The Chant of Savant

Wednesday 7 January 2009

Hamchoki kuongopa na kuongopewa!

Akalung’wando kakazungwa n’untwe
Akalung’wando kakazugwa n’untwe Kalug’wando.

Elinumbu’itale lyantoloowima
Elinumbu’itale lyantolowimama elinumbu.

Tafsiri
Sungura mjanja alipikwa na kichwa chake
Akaliwa pamoja na kiazi kinene

NIKIWA natokea kusherehekea kumalizika kwa mwaka mpya huko Bunda palipogeuka Bonda, nilianza kujiimbia wimbo huu wa busara. Nilifanya hivyo kuonya juu ya ujanja mwingi ambao mwisho wake huwa kiza.

Baada ya kufika nyumbani kwa mshirika wangu wa bedroom na kujipongeza nijuavyo-usiulize vipi-niliamua kuangalia mwaka uliopita ulivyokuwa huku nikitupia jicho kwenye nasaha za mkuu.

Sungura mjanja aliliwa na kiazi kinene sawa na walevi wanavyoliwa na mabonge ya dhahabu! Hayo tuyaache.

Baada ya mkuu kuja na tathmini kapa isiyo kufu iliyousifia mwaka ulioisha, nami kama rais wa wapayukaji natoa tathmini yangu ya mwaka wa mauza uza; nikongojea yatakayojiri kwenye mwaka ngwengwe tuliouanza kikaya.

Nianze na mauaji ya kinyama ya watu wenye ulemavu wa ngozi. Walichinjwa kama swala huku jamaa akimteua mmoja wao kuula asijue hii ni vunga. Mbona walevi wana wawakilishi lukuki lakini bado wanaula wa chuya?. Kinachotakiwa si kuteuana bali kuhakikisha usalama wa kila mwana kaya. Nyie ngojeni.

Siku wakiwanyonga wazungu wakidhani ni mazeruzeru huenda kwa vile mnawaabudia mtazinduka na kuachana na sanaa.

Njaa Kaya anafanya sanaa! Mwaka uliopita ulikuwa mbaya sana kwa walevi waganganyika. Maana aliwaficha akina Kagodamn wakaendelea kutanua na bilioni zaidi ya 40 za wachovu. Pia lisirikali liliendelea kufanya madudu hasa kwenye matumizi ya pesa ya umma. 2008 ulishuhudia kuzikwa kwa Air Tanzia ukiachia mbali mashirika mengine.

Ngoja tumnukuu kidogo uone sanaa zinavyotembea. “Bahati nzuri kaulimbiu hii inawiana na mpango wangu wa kazi nilipoingia madarakani. Nilikuwa nimepanga kuwa, katika nusu ya kwanza ya kipindi changu cha uongozi tuelekeze nguvu zetu katika upatikanaji wa huduma za kiuchumi na kijamii, na nusu ya pili tushughulikie kukuza uchumi,” alisema mkuu.

Je, kwa kuidedisha Air Danganyika ndiko kuleta hizo huduma za jamii na kiuchumi? Kama ndivyo, hizo huduma zimepatikana kwa nani zaidi ya mafisadi wachache? Hata mkii-‘bail-out’ si jibu. Kamateni walioidedisha. Huu nao wizi mwingine na matumizi mabaya ya pesa ya wachovu.

Tuangalie mipango ya nusu ya pili ya ulaji wake. Alisema angeshughulikia uchumi! Mwe! Tunageuzana majuha mchana kweupe! Mbona ngwe ilishaanza na hatuoni chochote zaidi ya kuzidi kufichuka wizi wa kutisha. Rejea kubumburuka kwa wizi wa CIS ambapo zaidi ya bilioni 500 zilirambwa.

Mwaka 2008 ulishuhudia umma ukitaka Denjaman Makapu, mkewe, watoto na wezi wenzake waadhibiwe lakini mkuu aliwakingia kifua kwa vile anafanya sawa nao.

Mwaka 2008 tulisuluhisha migogoro ya vijiwe vingine tukashindwa wetu kule Zenj.

Funga kazi ni kwamba mwaka 2008 zilifunguliwa kesi hewa dhidi ya mafisadi waliotumia madaraka vibaya badala ya kuhujumu uchumi. Pia tulishuhudia kuongezeka kuibiwa kwa raslimali za kaya hasa dhahabu kule Ukuryani ambako hata damu ilimwagika. Hii ndiyo amani anayoongelea mkuu?

Mwaka 2008, mkuu hakutimiza ahadi hata moja. Wadanganyika walijiona walivyotwikwa mkenge wazi wazi. Ajabu badala ya kutimiza ahadi mojawapo kupambana na ufisadi, anatoa onyo kwa wanaomwambia ukweli kuwa tusije tukalaumiana! Tisheni mafisadi hata kama ni shirika moja.

Kama kuna mafanikio ni mkuu na mkewe kuongeza uzito huku akina Dadi Ballalii wakifishwa ili kwenda na EPA.

Katika kuonyesha ukweli wa hili, mkuu aliumaliza mwaka akiuanza mwingine eti kwa kutoa onyo kwa wanaojihusisha na ufisadi badala ya kuwaweka lupango!

Mimi nilishusha bei ya kahawa. Wakati kaya nyingine zikipunguza bei ya mafuta yeye walevi waliachwa waendelee kulanguliwa na wezi na wachoyo. Hii ilisababisha kupanda gharama za maisha ukiachia mbali bei za bidhaa muhimu kama chakula na nauli za mabasi.

Bongo daladala walipandisha nauli zaidi ya mara tano kwa mwaka mmoja huku mkuu akichekelea! Unajua alijiteteaje? Eti kutoshuka kwa bei za mafuta kunatokana na ukaidi wa baadhi ya wafanyabiashara! Ukaidi au wanakata pochi sana!

Mwaka 2008 wanywaji kahawa tegemezi sawa na wanakaya wanaotegemea kusaidiwa chakula na lisirikali waliongezeka. Tuliwambia muimarishe kilimo. Mlikazania uwekezaji kwa vile mnapata ten pasenti.

Angalia nchi yenye mito, maziwa na watu wenye nguvu inakuwa na watu tegemezi hata wa mlo. Ni aibu kwa mswahili kuwa tegemezi wa msosi.

Mkuu alisema mwaka uliopita ulikuwa wa amani na utulivu, si kweli. Hivi kweli mazeruzeru nao waliuona kama mwaka wa amani na utulivu au vifo na kugeuzwa bidhaa? Mwanakaya mmoja anapokosa amani, wote tunaikosa. Maisha yake yanapokosa maana, yetu sote yanakosa maana.

Mwaka 2008 ulishuhudia uongo wa mwaka katika historia ya kaya. Waziri mkubwa Mizengwe Punda alisema: lisirikali lingepunguza mashangingi ya mashangingi ya kisiasa ili kumpunguzia mzigo mwana kaya. Ajabu hata kabla mate kukauka iligunduliwa kumbe ulikuwa ni urongo tena wa mchana. Nyuzi nilizo nazo ni kwamba li-siri-kali limeishaagiza mashumbwengu mengine kama elfu na ushei kutoka Ujepu!

Huu ndiyo mshikamano, amani na utulivu anaosema mkuu. Kumbe na ukondoo na ukuku ni amani na mshikamano! Mnaliwa mnashikamana tu. Badala ya kuwakabili wezi wenu mnaibiana nyinyi kwa nyinyi. Mama anamwibia baba, mtoto anamliza mama, naye analizwa na mwalimu wa tuisheni na mwalimu analizwa na li-sirikali. Hivyo ad infinitum.

Japo walevi wanajipiga vifua kuwa wameanza mwaka, hamna jipya. Jana itaendelea kuonekana bora kuliko leo na leo bora kuliko kesho, hivyo hivyo hadi mwisho wa mchezo anaingia bwana mazingaombwe mwingine.

Mwaka huu umeanza na Tyson Wassila kupopolewa kama kibaka! Kitakachofuatia baada ya walevi kuzinduka. Nani ajuaye? Ingawa mkuu alisema mwaka ulikuwa the best kwangu ulikuwa the worst one.

Chanzo: Tanzania Daima Januari 7, 2009.

No comments: