The Chant of Savant

Tuesday 20 January 2009

Hongera padri Karugendo kukata mikatale


Uamuzi kuwa padri Privatus Karugendo kavuliwa upadre umejadiliwa sana na watu wengi. Wengi wameupokea kwa hisia tofauti kulingana na imani na maoni yao . Ila kuna kitu kimoja wengi hawa wanakubaliana-KARUGENDO ameonewa. Mimi nilimtumia ujumbe wa kumpongeza na kumwasa asijione kama kashindwa bali kashinda kifungo cha ukimya na unafiki.

Kinachotusukuma kuamini hivi ni ile hali ya kuhukumiwa bila kusikilizwa. Kisheria husema uamuzi huu ni exparte. Mara nyingi hii hufanyika pale mshitakiwa anaposhindwa kuwasilisha utetezi wake. Je padri Karugendo alitakiwa afanye hivyo akashindwa au kugoma? Hasha. Kama alivyoeleza kwenye makala yake yenye kusikitisha na kufikirisha, ametumikia kifungo cha miaka ziaidi ya tisa bila kupewa nafasi hii ambayo ni haki ya binadamu bila kujali ana dini au la.

Na kwa msingi huu basi ndipo wengi wanaona ameonewa. Na hakika uamuzi huu licha ya kumwaibisha papa Bendikto XVI ambaye ni gwiji la mabadiliko katika kanisa. Je papa alipitiwa au ametumiwa kama mhuri kumaliza ngoa na visa vya bosi wa Karugendo, askofu wa jimbo la Rulenge Severin NiweMugizi? Je hatu hii inalijenga kanisa au kulibomoa? Mbona Yesu alipoletewe yule mwanamke aliyetuhumiwa kwa uzinzi alimtaka maelezo na ndipo akaamua-ASIYE NA DHAMBI AWE WA KWANZA KUTUPA JIWE.

Hadi tunaandika, Kanisa la Vatikana chini ya Rais wake, Papa Benedicto XVI linafanya mashauriano na baadhi ya wanamapinduzi ya kiroho juu ya sakramenti takatifu ya ndoa. Harakati hizi kwa upande mwingine zinaongozwa na Askofu mwenye mke, Emmanuel Milingo toka Zambia ambaye ameunda jumuia yake iitwayo Married Priest Now (MPN).

Ulimwengu unakumbuka jinsi gwiji huyu wa theolojia na uponyaji alivyolitia kanisa msambweni pale alipoamua kuachana na ukapela na kumuoa Daktari Maria Sung (48), toka Korea ya Kusini. Ndoa hii iliyofana ilibarikiwa na Mchungaji Sung Myung Moon wa kanisa la Unification mwaka 2001.

Kanisa kwa nguvu zake zote lilifanikiwa kumrubuni na kumrejesha Milingo kwenye kundi. Katika hatua hii mwezi Augusti 2001 alimkana mkewe na kurejea Vatikan alikofanya maombi na kufunga kabla ya kupelekwa uhamishoni nchini Argentina .

Kwa mara ya kwanza wakati huo, kanisa na Bi Milingo waliingia mvutano usio wa kawaida hasa pale Mke wa Milingo Daktari Maria Milingo alipodai kuwa kanisa lilikuwa limemteka mumewe.

Kwa kitambo kidogo kanisa liliona kama limeshinda kumbe wapi. Maana baadaye Milingo alimrudia mkewe na kuendelea na kazi yake ya uponyaji na kuishi maisha ya ndoa.

Mlingo mwanamapinduzi na mwanatheolojia asiyeshindwa na anayejua anachofanya, ameibuka upya jijini New-York akiwa na mkewe. Amekwenda maili moja mbele kwa kuanzisha jumuia inayoitwa "Married Priests Now".

Kanisa limemtimua tena baada ya kuwapa daraja la uaskofu mapadre wanne waliooa nchini Marekani. Ambao ni Rev. George Augustus Stallings Jr wa Washington, Peter Paul Brennan wa New York, Patrick Trujillo wa New wark New Jersey na Joseph Gouthro wa Las Vegas Nevada.

Katika kutaka upatanisho Milingo alikaririwa akisema : Hakuna upatanisho mzuri kama na kulinusuru kanisa kama kuangalia familia na ndoa. Kuna mapadre zaidi ya 150,000 waliooa.

Milingo ameishaitanga jumuia yake na ameishakutana na mapadre waliiooa zaidi ya 1,000.

Tukirudi kwa Karugendo, kuna haja ya kanisa kuanza mchakato wa kujali upya useja kwa kuzingatia maneno mtume Timetheo ambayo tutayakariri huko mbele.

Wale wanaopinga useja kwa makasisi wanadai kuwa hata Papa wa Kwanza, ( kama kanisa linavyotuaminisha),Petro alikuwa ni mtu aliyeoa. Vile vile ukisoma Biblia hakuna sehemu hata moja Mungu anapozuia Mapadre kuoa wala Masista kutoolewa.

Kitu kingine kinachofanya wanaopinga useja wa kulazimishwa kwenye kanisa la Roma ambao umekuwapo kwa takribani miaka 1,000, ni kuongezeka kwa kashfa za uzinzi na ulawiti miongoni mwa Mapadre na uzinzi kwa Masista. Karugendo amekuwa muwazi na kuepuka dhambi ya unafiki. Je ni mapadre na maaskofu wangapi wana vimada wao hata watoto? Kuna padre mmoja mwenye majina ya SNM ana mtoto Arusha.

Tukariri maneno ya Timotheo kwenye 1 Timotheo 3:1-12 anasema ukiitaka kazi ya uaskofu umetaka kazi njema.

Askofu awe mume wa mke mmoja,mtu wa makamo,asiwe mpenda mvinyo na pesa na mtu anayeweza kuitiisha familia yake. Je maaskofu wa Kikatoliki wanazo sifa hizo?

1 Timotheo 4:1-4 roho asema wazi kuwa kutakuja wakati wengi wataanguka wakizitii roho chafu na itikadi za kishetani.

Kwa kutumia unafiki wa waongo tena kwa ugumu wa chuma. Wanaozuia ndoa na kutetea kuacha kula baadhi ya vyakula....

1 Timotheo 5: 9-11 kwa watawa au masista awe na umri si chini ya miaka 60 kwani chini ya hapo bado anahitaji kuolewa na kuzaa watoto.

Je masista wetu wapo?

Kwa vile wengi wameishatia mikono kwenye kesi ya Karugendo, tutatumia historia kama shahidi ili umma na kanisa viamue upya na vizuri.

Papa Paulo V (1605-1621) Alipotaka madanguro yote ya Roma iliyokuwa na watu 100,000 na madanguro 6,000, waumini walikuja juu wakisema kuwa kufanya hivyo kutafanya mapadri wawatongoze wake zao.

Papa Grigori XV (1621-1623) Alipoamru kisima karibu na nyumba ya watawa kikaushwe, alishtuka kukuta mafuvu ya vichanga zaidi ya 6,000.

Kardinali Peter D'Ailly aliwahi kusema kuwa kuvaa joho la usista ni sawa na kutangaza kuwa u kahaba wa jamii.

Albert The Magnificient wa Humburg Ujerumani, mnamo mwaka 1477 alipigwa na butwaa baada ya kugundua kuwa wanawake wapatao 11,000 kwenye jimbo lake walikuwa wamewekwa kinyumba na watawa. Msemo kuwa Padre ni kuwa mume wa wanawake wote ulianzia hapa na ukawa na maana zaidi ya inayoeleweka.

Akiwaonya Mapadre wake Albert alisema "Si non caste,tamen caute" yaani kama huuwezi utaua basi uwe mwangalifu. Yaani ufanye mambo yako kwa usiri. Je huu ni usiri au unafiki? Karugendo kalishinda hili.

Hivyo basi ni wakati muafaka wa kulirudisha kanisa kwenye ukweli kwa kuruhusu Mapadri waoe na Masista waolewe. Tena itakuwa rahisi maana wawili hawa wanajuana vilivyo ni suala la kutangaza kuachana na usiri na unafiki vinginevyo tendo lipo na halina ubishi.

Kufanya hivyo kutarejesha hata imani ya waumini kwa watumishi wa Mungu ambao kusema ukweli kwa sasa ni hatari na uzembe kuwaamini hasa katika masuala ya ndoa au kuwa karibu na wapendwa wetu.

Kwa machache haya kuna haja ya kumpongeza ndugu yetu na padri wetu Privatus Karugendo kukata mikatale na kuushinda unafiki. Na isitoshe, huu siyo mwisho wa maisha na ajuaye nini kitatutokea siku ya mwisho si mwana wala nani isipokuwa baba mwenyewe. wengi.

Amwachie baba baada ya kanisa lake kumuangusha . Asirudi nyuma. Aandike na kuelezea aliyoona ni dhambi kuyaeleza. Atasaidia. Mwanzo wa kushinda mawazo mgando ni kuasi na haya ndiyo matokeo ya kuelimika vilivyo. Akina Yesu, Plato, Sophocles, Martin Luther na wengine walikuwa waasi walioshia kuwa wateule.

No comments: