamlo. Hawana utapiamlo wa chakula tu bali hata mawazo. Huu umewakumba hata watawala ambao ukiuliza faida ya uwepo wao si chochote bali maangamizi.

Watawala wa Makengeza wanaweza kwenda benki kuu ya Makengeza na kujichotea pesa watakavyo bila kushitakiwa! Watawala hawa vidhabu wamejichotea mabilioni ya pesa kiasi cha kulihonga hata jeshi ambalo haliwezi kuwafanya kitu. Mambo ya nchi ya Makengeza yangefanyika Guinea bila shaka Mousa Dadis Camara asingevumilia.

Makufuru ya Makengeza yangefanyika Afrika Kusini, Mosioua Terror Lekota asingeacha kuasisi chama na kuunda chama kipya ili kupambana na watawala wa Makenge kengeza. Makengeza inahitaji kina Lekota milioni moja. Inahitaji watu wasio vyongo wala makengeza kuona makengeza yanayofanyika nchini Makengeza.

Ajabu wakati kufuru ambayo haijawahi kutendeka popote ikiendelea, wana Makengeza wanaaminishwa kuwa mambo ni safi si kawaida. Wanaambiwa hawana Makengeza bali kuitwa wana Makengeza ni utani unaomaanisha kinyume wakati siyo!

Kuishi kwenye nchi ya Makengeza ni hatari kuliko hata Baghdad. Ukiwa una ulemavu wa ngozi ndiyo usiseme. Ukizeeka baada ya kunyonywa jua utanyongwa kama mbwa ukidhaniwa mchawi wakati wachawi ni watawala, hii ndiyo hasara ya kuwa na makengeza. Mwenye nayo huona ndiyo siyo.

Nchi ya Makengeza ni sawa na ile rais wa zamani wa nchi tukufu ya Tanzania mzee Ali Hassan Mwinyi aliilinganisha na kichwa cha mwendawazimu walevi kujifunzia kunyoa. Kadhalika na makengeza imebakwa na vibaka kiasi cha kutokuwa na tofauti na kundi la mainzi mafu.

Uliona wapi mwizi anaitwa mheshimwa hata kama ni mwizi mkubwa kama Tunituni, Ewassa, Kagodamn Roast Tamu L’Aziz? Uliona wapi mtu anashutumiwa kwa wizi anaendelea kukaa ofisini akiiba na kuharibu kumbukumbu kama Johanson Mwananyika na Eddie O’shea?

Ni katika Jamhuri ya Mgongono wa Makenge wenye makengeza tu. Uliona wapi Karumekenge akiiba kura na kuendelea kuula huku akiwaambia wapingaji wameula wa chuya? Jibu unalo nimeishatoa. Kazi kwenu wajameni.

Uliona wapi mwizi anaanzisha magazeti kuwachafua wenzake akabaki kuwa mwakilishi wa wale anaowaibia? Basi kama hujui, hii ni jamhuri ya mgongano ya Makengeza. Nchini Makengeza wezi na majambazi huitwa waheshimiwa huku waadilifu wakiitwa washamba. Katika nchi hii laanifu ujanja ni kupata hata kama kupata kwenyewe ni matokeo ya ufisadi na uuaji wa watu wasio na hatia.

Katika nchi hii, wakubwa hula watakavyo huku wadogo wakiliwa kadri ya wakubwa watakavyo. Hii haina tofauti na nchi ya hayawani waitwao samaki ambao mkubwa humla mdogo na mdogo humla mdogo zaidi.

Katika nchi hii, ubongo hauna kazi zaidi ya kutenda jinai. Rejea daktari mmoja wa uchumi aliyewahi kuruhusu majambazi naye akiwamo kuibomoa benki yake na hatimaye akatundikwa sumu akaishia kufa kama mbumbumbu.
Chanzo: Tanzania Daima Februari 17, 2009.


Kufuru na upuuzi wa Jamhuri ya Mgongano wa Makenge wenye makengeza ni mengi. Huwezi kuyaelezea kwenye ukurasa mmoja wala kwa siku moja. Tumewaambia Makenge waachane na ukenge na makengeza wajikomboe. Lakini hawatueliwi! Wataelewa lini? Ipo siku.

Naona macho yanauma. Huenda naambukizwa makengeza! Wacha nikitoe kabla ya jamaa hawajaja kunikolimba hata kunibalali.

No comments: